Juma Mtanda, Morogoro.
Timu ya soka ya Stend Misuna FC ya Singida imeibuka kinara katika ligi ya mabingwa wa mikoa baada ya kuizidi maarifa Namungo FC ya Ruangwa kutoka Lindi iliyokuwa ikiongoza muda mrefu katika msimamo wa ligi hiyo kituo cha Morogoro.
Namungo FC inayonolewa na kocha mkuu, Amri Saidi ilipoteza mahesabu katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Stend Bagamoyo mkoani Pwani kwa kulazimishwa sare ya 0-0 huku mshambuliaji wake, Emmanuel Thomas alitolewa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kibao usoni mchezaji wa Stend Bagamoyo na mwamuzi wa kati, Athman Ladhi kumpa adhabu hiyo.
Mchezo huo uliofanyika majira ya saa 8 mchana na kuipunguzia presha timu ya Stend Misuna FC iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Sifa Politani ulifanyika majira ya saa 10 jioni huku ukitawaliwa na mashambulizi hafifu kwa upande wa Stend Bagamoyo.
Vinara hao katika kituo cha Morogoro, Stend Misuna FC ni kama ilikuwa inaiombea dua mbaya timu ya Namungo FC imalize mchezo wake kwa sare au kupoteza mbele ya Stend Pwani na dua hiyo kutimia kwa sare ya 0-0 baada ya dakika 90 kumalizika.
Bao la Stend Misuna lilipachikwa wavuni na mshambuliaji, Saidi Mjie dakika 23 akitumia uzembe wa mlinzi wa Sifa Politani, Ally Saidi aliyeshindwa kumdhibiti mfungaji na kumfunga kirahisi kipa, Idrisa Ramadhan.
Washambuliaji wa Sifa Politan FC walishindwa kuonyesha kandanda safi licha ya kufika eneo la hatari la wapinzani wao mara kwa mara hata ilipotokea mipira ya adhabu ndogo nje ya 18 ilipigwa mipira hafifu iliyokuwa inaokolewa na wachezaji wa Stend Misuna ama kipa na kuufanya mchezo huo kukosa mikimiki ya ushindani.
Akizungumza na gazeti hili mjini hapa, Msimamizi kutoka TFF kituo cha Morogoro, Charles Ndagala alisema kuwa Stend Misuna FC ndio mshindi wa kwanza wa kituo hicho huku michezo ya kumalizia panzi leo majira ya saa 10 kati ya Mbuga FC ya Mtwara na Makumbusho FC ya Dar es Salaam.
Ndagala alisema Stend Misuna FC imemaliza na pointi 12 wakati nafasi ya pili ikishikwa na Namungo FC yenye pointi 11 na Sifa Politani ina pointi sita.
Stend Bagamoyo imemaliza na pointi tano wakati timu ya Muheza United FC ambayo ilijitoa ikiwa na pointi nne.
Mabadiliko ya msimamo wa ligi hiyo yanatarajia kujitokeza katika mchezo baina ya timu ya Makumbusho yenye pointi nne na Mbuga FC poiniti mbili katika mchezo wao wa kukamilisha ratiba leo katika uwanja wa jamhuri Morogoro na kuhitimisha ligi hiyo.

0 comments:
Post a Comment