BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RUNGU LA RAIS MAGUFULI LATUA KWA KISHINDO BENKI KUU YA TANZANIA.



Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameizuia Benki Kuu (BoT) kufanya malipo ya zaidi ya Sh900 bilioni kwa watu na taasisi mbalimbali na kuagiza kufanyika kwa uhakiki ili kubaini wanaostahili kulipwa na taasisi hiyo nyeti ambayo imekuwa ikikumbwa na kashfa za uchotwaji fedha.


Rais, ambaye tangu aapishwe Novemba 5 amekuwa akifanya juhudi za kudhibiti fedha za umma, alitoa zuio hilo jana wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za BoT zilizoko takriban mita 700 kutoka Ikulu.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ikulu jana imeeleza kuwa Rais aliagiza usitishaji wa malimbikizo ya malipo hayo ambayo yalikuwa yameshaidhinishwa na Wizara ya Fedha na kutaka zirejeshwe wizarani kwa ajili ya uhakiki.

“Mpaka Rais Magufuli anatoa agizo hilo, Benki Kuu ya Tanzania ilikuwa katika mchakato wa kufanya malipo ya Shilingi bilioni 925.6 ambazo Wizara ya Fedha ilitoa idhini ya kufanyika malipo,” ilieleza taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Gerson Msigwa.

“Rais ametaka Wizara ya Fedha ifanye upya uhakiki wa malipo hayo, ili kubaini kama walengwa walioidhinishwa kulipwa wanastahili kulipwa au vinginevyo.

“Aidha, Dk Magufuli ameagiza Kitengo cha Madeni ya Nje ambacho awali kilikuwa chini ya Benki Kuu na baadaye kikahamishiwa Wizara ya Fedha, kirejeshwe BoT mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni.”

Alitoa agizo hilo kwenye kikao na watendaji wakuu wa BoT wakiongozwa na Gavana na manaibu wake, wakurugenzi na mameneja.

BoT imekuwa ikikabiliwa na kashfa za uchotwaji fedha za Serikali ambao ulisababisha wanasiasa na watumishi waandamizi wa umma kutimuliwa, kusimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani huku wanasiasa wakivuliwa nyadhifa.

Kashfa ya Sh200 bilioni
Mwaka 2008 iliibuka kashfa ya uchotwaji wa Sh200 bilioni uliofanywa na wanasiasa na wafanyabiashara maarufu nchini kwa kivuli cha uagizaji bidhaa kutoka nje chini ya Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support – CIS).

Kashfa ya Sh133 bilioni za EPA
Mwaka huo pia ilibainika kuwa zaidi ya Sh133 bilioni zilichotwa kutoka Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) kutoka BOT baada ya wafanyabiashara kughushi barua za malipo ya kampuni za nje zilizokuwa zinadai fedha hizo.

Wafanyabiashara wengi maarufu walihusika kwenye uchotwaji fedha hizo na wakati wananchi wakipiga kelele kuitaka Serikali ichukue hatua, Rais alitoa msamaha kwa wachotaji fedha ambao wangezirejesha na akawafikisha mahakamani walioshindwa kufanya hivyo.

Kashfa ya Sh306 bilioni za Escrow
Mwaka juzi, kashfa nyingine iliibuka BoT baada ya kugundulika kuwa zaidi ya Sh306 bilioni zilichotwa kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na kugawiwa kwa mawaziri, majaji, maaskofu, watumishi wa Serikali na wabunge.

Fedha hizo zilifunguliwa akaunti hiyo maalumu kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya nishati baada ya Shirika la Umeme (Tanesco) kuingia kwenye mgogoro wa kimkataba na kampuni binafsi ya ufuaji umeme ya IPTL na kupelekana mahakamani.

Kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wa akaunti ya aina hiyo, fedha hizo zilitakiwa zitolewe kwa ridhaa ya pande zote mbili baada ya kutolewa kwa hukumu, lakini taratibu kadhaa zilikiukwa ikiwa ni pamoja na kutolipwa kwa kodi ya Serikali na kiasi kikubwa cha fedha kutolewa benki kwa mkupuo zikiwa taslimu.

Wafanyakazi BoT
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemuagiza Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu kupitia upya orodha ya wafanyakazi wake na kuwaondoa mara moja wale wote ambao hawana ulazima wa kufanya kazi kwenye taasisi hiyo.

“Haiwezekani tukawa na kundi kubwa la wafanyakazi, wanaolipwa mishahara wakati hata kazi wanazofanya hazijulikani,” Dk Magufuli amekaririwa kwenye taarifa hiyo. 


Benki hiyo imekuwa ikituhumiwa kuajiri kwa kupendelea watoto wa viongozi wa Serikali, baadhi wakituhumiwa kutokuwa na sifa. 

Mwaka jana, watumishi wanane wa BoT walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kughushi vyeti na kutoa haki zisizo sahihi kisheria wakati wakiomba kazi kwenye taasisi hiyo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: