BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MARUFUKU KUWAPELEKEA CHAKULA WAGONJWA HOSPITALI YA TAIFA YA MUHIMBILI

Dar es Salaam. Kwa waliokuwa wakiwapelekea chakula wagonjwa wao Muhimbili, sasa waandae Sh6,000 kwa siku.

Sasa hawataruhusiwa tena kupeleka chakula kwa kuwa hospitali hiyo ya Taifa imeanzisha utaratibu mpya wa kuhudumiwa wagonjwa wanaolazwa.

Kuanzia Julai Mosi, ndugu watakaokuwa na wagonjwa Muhimbili watalazimika kulipa Sh6,000 kila siku kwa ajili ya huduma ya chakula.

Utaratibu huo ulitangazwa jana na mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano (MNH), Aminiel Aligaesha aliyesema tayari hospitali hiyo imeingia ubia na mzabuni wa kutoa huduma hiyo ya chakula kwa wagonjwa.

Kutokana na mabadiliko hayo, muda wa kutembelea wagonjwa utabaki saa 12.00 asubuhi hadi saa 1.00 asubuhi na saa 10.00 jioni hadi saa 12.00 jioni.

Muhimbili haitaruhusu ndugu ambao watataka kupeleka chakula mchana kama ilivyokuwa awali na hata kuona wagonjwa mchana kumefutwa.

Kwanini hatua hiyo
Aligaesha alisema hospitali hiyo inataka kujikita katika majukumu yake ya msingi ambayo ni kushauri, kuchunguza na kutibu.

“Hospitali inataka kuwaondolea adha ndugu wa wagonjwa ambao wamekuwa wakiingia gharama kubwa kusafiri mara tatu kwa siku kupeleka chakula.

Alisema kwa kukadiria ndugu hutumia kati ya Sh6,000 na Sh10,000 kulingana na anapoishi kupeleka chakula hospitalini na kuwa huacha shughuli za maendeleo kwa ajili ya kuwaona wagonjwa mara kwa mara,” alisema Aligaesha.

Pia, alisema wameamua kuchukua uamuzi huo kupunguza msongamano wa watu ndani ya hospitali hiyo kubwa nchini kati ya saa 12.00 asubuhi mpaka saa 12.00 jioni.

Alisema msongamano wa watu huathiri utoaji huduma, hasa nyakati za mchana, kutokana kuingilia utendaji wa watalaamu wanapokuwa wakizungukia wagonjwa.

Alisema msongamano pia ni changamoto katika masuala ya kiusalama, kwani miongoni mwa watu wanaoingia Muhimbili kwa ajili ya kuona wagonjwa, wapo waliokuwa wanaingia kwa lengo la kufanya uhalifu, kama wizi wa mali za taasisi hiyo na vifaa vya magari.

Akizungumzia utaratibu huo, mkurugenzi mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria alihoji kama uongozi utaweza kutoa chakula kwa utashi wa wagonjwa.

“Kwanza, kila mgonjwa ana chakula anachokipenda na wanaolazwa ni wa umri tofauti. Sijajua kama uongozi wa hospitali hii wataandaa chakula baada ya kuwasikiliza wagonjwa wanataka nini kwa siku hiyo. Jambo hilo linahitaji mjadala mpana,” alisema.

Alisema huduma katika hospitali hiyo zinalalamikiwa kila kona, lakini badala ya kuzitatua linatolewa wazo la kuanza huduma nyingine.

“Nadhani wangeanza kwanza kuboresha huduma zao na baada ya hapo ndiyo waongeze huduma nyingine,” alisema Kiria.

Hata hivyo, mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga wa Muhimbili, Agness Mtawa alisema tayari timu ya wauguzi ipo kwenye mafunzo maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa.

“Tunaendesha semina mbalimbali kwa ajili ya kukumbushana kuhusu majukumu yetu ya msingi na namna tutakavyotekeleza kazi ya kugawa chakula kwa wagonjwa,” alisema.

“Tunajua wapo ambao watatakiwa kulishwa na haya yote tumejipanga, hivyo ndugu watatakiwa kuja kuwaona tu.”

Utaratibu wenyewe
Aligaesha alisema mzabuni aliyeteuliwa ndiye atakayepika chakula kwa wagonjwa wote waliolazwa na atatayarisha, kukipeleka na kukikabidhi katika wodi husika.

Alisema jukumu la kumpa mgonjwa kifungua kinywa, chakula cha mchana na jioni linabaki kwa hospitali, huku wagonjwa wakipewa milo mitatu kwa siku, yaani asubuhi, mchana na jioni.

“Wagonjwa watagawiwa chakula na muuguzi wa zamu ambaye atahakikisha wagonjwa wote wamepata chakula kufuatana na mahitaji yaliyowasilishwa jikoni,” alisema Aligaesha.

Malipo ya chakula
Alisema mgonjwa aliyelazwa kwa siku tano atatakiwa kulipa cha Sh50,000, kati ya hizo Sh10,000 zitakuwa ni gharama ya kumuona daktari, Sh10,000 ya kulazwa na bei ya chakula itakuwa Sh30,000 sawa na Sh6,000 kwa siku.

Kwa sasa hospitali hiyo inatoa chakula kwa wagonjwa ambao wamepata rufaa kutoka hospitali za nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Kwa wastani, idadi ya wagonjwa 650 hupatiwa chakula kwa siku. Gharama ya kuwalisha wagonjwa hao ni wastani wa Sh1.8 bilioni kwa mwaka, sawa na Sh150 milioni kwa mwezi kwa chakula pamoja na gharama nyingine kama vile za nishati.

“Hii ina maana kwamba takribani wagonjwa kati ya 600 na 700 ambao rufaa zao ni kutoka Hospitali za Dar es Salaam, walikuwa hawapati chakula kutoka hospitalini na ilibidi ndugu zao wawaletee chakula,” alisema. 


Hata hivyo, alisema hospitali ilikuwa inawapatia chakula iwapo ndugu zao wakishindwa kuwaletea.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: