MAMBO HATARI YALIYOJIFICHA KWENYE MAFUTA YA KUPIKIA.
Mafuta ya kupikia yanatokana na muunganiko wa kemikali zinazozalishwa na malighafi za asili kama vile seli za mbegu,
matunda ya mimea au wanyama.
Mafuta ni moja ya vinogesho vya chakula vinavyoongeza hamu ya kula hasa yanapotumika kwa kukaanga vitu mbalimbali kama chapati, maandazi, chipsi, mayai, mihogo, vitumbua, kalimati na nyama.
Mafuta pia hunogesha vyakula mbalimbali kwa kuviongezea utamu. Baadhi ya sifa za mafuta ni kutoyeyuka katika maji, uwezo wa kuwaka, kuzalisha nishati, kulainisha ngozi au mitambo pamoja na uwezo wa kutibu baadhi ya maradhi na kutumika kama chakula cha binadamu au wanyama.
Kwa miaka mingi wataalamu wa afya na lishe, wanashauri watu kuhusu athari za ulaji wa kiasi kikubwa cha mafuta.
Ubaya wa mafuta
Ulaji wa mafuta hasa yale yanayotokana na wanyama, yanahusishwa na matatizo mengi ya kiafya kama vile magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani na magonjwa ya mishipa ya damu. Kutokana na sababu hiyo, ulaji wa mafuta mengi umekuwa ukihusishwa na kutokea kwa vifo vya watu wengi duniani.
Katika utafiti mmoja uliochapishwa mapema mwaka huu kwenye jarida liitwalo The Journalof the American Heart Association, watafiti waligundua kuwa watu wengi wanapata magonjwa ya moyo kutokana na kula kiasi kikubwa cha mafuta yatokanayo na mazao ya wanyama.
Pia utafiti huo ulibaini kuwa takribani watu 700,000 sawa na asilimia 10 ya wale wanaokufa kutokana na magonjwa ya moyo duniani kote, chanzo ni kula kiasi kikubwa cha mafuta mabaya kuliko yale mazuri ambayo ni muhimu katika kuimarisha afya.
Dk Dariush Mozaffarian, mmoja wa watafiti hao wa Chuo cha Sera na Sayansi ya Lishe cha Tufts Friedman nchini Marekani anasema, Dk Dariush Mozaffarian, mmoja wa watafiti hao wa Chuo cha Sera na Sayansi ya Lishe cha Tufts Friedman nchini Marekani, anasema ingawa wataalamu wengi wamekuwa wakisisitiza zaidi kupunguza ulaji wa mafuta yatokanayo na wanyama, ipo haja ya kuwapunguzia watu hofu dhidi ya aina zote za mafuta ya kula.
Ni vizuri watu wakaelezwa umuhimu wa kutumia kiasi cha kutosha cha mafuta mazuri yanayoimarisha afya.
Baadhi ya faida za mafuta ya kula katika mwili wa binadamu ni pamoja na kufanya kazi kama chanzo cha nguvu na nishati, kusaidia mwili ili uweze kusharabu vitamini A, D, E na K kutoka katika utumbo na kuzisafirisha sehemu mbalimbali za mwili kwa ajili ya kulinda afya ya mwili.
Vitamini hizi ni muhimu kwa ajili ya afya ya mifupa, mishipa ya fahamu, utendaji mzuri wa seli za kinga ya mwili na uzalishaji wa insulini inayorekebisha kiwango cha sukari mwilini.
Kiasi cha wastani cha mafuta mazuri pia kinasaidia mwili kuzalisha lehemu nzuri ambayo ni muhimu kwa ajili ya kutengeneza vichocheo vya homoni, kuzalisha nyongo, afya nzuri ya kuta za utumbo, utendaji mzuri wa ubongo, kupunguza msongo wa mawazo na ukuaji mzuri wa mwili.
Aina za mafuta
Kimsingi mafuta yanatokana na kemikali zinazojulikana kama triglycerides ambazo zinaundwa na molekuli za glycerin au glycerol pamoja na tindikali.
Mafuta ya kula yamegawanyika katika makundi makuu mawili. Kuna mafuta dabwadabwa; yaani mazito yanayoganda na yale yaliyoko katika hali ya kimiminika wakati wote; yaani yasiyoganda katika joto la kawaida la ndani ya nyumba.
Mafuta dabwadabwa yana kiasi kikubwa cha lehemu na kwa sababu hiyo, huchochea ini lizalishe kiasi kikubwa cha lehemu mbaya. Mafuta yasiyoganda (yaliyo katika hali ya kimiminika wakati wote), yana kiasi kidogo cha lehemu na kwa sababu hiyo, yanapunguza kiasi cha lehemu mbaya na kuongeza nzuri ndani ya damu.
Kwa sehemu kubwa mafuta dabwadabwa au mafuta mazito yanatokana na mazao ya wanyama kama vile nyama yenye mafuta, maziwa, siagi, jibini na mayai.
