Dar es Salaam. Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemtia hatiani Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed
Kubenea (Chadema) kwa kosa la kumtukana aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, Paul Makonda.
Kutokana na kumtiwa hatiani Kubenea, mahakama hiyo imempa adhabu ya kukaa nje miezi mitatu bila kujihusisha na kosa kama hilo.
Hata
hivyo upande wa Utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala ulisema
unakusudia kukata rufaa kutokana na mahakama hiyo kumtia hatiani mteja
wao.
Kabla ya kupewa adhabu hiyo, Kubenea aliiomba mahakama hiyo
impe adhabu nafuu ambayo itamfanya aendelee kuhudumia wananchi wake.
“Mheshimiwa
Hakimu naiomba mahakama yako tukufu inipe adhabu nafuu ambayo
itanifanya niendelee kutumikia wananchi wangu na kutimiza majukumu yangu
kwa wananchi wangu” alidai Kubenea.
Akisoma hukumu hiyo leo,
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Thomas Simba alikubaliana na ombi la
mshtakiwa huyo na kumhukumu adhabu ya kukaa nje miezi mitatu bila
kujihusisha na kosa kama hilo.
“Kwa kuwa mshtakiwa hii ni mara
yake ya kwanza kushtakiwa mahakamani kwa kosa hili, nakubaliana na
maombi ya mshtakiwa aliyotoa Mahakamani hapa hivyo anastahili kupewa
adhabu ya huruma na mahakama inampa adhabu ya kukaa nje kwa muda wa
miezi mitatu bila kujihusisha na kosa kama hili”alisema Hakimu Simba.
Hakimu
Simba alisema mbali na adhabu hiyo, Kubenea pia atasaini karatasi ya
mahakama ambayo inaonyesha kukubali kwa adhabu hiyo.
“Nafasi ipo wazi kwa upande wa mashtaka kukata rufaa iwapo kama hawajaridhika na adhabu hii” aliongeza hakimu Simba.
Akisoma
hukumu hiyo, hakimu Simba alisema mshtakiwa huyo ametiwa hatiani baada
ya mahakama kujiridhisha na ushahidi wa mashahidi watatu kutoka upande
wa mashtaka waliotoa mahakamani hapo.
Alisema kwa mujibu wa
ushahidi uliotolewa na Shahidi namba moja katika kesi hiyo Paul Makonda,
alidai Desemba 14, 2015 katika kiwanda cha TOOKU Garments Co. Ltd
kilichopo Mabibo External, alisikika Kubenea akimtolewa lugha chafu kuwa
ni kibaka, mjinga, mpumbavu na kwamba nafasi yake ni ya kupewa.
Hata
hivyo katika ushahidi uliotolewa na Kubenea, hakimu Simba alisema
mshtakiwa alidai kuwa alikwenda katika kiwanda hicho kwa lengo la
kutatua mgomo wa wafanyakazi ambao waligoma wakidai nyongeza ya mshahara
wao ambao baadhi yao ni wananchi wake.
Hakimu huyo alisema
baada ya kuchunguza ushahidi wa pande zote mbili, mahakama
imedhibitisha pasina kuacha shaka kuwa maneno hayo yangeleta uvunjifu wa
Amani, na hivyo mahakama ilimtia hatiani kwa lugha ya matusi.
Hata
hivyo upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali ,Mtalemwa
Kishenyi ulidai mahakamani hapo kuwa hauna kumbukumbu za nyuma kuhusiana
na hatia za mshtakiwa.
“Tunaomba mahakama hii itoe adhabu
stahiki kwa mujibu wa kifungu cha 89 (i) (a) cha kanuni ya adhabu, sura
ya 16” alisema Kishenyi.
Kutokana na maelezo hayo, hakimu Simba alitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwa nini asipewe adhabu.
Hali ilikuwa hivi wakati wa kujitetea Kubenea:
“Mheshimiwa
mimi nilienda pale kiwandani katika kiwanda cha TOOKU Garments Co. Ltd
kilichopo Mabibo External, kwa nia njema tu ya kutatua mgogoro wa
wafanyakazi ambao baadhi yao walikuwa ni wapiga kura wangu wa jimbo la
Ubungo”alijitetea Kubenea.
Pia , Mshtakiwa huyo alijitetea kuwa
hakukuwa na fujo zilizojitokeza na pia hakuna na nia mbaya wala miadi
na aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda hivyo anaiomba
mahakama hiyo impunguzie adhabu.
Vile vile alijitetea kuwa bado
wananchi wake wanahitaji awahudumie kwa kuwa ni mbunge wa Ubungo na pia
upande wa Jamhuri umekiri kuwa hana rekodi ya mashtaka hivyo aliimba
mahakama hiyo impunguzie adhabu.
Kutokana na maombi hayo ,
hakimu Simba alifafanua kuwa kesi kama hiyo hukumu yake inaweza kuwa
ni faini au kwenda jela, au kwenda jela bila faini au mahakama inaweza
kumuachia bila masharti yoyoye au kwa masharti maalumu.
“Nimefikira
kosa lilivyotendeka na mazingira yake hivyo nakubaliana na mshtakiwa
kwamba anastahili kupunguziwa adhabu hii, hivyo atatumikia adhabu ya
kukaa nje miezi mitatu kwa masharti ya bila kujihusisha na kosa kama
hili” alifafanua Hakimu Simba.
Katika kesi ya msingi, Kubenea
anadaiwa kuwa Desemba 14, 2015 katika kiwanda cha TOOKU Garments Co. Ltd
kilichopo Mabibo External, alimtolea lugha chafu Makonda kuwa ni
kibaka, mjinga, mpumbavu na kwamba nafasi yake ni ya kupewa.
Hali ilivyokuwa mahakamani:
Kubenea alifika mahakamani hapo asubuhi ya saa mbili huku akiambatana na wakili wake, Peter Kibatala na wafausi wake.
Kubenea alikuwa amevalia suti rangi ya kijivu pamoja na viatu vyeusi na miwani.
Hukumu hiyo imechukua muda wa dakika zipatazo 50 ambapo ilianza saa 6:57 mchana na kukamilika saa 7:47 mchana.
Nje ya mahakama:
Kubenea
alisema amepokea hukumu hiyo kwa moyo mkunjufu ila wanatarajia kukata
rufaa kwa hati ya dharura kupinga mahakama kumkuta na hatia.
Alisema
kesi hiyo inafananishwa na kesi ya kisiasa na kwamba yeye ataendelea
kusonga mbele katika kuwatumikia wananchi wake ambao walimchangua kwa
kura zaidi ya asilimia 87.
“Mimi nimepewa adhabu ya kukaa nje
miezi mitatu bila kufanya kosa kama hili na sio kifungo kwa hiyo
imeipokea vizuri”alidai Kubenea.MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
siasa /
slider
/ MBUNGE WA JIMBO LA UBUNGO AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIEZI MITATU NA MAHAKAMA YA KISUTU KWA KOSA LA KUMTUKANA PAUL MAKONDA DAR ES SALAAM
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment