
Utafiti huo uliofanyika kwa watu 1,811 wa Tanzania Bara pekee, umebainisha kwamba asilimia 91 wametoa pendekezo kwamba kabla Serikali haijalifungia gazeti lolote, basi vielelezo vya maamuzi hayo vitolewe mahakamani ili chombo hicho ndiyo kitoe uamuzi.
Januari, mwaka huu, Serikali ililifungia moja kwa moja gazeti la Mawio kwa kosa la uchochezi. Mwaka 2012, gazeti la MwanaHalisi lilifungiwa pia na kufunguliwa mwaka huu. Kadhalika, Serikali ilifungia kusambazwa kwa gazeti la The EastAfrican.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo jana, Meneja wa Sauti za Wananchi, Meliana Omengo alisema wananchi wanadai Serikali iruhusiwe kuweka vizuizi pale itakapoona kutolewa kwa taarifa ni muhimu kwa usalama wa taifa.
“Asilimia 78 ya wananchi wanasema wangekuwa na uhuru wa kupata taarifa, ingepunguza vitendo viovu vya rushwa. “Asilimia 60 wamesema Serikali iwe na uwezo wa kuzuia taarifa za usalama wa taifa,” alisema Omengo.
Alisema asilimia 55 walisema vyombo vya habari vinapaswa kuchunguza na kutoa taarifa mara kwa mara, kuhusu vitendo vya rushwa na maovu ya Serikali.
Kuhusu upatikanaji wa habari, Omengo alisema wananchi wengi hupata taarifa kwa kutembelea taasisi za umma. Alisema asilimia 74 hupata taarifa kwa kutembelea taasisi za umma, asilimia 14 simu na asilimia moja tu kutembelea tovuti zao.
Alisema wananchi wengi hawafuatilii kuhusu huduma za umma au jinsi taasisi za umma zinavyoendeshwa.
Akichangia kuhusu utafiti huo, Mwakilishi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF), Ernest Sungura alisema anashangaa kuona watu wengi wanatumia simu za mkononi, lakini hawaamini mitandao ya kijamii.
Alisema ni wakati wa vyombo vya habari kujielekeza kwenye mitandao ya kijamii ili kutoa habari za uhakika.
Alisema vyombo vya habari visitegemee kupata taarifa kutoka kwa wanasiasa, bali wafanye uchunguzi na kuibua uozo.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment