Mwandishi mkongwe, Thadei Hafigwa kulia akifanya mahojiano na mmoja wa wakazi wa Tambuu halmashauri ya Morogoro Vijijini mwaka 2009.
KUTOKA KWENYE KUMBUKUMBU ZA MTANDA BLOG ZA DEC 17, 2009.
Kwa mujibu wa wazee kadhaa waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi katika kijiji cha Mtombozi,wilaya ya Morogoro vijijini wamebainisha ya kuwa viongozi hao wa jadi walikuwa na ushindani wa kimadaraka na kupelekea kukutana katika miamba ya mawe iliyopo katika makutano ya mito ya Mtombozi na Mngazi na kuunda mto Mvuha.
Mzee John George (70) mkazi wa kitongoji cha Tambiko alisema kwa mujibu wa mapokeo kutoka kwa wazee Mkoa wa Morogoro ina historia kubwa kutokana na kuwepo kwa mambo mengi ya kale ambayo hayajatangazwa na kufahamika na wengi.
Alisema kumbukumbu za kale kutoka kwa wazee zinaonesha kuwa karne nyingi zilizopita viongozi wa Jadi chifu Kingalu wa Kwanza na Hega waliwahi kushindana nani mwenye uwezo na nguvu za kutawala jamii inayoishi milima ya uluguru ambapo katika ushindani huo walilazimika kuoneshana umwamba wa kuchonga mwamba wa jiwe kwa kutumia kisigino mithili ya usolo au mchezo wa bao.
Aidha mwandishi wa gazeti hili aliweza kufika katika kitongoji cha usolo katika Kijiji cha Tambuu na kushuhudia vishimo vilivyosadikiwa kuchimbwa kwa kutumia ncha ya visigino vya viongozi wa Jadi hao Chief Kingalu na Chief Hega katika ushindani wao.
Katika ushindani huo kwa kujibu wa taarifa zilizopatikana katika eneo la tukio zinaeleza kuwa Kingalu aliweza kumzidi mwenzake maarifa kwa kushimba vishimo 36 huku Hega akiambulia vishimo 16 pekee ambapo baada ya ushindani huo waliweka mipaka ya kiutawala Hega aliweza kumiliki eneo la ardhi kuelekea Kisaki ambapo Kingalu aliendelea kutawala eneo la Kinole hadi leo.
Mtawala wa sasa wa jamii ya Waluguru ni Chifu Kingalu Mwana Banzi wa 14 anaishi katika Kitongoji cha Kinole Morogoro Vijijini huku mila na desturi zikiendelea kuenziwa kwa kufanya tambiko kila mwaka kwa kuomba ustawi wa jamii.

0 comments:
Post a Comment