Kwa mfano, maziwa ya ng’ombe yana asilimia 65.8 ya mafuta mazito, maziwa ya mbuzi yana asilimia 66.4 ya mafuta mazito na maziwa ya binadamu yana asilimia 48.1 ya mafuta mazito na asilimia 51.9 ya mafuta mazuri kwa afya. Hii ni kwa mujibu wa Dk George Pamplona-Roger katika kitabu chake kiitwacho The Ecyclopedia of Foods and Their Healing Power.
Lehemu mbaya inapatikana kwenye mafuta ya nyama nyekundu, ngozi ya nyama nyeupe kama vile ya kuku na mayai hasa yaliyokaangwa au kiini cha yai lililochemshwa.
Wakati wataalamu wa afya wanapendekeza kuwa ulaji wa lehemu kwa siku usizidi miligramu 300 au miligramu 200 kwa watu walioko kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo, yai moja linakadiriwa kuwa na kiasi cha miligramu 200.
Mafuta dabwadabwa pia yanaweza kuzalishwa na mazao ya mimea kama mafuta ya nazi. Ingawa mafuta ya nazi ni mazito, wanasayansi kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa mwaka 2009 nchini Brazil katika jarida la Lipids, wanadai kuwa ni mazuri kwa afya kwa vile tindikali za mafuta katika molekuli zake haziongezi kiasi kikubwa cha lehemu mwilini. Baadhi ya watafiti wanadai kuwa ni mazuri kwa afya ya ubongo na tezi shingo.
Matumizi makubwa ya mafuta dabwadabwa yanasababisha mwili kunenepa kupita kiasi, kwa vile yanakwenda kujikusanya katika misuli, chini ya ngozi na kujishikiza kwenye kuta za mishipa ya damu. Kwa sababu hiyo, mafuta haya yanaweza kuwa chanzo cha magonjwa ya moyo, kiharusi na magonjwa ya mishipa ya damu.
Kwa upande mwingine, mafuta yasiyoganda yanatambulika kuwa ni mazuri kwa afya. Yanaimarisha afya ya mishipa ya damu, moyo na kupunguza kiasi cha lehemu mbaya mwilini. Mafuta haya pia yanasaidia mwili kurekebisha kiasi cha sukari katika damu na tezi shingo kufanya kazi vizuri.
Mafuta haya kwa sehemu kubwa yanatokana na mazao ya mimea kama vile mbegu, kokwa na matunda. Lakini pia mafuta yasiyoganda yanaweza kuzalishwa na mazao ya wanyama kama vile samaki.
Mafuta ya samaki yanadaiwa kuwa ni bora zaidi kwa afya ya moyo na ubongo kutokana na kiasi cha kutosha cha yale mazuri ya omega 3.
Mafuta haya pia yanaimarisha afya ya utumbo, yanazuia na kutibu tatizo la baridi yabisi au jongo pamoja na kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya mwili yanayotokana na mzio kama vile pumu na magonjwa ya mzio wa ngozi. Mafuta haya pia yanapunguza uwezekano wa mtu kupata maradhi ya kipanda uso na wasichana kusumbuliwa na matatizo ya tumbo kuuma wakati wa hedhi.
Mafuta yasiyoganda yanayotokana na nafaka, kokwa na mbegu za mimea na yanaweza kuchakatwa viwandani na kubadilishwa kuwa dabwadabwa yaani mazito.
Mafuta haya yakichemshwa kwa joto kali linalofikia nyuzi 200 za jotoridi na kuongezewa haidrojeni, baadhi ya tindikali takribani asilimia 15, hubadilika na kuwa dabwadabwa kiasi kwamba yanaganda katika hali ya joto la kawaida la ndani ya nyumba.
Hapo ndipo mafuta haya yanakuwa ni mabaya kwa sababu huweza kujirundika ndani ya mishipa ya damu na matokeo yake kufanya njia kuwa ndogo.
Hali hiyo, husababisha moyo kutumia nguvu nyingi kusukuma damu na kusababisha shinikizo kubwa la damu. Hali hiyo ikiendelea huwa rahisi kusababisha magonjwa sugu kama vile kiharusi na kisukari. Pia mafuta yanayojirundika kwenye tishu na nje ya ogani mbalimbali mwilini husababisha uzito kupita kiasi na unene uliokithiri.
Mafuta mazito ambayo watu wengi hupendelea kuyatumia kwa kupaka kwenye mkate, yanaweza kuchochea uzalishaji wa kiasi kikubwa cha lehemu mwilini.
Kwa ajili ya afya bora, jamii inashauriwa kuepuka matumizi ya mafuta yanayoganda na hata kuepuka kula nyama yenye mafuta mengi. Ni vizuri kuongeza utumiaji wa mafuta yasiyoganda hasa yale yanayotokana na samaki pamoja na mimea.
Ni vizuri pia kufanya mazoezi na kazi nzito kila siku ili kupunguza kiasi cha mafuta yanayorundikana katika misuli, chini ya ngozi na katika mishipa ya damu.
Kwa kuzingatia haya, jamii itapunguza mzigo wa magonjwa sugu yasiyoambukiza ambayo yanaathiri ubora wa afya na uchumi wa familia pamoja na taifa kwa ujumla.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment