BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MWL JULIUS NYERERE ALIWEZA LAKINI RAIS DKT JOHN MAGUFULI HAWEZI.


By Nyambo Aariz,Mwananchi 
Pamba zimewekwa masikioni kuhusu tofauti za kisiasa zilizopo Zanzibar. Huo ndiyo utaratibu uliopo na wenye kutakiwa kueleweka.

Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama dola, kimeshinda uchaguzi wa marudio. Chama cha Wananchi (CUF) ni chama kikuu cha upinzani kilisusia na sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) imekufa kama siyo kuuawa.

CCM na CUF wanajua umuhimu wa wao kuelewana na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa ajili ya ustawi wa Zanzibar. Wote wamekataa kujishusha na hayo ni matokeo ya kufikiria mamlaka kuliko ustawi wa wananchi.

Ngoja nikuambie jinsi siasa ilivyo ulevi mbaya japo ni halali kwa matumizi. Wenye kuutumia na kuathirika nao hali zao ni mbaya. Usijaribu kumshauri mwanasiasa aache siasa kabla hajachoka mwenyewe, hatakuelewa.

Mfuatilie mwanasaisa ambaye alikuwa mbunge kwa miaka kadhaa, kisha akashindwa uchaguzi. Ni nadra kukubali matokeo. Anapokaa nje ya ulingo maisha yake hutawaliwa na msongo wa mawazo au hata huzuni.

Mtumiaji wa dawa za kulevya (teja) anapokosa mihadarati hupata hali inayoitwa alosto.

Kwa taarifa yako, siasa zina alosto mithili ya mtumia dawa za kulevya anapokosa vitu vyake. Je, unayajua mateso ya teja anapokosa mihadarati? Basi kutana na mwanasiasa aliyekuwa na nafasi kisha akaipoteza.

Mamlaka yanaweza kumpa ukichaa mwenye mamlaka. Hii ni kwa sababu mamlaka hupumbaza kuliko mihadarati. Watu wengi wazuri walibadilishwa na mamlaka.

Mgogoro wa Zanzibar ni ulevi tu wa kisiasa. Kinachobishaniwa ni vyama na mamlaka. Ingekuwa kinachotazamwa ni ukweli na maridhiano kutokana na hali halisi, mgogoro ungekwisha siku nyingi na maisha yangerejea katika hali ya kawaida.

Badala ya kuwatazama Wazanzibari katika jicho la kwanza, kinachoangaliwa ni vyama. Wanasiasa wanajikita kwenye hatari ya kukosa utamu wa kupata.

Tatizo la Zanzibar ni CCM na CUF, kila upande kutafsiri matokeo katika sura ya faida na hasara.

Siku zote uchaguzi siyo tatizo kama ridhaa ya wapigakura itaheshimiwa. Uchaguzi ni wa wananchi na wao ndiyo huamua kupata au kukosa.

Shida kubwa ya wanasiasa ni kujiangalia wao, wanaposhindwa hujiona wamepoteza. Hicho ndicho chanzo cha uking’ng’anizi. Vyama vinawajibika kwa wananchi. Wananchi ndiyo huamua na uamuzi wao hupaswa kuwa wa mwisho.

Tamaa za wanasiasa ni adui mkubwa wa wananchi. Katika uchaguzi hakuna mwanasiasa mwenye kukosa. Wanaopatia au kukosea ni wananchi kutokana na uchaguzi wao. Masanduku ya kura yakishaongea, huo ndiyo huwa uamuzi. Kama wamekosea waachwe wajute wenyewe.

Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln alipata kusema: “Elections belongs to the people. It’s their decision. If they decide to turn their back on the fire and burn their behinds, then they will just have to sit on their blisters.”

Tafsiri isiyo rasmi ya maneno hayo ni kwamba, uchaguzi ni mali ya watu. Ni uamuzi wao. Kama wanaamua kuigeuza migongo yao kuelekea kwenye moto na kuungua makalio, wao wenyewe ndiyo wanalazimika kukalia majeraha ya moto.

Lincoln alimaanisha kuwa kama uchaguzi umefanyika na wananchi wameamua hutakiwi kupingana na kile ambacho kimeamriwa. Kama wamekosea ni wao wenyewe wataona matokeo ya makosa waliyofanya.

Kwa hali zote ambazo zilijiri Zanzibar, kitendo cha matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kuahirishwa, kisha kuitishwa uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu ni usaliti kwa wananchi.

Kwanza, fedha zilitumika nyingi ambazo ni mzigo mkubwa kwa wananchi. Pili, kama CUF kweli walihusika na dosari (kama kweli zilikuwapo) katika uchaguzi wa awali ni wasaliti.

Tatu, ikiwa CCM na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) waliamua uchaguzi urudiwe kibabe, ni udhalimu wa kiwango cha juu.

Msimamo wa JPM na uwezo wa Nyerere
Kabla ya uchaguzi wa marudio Zanzibar ambao ulisusiwa na CUF, kisha kumpa ushindi wa asilimia 91 Dk Ali Mohammed Shein wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli aliombwa kuingilia mgogoro wa Zanzibar.

Hata hivyo, Dk Magufuli baada ya wito wa wengi alifanya mkutano na wazee wa Jiji la Dar es Salaam na kusema kuwa hataingilia mgogoro huo, kwamba kazi yake ni kulinda amani. Akaongeza kuwa yule atakayeleta vurugu ndiye atashughulika naye.

Msimamo wa Dk Magufuli na shaka ya Zanzibar kuwa na Serikali isiyoungwa mkono na asilimia kubwa ya watu wa Pemba, inaleta sababu ya kumkumbusha namna ambavyo Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alivyomshughulikia Rais wa Pili wa Zanzibar, Abdul Jumbe Mwinyi.

Japo itasemwa kuwa kipindi Mwalimu Nyerere anamshughulikia Mzee Jumbe kilikuwa ni zama za chama kimoja, ukweli unabaki palepale kuwa alisimama kama mkuu wa nchi, kwamba yeye ni mlezi wa pande zote mbili za Muungano; Tanganyika (Tanzania Bara) na Zanzibar (Tanzania Visiwani).

Hivyo, Dk Magufuli anayo mamlaka yote ya kusawazisha matatizo ya Zanzibar. Anatakiwa kuwafanya wananchi wa pande zote mbili waishi kindugu.

Mwalimu Nyerere alimfanya Mzee Jumbe aishi Kigamboni, Dar es Salaam kwa masilahi ya umoja wa Wazanzibari.

Kama ndivyo, Magufuli hawezi kujiweka pembeni na hapaswi kuweka pamba masikioni. Nikumbushe kuwa uhalali wa uongozi siyo utulivu wa wananchi, ni ridhaa.

Mwalimu Nyerere kabla hajafikwa na mauti Oktoba 14, 1999 aliwahi kuuzungumzia mgogoro wa kiasisa Zanzibar kuwa maridhiano hayawezi kufanikiwa bila kumshirikisha Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad kutokana na nguvu kubwa ya kisiasa aliyonayo visiwani humo.

Maneno hayo ya Mwalimu Nyerere ndiyo ukweli wenyewe. Nguvu ya Seif bado ipo hai na kila kitu kipo wazi. Haipaswi kumbezwa hata kidogo.

Tukumbushane ya Angola
Mwaka 1992 ulifanyika Uchaguzi Mkuu wa Angola ikiwa ni baada ya miaka 17 ya vita vya kiraia. Uchaguzi ulikutanisha vyama 11, lakini mchuano ulikuwa mkali kati ya chama tawala cha MPLA na Unita.

Rais Jose Eduardo dos Santos alikuwa anatetea kiti chake akiwa na MPLA dhidi ya Jonas Savimbi wa Unita. Dos Santos ni Rais wa Angola mpaka sasa, alianza kuongoza nchi hiyo mwaka 1979 baada ya kifo cha shujaa wa wakati wote, Augostinho Neto, aliyetawala tangu mwaka 1975 hadi mwaka 1979 alipofikwa na mauti.

Uchaguzi ulipofanyika Santos aliongoza kwa asilimia 49 na Savimbi alipata asilimia 40. Uchaguzi ukatakiwa kurudiwa maana katiba ilitaka mshindi atangazwe baada ya kuzidi asilimia 50.

Uchaguzi wa mara ya pili uliitishwa kati ya Savimbi na Santos ili mmoja aweze kutangazwa mshindi kwa kupata kura zaidi ya asilimi 50.

Mvutano ukatokea, Savimbi alitaka mabadiliko kwenye tume kwa sababu alizodai kuwa Santos aliiba kura. Santos akasisitiza uchaguzi urudiwe hivyo hivyo. Ikawa vuta nikuvute, mwisho Santos akaamua kujitangaza kuwa rais halali na akatawala bila ya kuwapo kwa uhalali wa kidemokrasia.

Uamuzi wa Santos ulikuwa wa kibabe na usiojali damu zisizo na hatia. Pamoja na ukorofi wa Savimbi, ilikuwa ni jambo jema kusikiliza madai yake na kuyafanyia kazi, kwamba tume irekebishwe ili uchaguzi uwe huru na haki.

Ikumbukwe kuwa nchi hiyo ilikuwa imefanya uchaguzi baada ya kusaini mkataba wa kusitisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na ni Santos na Savimbi waliosaini Mei 31, 1991, chini ya usuluhishi wa Serikali ya Ureno. Mkataba huo ulisainiwa baada ya vifo vya maelfu ya raia na wengine wengi kujeruhiwa.



Mwandishi ni mchambuzi wa masuala la kisiasa anapatikana kwa baruapepe:darasalamashauriano@gmail.com na maoni@mwananchi.co.tz

 
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: