SERIKALI KUWAPANGIA BEI ELEKEZI VITUO VYA AFYA
SERIKALI imesema itatoa bei elekezi katika sekta ya afya hivi karibuni baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kubariki bei hizo kuanza kutumika kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wa gharama wananchi.
Bei elekezi kwa vituo vya afya zimeshasainiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na baadhi ya vituo vya afya vimeshaanza kutumia bei hiyo.
Aidha, serikali imepanga kuweka utaratibu wa wagonjwa kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikiwa ni hatua ya kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali hiyo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Hamis Kigwangalla wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzindua Matokeo ya Utafiti wa Kutathmini utoaji wa huduma za afya nchini kwa mwaka 2014/2015.
“Bei elekezi ziko mbioni kutoka na baadhi ya vituo wameshaanza kuzitumia kwa sababu zimeshasainiwa na Waziri, sasa hivi tunasubiri baraka za Waziri Mkuu akiziridhia tutazitangaza rasmi,” alisema Dk Kigwangalla.
Akizungumzia msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Muhimbili, Dk Kigwangalla alisema suluhu ya kutatua tatizo la msongamano katika hospitali hiyo ni kuboresha mfumo mzima wa rufaa za wagonjwa kuanzia vituo vya afya ili kuhakikisha wagonjwa wanaoenda kutibiwa Muhimbili ni wale wanaohitaji huduma za kibingwa.
Alisema wataweka utaratibu mgumu wa kwenda kutibiwa Muhimbili ili kuwafanya watu kuona ni rahisi zaidi kupata huduma katika hospitali za chini, badala ya kwenda katika hospitali hiyo ya Taifa.
“Hilo litakuwa suluhisho la kudumu la msongamano, leo hii tumeongeza vitanda Muhimbili lakini na wateja nao wameongezeka na nakuhakikishia kuwa baada ya mwezi mmoja au miwili utakuta wagonjwa wanalala chini tena.
Kama tusipotatua tatizo la msingi la rufaa za wagonjwa kutoka chini kwenda juu, hata tukifikisha vitanda 2,000 kama huku chini patakuwa hapafanyi kazi ipasavyo maana yake wateja watajaa na watalala chini,” alisema Dk Kigwangalla.
Alitaja utaratibu utakaowekwa ili wagonjwa waweze kwenda kutibiwa Muhimbili au kupata huduma katika hospitali za ngazi ya juu, watalazimika kuwa na rufaa kutoka ngazi ya chini na rufaa yao itaeleza wanaenda kumuona daktari gani, idara gani na kama amekubali kuonana na mgonjwa huyo.
Alisema kama hospitali za chini zitaboreshwa, wateja kuona kuwa hospitali hizo zina ubora unaofanana na Muhimbili ili kupunguza msongamano, isipokuwa kwa wagonjwa watakaokuwa wakihitaji huduma za kibingwa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment