WAKUU WA WILAYA 10 WAZUIWA KWENDA NCHINI CHINA KATIKA MAFUNZO YA UCHUMI WA KIMAENEO NA IKULU.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John William Kijazi
Dar es Salaam. Ikulu imefuta safari ya wakuu wa wilaya 10 na wakurugenzi idadi kama hiyo waliotakiwa kwenda China kwa mafunzo ya uchumi wa kimaeneo kuanzia jana, na kuna uwezekano mkubwa ikatangaza uteuzi mpya leo.
Wakuu hao wa wilaya na wakurugenzi wao (majina tunayahifadhi) walikuwa waondoke jana kwa ufadhili wa Serikali ya Watu wa China, lakini habari ambazo Mwananchi imezipata Ikulu iliamua kutotoa kibali, hali inayozidisha ubashiri kuwa uamuzi huo umetokana na kukamilika kwa uteuzi wa wakuu wapya.
Safari hiyo ilishakamilika kwa kiwango kikubwa baada ya kupata visa na wengi wao kuwasili jijini Dar es Salaam tayari kwa safari hiyo, lakini wakalazimika kurejea kwenye vituo vyao baada ya kukosa kibali cha Ikulu ambacho hutolewa na Katibu Mkuu Kiongozi.
Mara tu baada ya kuapishwa Novemba 5 mwaka jana, Rais John Magufuli alitangaza kudhibiti safari za nje za watumishi na viongozi wa umma kwa kuagiza kuwa Ikulu ndiyo itakayotoa kibali baada ya kujiridhisha na umuhimu wa safari hizo kwa Taifa.
Tangu atoe agizo hilo, ni mawaziri wawili tu ambao wameruhusiwa kwenda Vietnam kwenda kujifunza kilimo na viwanda. Mawaziri hao ni Mwigulu Nchemba (Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi) na Charles Mwijage (Viwanda na Biashara).
Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji alikwenda nchini Ethiopia kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa fedha, wakati kwa nyakati tofauto Makamu wa Rais Samia Suluhu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walikwenda Afrika Kusini na Botswana.
Mpaka sasa, Rais Magufuli amefanya safari moja tu ya nje alipokwenda Rwanda kwenye maadhimisho ya mauaji ya kimbari.
Lakini safari ya wakuu hao wa wilaya ilikuwa ifadhiliwe na China, kwa mujibu wa habari hizo na hivyo isingeisababishia Serikali kutumia vibaya fedha za walipa kodi.
Uamuzi huo unaonekana kuzingatia zaidi uteuzi wa wakuu wapya ambao taarifa zinasema unaweza kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa, wakati wa wakurugenzi wa wilaya unatazamiwa kutangazwa baadaye wiki hii au wiki ijayo.
Juhudi za kumpata Katibu Mkuu Kiongozi John Kijazi kuzungumzia suala hilo, hazikuzaa matunda.
Kuanzia saa 7:00 mchana alitafutwa kwa simu na alikuwa hapokei na mara mbili wakati wa jioni alipokea na kukata bila ya kuzungumza lolote, kuashiria kuwa yuko kwenye kazi nyingine muhimu.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alikiri kuwapo kwa safari hiyo, lakini akasema hajui kama imeidhinishwa na Ikulu kwa kuwa si muhusika.
“Katika hatua za awali nilisaini safari hiyo kuwaruhusu waende China, lakini sijui kama wamenyimwa kibali kwa sababu hilo si suala la ofisi yangu,” alisema Waziri Simbachawene.
Kama ni kweli, alifafanua Simbachawene, inaweza kuwa ni kutokana na umuhimu wao wa kuwatumikia wananchi kwenye maeneo wanayotoka. “Hawawezi kuondoka na kuziacha wilaya zao ilhali wao ndiyo waangalizi,” alisema Simbachawene.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa alisema yupo nje ya ofisi hivyo hana taarifa kamili.
“Nilikuwa msibani na hivi sasa nipo safarini natoka Njombe. Nikifika ofisini nitakuwa na majibu sahihi,” alisema Msigwa na kukumbusha kuwa aliyekataza safari za nje ni Rais na hakuna anayeweza kufanya kinyume na hilo.
“Inawezekana mamlaka imeona hakuna tija ya kuwaruhusu waondoke hata kama wanalipiwa na Serikali ya China,” aliongeza.
Rais aliwasimamisha kazi watumishi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kosa la kukaidi agizo lake la kutosafiri bila kupata kibali. Watumishi hao ni Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani, Rukia Nikitas na Mary Mosha.
Sakata la wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri limekuja katika kipindi ambacho Rais anasubiriwa kutangaza safu yake mpya kwenye uongozi wa wilaya baada ya kukamilisha wakuu wa mikoa mwezi uliopita.
Akiwa Chato mkoani Geita, Rais aliwataka wakuu wa wilaya kuchapa kazi badala ya kuwa na woga wa kutoteuliwa akisema uchapaji kazi ndio utawafanya waendelee kuwapo kwenye nafasi zao.
Rais pia amekuwa akitoa maelezo kadhaa yanayoonyesha atafanya uteuzi kwa kutumia vigezo hivyo, hasa suala la elimu ambayo inakabiwa na tatizo kubwa la uhaba wa madawati na vyumba na majengo, kipindupindu, njaa, migogoro ya ardhi na watumishi hewa.
Baadhi ya wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuueleza umma jinsi wanavyofanya kazi kutatua changamoto zinazozikabili jamii wanazoziongoza, huku mmoja wao akiwa ameshamuomba Rais asimfikirie kwenye uteuzi mpya.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment