WANYWAJI WA POMBE ZINAZOHIFADHIWA KATIKA VIROBA KUATHIRIKA BAADA YA SERIKALI KUSHUSHA RUNGU KALI
Dar es Salaam. Mifuko ya plastiki inayofungasha pombe maarufu kama ‘viroba’ imepigwa marufuku na Serikali kuanzia mwakani.
Sambamba na hilo Serikali pia, imepiga marufuku moja kwa moja utengenezaji, usambazaji, uingizaji nchini wa mifuko ya plastiki kuanzia mwaka huo.
Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliwaambia wanahabari jana sehemu kubwa mifuko hiyo inatolewa bure imekuwa ikichangia uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kikubwa.
Wakati Makamba akiyasema hayo, Februari mwaka huu Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina aliondoa zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki akisema kuwa itaziweka rehani ajira za Watanzania wanaofanya kazi kwenye viwanda vinavyotengeneza mifuko hiyo.
Pia, Mpina alisema itapunguza kasi ya uwekezaji wa viwanda vilivyowekeza katika bidhaa hiyo.
Akizungumza katika siku ya Mazingira Afrika, Mkurugenzi wa Mazingira, Dk Julius Ningu alisema maamuzi hayo yamelenga kulinda viwanda vilivyoajiri mamia ya Watanzania, tofauti na nchi nyingine zinazotegemea wazalishaji wa nje ya nchi.
Makamba akizungumzia uamuzi mpya wa kuzuia mifuko ya plastiki, alisema matumizi ya mifuko inayofungashia vileo na inayotumika katika matumizi mengine husambaa na kuchafua mazingira.
Alisema mifuko ya plastiki inatajwa kuziba mifereji na kusababisha mafuriko na athari nyingine za mazingira.
“Leo (Jana), tumeamua kutangaza ili kuwaanda wahusika wasiendelee kuwekeza katika mifuko hii badala yake wasubiri utaratibu mwingine utakaowekwa na Serikali,” alisema Makamba na kuongeza kuwa:
“Asilimia kubwa ya uchafu kwenye nyanzo vya maji, mito, maziwa na fukwe za bahari ni mifuko ya plastiki.”
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema Serikali inakamilisha majadiliano ya ndani na baadaye itawahusisha wadau kuhusu dhamira ya kupiga marufuku ya moja kwa moja mifuko hiyo.
Alifafanua kwamba Serikali itatoa muda kwa walioajiriwa, kujiajiri na kuwekeza kwenye biashara ya mifuko hiyo ili kujiandaa kuacha shughuli hizo na badala yake itawezesha mazingira ya utengenezaji na upatikanaji wa vifungashio mbadala.
“Kwa wanaotengeza mifuko hii na kuiuza katika soko la nje hatuna tatizo nao waendelee. Ila kwa soko la ndani hawataruhusiwa kufanya hivyo. Zuio hili litakuwa la kisheria siyo kwa maneno,” alisisitiza Makamba.
Aliongeza kuwa katika kuonyesha Serikali imedhamiria kupambana na hali hiyo wizara yake imeamua kutuma timu ya watu watano kwenda Rwanda kujifunza namna bora ya kudhibiti matumizi na kuzuia mifuko hiyo tangu mwaka 2008.
Waziri huyo alitoa wito kwa watengenezaji, wasambazaji na waagizaji wa mifuko hiyo kujiandaa na zuio hilo na katika siku zijazo Serikali itatoa utaratibu na maelekezo ya tarehe ya kuanza zuio huku taratibu nyingine za kina zikifuata ili kuondoa mkanganyiko.
Katika hatua nyingine, Makamba alisema maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5 kila mwaka hayatafanyika kitaifa badala yake wizara imewaelekeza wakuu wa mikoa kufanya maadhimisho katika maeneo yao.
“Tumewapa miongozo kuhusu utekezezaji wa shughuli hizo za maadhimisho zinazolenga kutoa hamasa ya hifadhi ya mazingira hususan nyanzo ya maji amabayo ni muhimu kwa viumbe hai,” alisema Makamba.
Kwa mujibu wa Makamba, kauli mbiu ya mwaka huu kitaifa juu ya maadhimisho hayo ni ‘ tuhifadhi vyanzo vya maji kwa uhai wa taifa letu’aliwashauri na kuwataka Watanzania kutumia siku hiyo kupanda miti, kudhibiti uchomaji wa misitu
Ofisa Mwandamizi Mazingira wa Nemc, Arnold Kisagala alisema nusu ya mifuko ya plastiki nchini inazalishwa na kuingizwa kutoka nchi jirani ya Kenya.
Alisema agizo la Waziri Makamba litawezekana, lakini linahitaji ushirikiano kutoka kwenye sekta zingine kwa kuwa viwanda vingi vya mifuko ya plastiki vipo Kenya.
NEMC tayari tulishaanza mazungumzo na wazalishaji kuhusu mifuko ya plastiki,” alisema.
Wafanyabiashara wanena
Wafanyabiashara kwenye maduka ya nguo na ya vyakula walisema kama Serikali imeamua hayo inatakiwa ije na suluhisho la vifungashio vingine.
Kulwa Kassim, mmiliki wa duka la vyakula lililopo Mbezi, alisema kama Serikali haitaki mifuko ya plastiki ni lazima watafute mbadala wake.
Mmiliki wa duka la nguo eneo la Kariakoo, Jamal Hamsini alisema mifuko hiyo imekuwa ikipigwa marufuku, lakini zuio hilo halidumu bali ni maneno tu.
“Tangu walipoanza kupiga marufuku si leo, labda safari hii wameamua kweli, ngoja tuone,” alisema.CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment