Kahama/Dar es Salaam. Mzimu wa intelijensia ya polisi umeendelea kuwaandama Chadema, huku ukisababisha Mji wa Kahama mkoani Shinyanga kusimama kwa saa kadhaa baada ya Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya viongozi wa chama hicho na wanachama wao waliokuwa katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa ziara ya Operesheni Demokrasia. Baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana, polisi walipiga marufuku mikutano yote ya siasa baada Chadema kutangaza kuzunguka nchi nzima kuwashukuru wananchi kwa kura walizompigia mgombea wao wa Urais, Edward Lowassa.
Hatua hiyo ya jana ya polisi imekuja baada ya CCM kutangaza kupita maeneo yote itakakopita Chadema ‘kufuta nyayo zake’ kujibu hoja zao, hatua ambayo polisi kupitia Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya amedai inaweza kusababisha vurugu.
Wakati hayo yakijiri Kahama, jijini Dar es Salaam mmoja wa wabunge waliosimamishwa, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) jana aliitwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kuhojiwa.
Jumapili iliyopita, Zitto alihutubia mkutano wa chama chake jijini Dar es Salaam na kutoa matamko mbalimbali.

0 comments:
Post a Comment