Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (kulia) akitafakari alipokuwa akisubiri kusomwa kwa hukumu ya kesi yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo
Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea amehukumiwa kifungo cha nje cha miezi mitatu, akitakiwa kutokufanya kosa la kutumia lugha ya matusi baada ya kutiwa hatiani kwa kumtukana aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Adhabu hiyo ilitolewa jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya Jamhuri kumshtaki ikidai kuwa Desemba 14, mwaka jana katika kiwanda cha Tooku Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo External, Kubenea alimtolea lugha chafu Makonda, ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni kibaka, mjinga, mpumbavu na kwamba nafasi yake ni ya kupewa.
Kabla ya kupewa kwa adhabu hiyo na Hakimu Mkazi, Thomas Simba, Kubenea aliiomba Mahakama impe adhabu nafuu ambayo itamfanya aendelee kuhudumia wananchi wake.
Katika hukumu yake, Hakimu Simba alikubaliana na ombi la mshtakiwa huyo na kumhukumu adhabu ya kifungo cha nje cha miezi mitatu akimtaka kutojihusisha na kosa kama hilo.
“Kwa kuwa mshtakiwa hii ni mara yake ya kwanza kushtakiwa mahakamani kwa kosa hili, nakubaliana na maombi aliyotoa mahakamani hapa hivyo anastahili kupewa adhabu ya huruma na Mahakama inampa adhabu ya kukaa nje kwa muda wa miezi mitatu bila kujihusisha na kosa kama hili,” alisema Hakimu Simba.
Hakimu Simba alisema mbali na adhabu hiyo, Kubenea pia atasaini karatasi ya Mahakama ambayo inaonyesha kukubali adhabu hiyo.
“Nafasi ipo wazi kwa upande wa mashtaka kukata rufaa iwapo hawajaridhika na adhabu hii,” aliongeza hakimu Simba.
Hakimu Simba alisema mshtakiwa huyo ametiwa hatiani baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi wa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka.
Kubenea
Akijitetea mahakamani hapo, Kubenea alisema: “Mheshimiwa mimi nilikwenda katika kiwanda cha Tooku Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo External, kwa nia njema tu ya kutatua mgogoro wa wafanyakazi ambao baadhi yao walikuwa ni wapigakura wangu wa jimbo la Ubungo.”
Alidai kuwa hakukuwa na fujo zilizojitokeza na pia hapakuwa na nia mbaya wala miadi na Makonda hivyo anaiomba Mahakama hiyo impunguzie adhabu.
Alijitetea kuwa bado wananchi wake wanahitaji awahudumie kwa kuwa ni mbunge wa Ubungo na pia upande wa Jamhuri umekiri kuwa hana rekodi ya mashtaka hivyo Mahakama impunguzie adhabu.
Baada ya maombi hayo, Hakimu Simba alisema hukumu ya kesi hiyo inaweza kuwa faini au kifungo; kwenda jela bila faini au Mahakama inaweza kumuachia bila masharti yoyote au kwa masharti maalumu.
“Nimefikiria kosa lilivyotendeka na mazingira yake, hivyo nakubaliana na mshtakiwa kwamba anastahili kupunguziwa adhabu hii,” alisema.
Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala ulisema unakusudia kukata rufaa kupinga hukumu hiyo. Kubenea pia alisema licha ya kupokea hukumu hiyo kwa moyo mkunjufu, anatarajia kukata rufaa.MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM PAULO MAKONDA NAMNA ALIVYOMCHONGEA MBUNGE MAHAKAMANI.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment