Juma Mtanda, Morogoro.
Mshindi wa kwanza ligi ya mabingwa wa mikoa kituo cha Morogoro msimu wa mwaka 2015/2016 pamoja na mshindi wa nafasi ya pili huenda wakakumbwa na adhabu kali kutoka shirikisho la soka la Tanzania (TFF) baada ya kudaiwa kuwachezesha baadhi ya wachezaji waliokosa sifa za kucheza michezo ya ligi hiyo iliyomalizika hivi karibuni.
Akithibitisha kupokea kwa rufaa hizo, Msimamizi wa ligi ya mabingwa wa mikoa kutoka TFF kituo cha Morogoro, Charles Ndagala alisema kuwa amepokea rufaa mbili za timu ya Makumbusho FC ya Dar es Salaam na Stendi Bagamoyo ya Pwani dhidi ya wapinzani wao.
Ndagala alizitaja timu zilizokatiwa rufaa kuwa ni Stend Misuna FC iliyoshika nafasi ya kwanza na Namungo FC nafasi ya pili kwa madai ya kuchezesha wachezaji waliokosa sifa za kucheza ligi ya mabingwa wa mikoa na rufaa hizo tayari amewasilisha katika shirikisho la soka Tanzania (TFF).
“Ni kweli nimepokea rufaa mbili ikiwemo timu ya soka ya Makumbusho FC ikidai bingwa katika kituo cha Morogoro, Stend Misuna FC imechezesha wachezaji waliocheza ligi daraja la kwanza katika msimu mmoja na Namungo nayo imekatiwa rufaa na Stend Bagamoyo kwa madai hayo hayo.”alisema Ndagala.
Akizungumza na gazeti hili juu ya kukata rufaa hiyo, Kocha msaidizi wa timu ya Makumbusho FC, John Mashaka alisema wamekata rufaa kupinga timu ya Stend Misuna FC kuwatumia wachezaji watatu ambao tayari wamecheza ligi daraja la kwanza katika msimu wa mwaka 2015/2016 na wachezaji hao hao kutumika katika ligi ya mabingwa wa mikoa kinyume na kanuni za TFF.
Mashaka alisema kuwa wana ushahidi usio na shaka kuwa Stend Misuna imevunja kanuni za TFF za mchezaji mmoja kutochezea ligi mbili katika msimu mmoja na kudai kuwa lakini timu ya Stend Misuna FC imefanya hivyo.
“Kuna wachezaji watatu wa Stend Misuna FC wamecheza ligi daraja la kwanza na ligi hii ya mabingwa wa mikoa wachezaji hao hao wamecheza kituo cha Morogoro ikiwa ni kinyume na kanuni za ligi ya mabingwa wa mikoa.”alisema Mashaka.
Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Hamis Mayombo ambaye anadaiwa kuchezea ligi daraja la kwanza na kutumia jina la Stanley Msahila akiwa na leseni No:920804005, Costa Byryani ligi daraja la kwanza akitumia jina la Brown Chalamila leseni No:921004001 ambao wachezaji hao wanadaiwa kuchezea timu ya Kurugenzi FC ya Iringa.
Wengine ni Fred John Razaro kwenye ligi daraja la kwanza amedaiwa kuchezea Singida United akitumia jina la Adolfu Athony akiwa na leseni No:950725003.alisema Mashaka.
Ushindi hauwezi kuwa na thamani iwapo umepatikana katika njia isiyo halali au kwa udanganyifu.alisema Mashaka akinuu kanuni ya 30 ya ligi hiyo.
“Stend Misuna FC haifai kuthaminiwa ushindi wowote walioupata kwa udanganyifu na kutokana na vielelezo tulivyowasirisha TFF, inafaa ipokonywe pointi kwa ajili ya udanganyifu kama ilivyowahi kupokonywa ushindi timu zzilizofanya makosa na kuondolewa katika mashindano.”alisema Mashaka.
Kwa upande wa Stend Bagamoyo FC imemkatia rufaa mchezaji wa Namungo FC, Emmanuel Thomas anayedaiwa kucheza ligi daraja la kwanza katika timu ya Kurugenzi FC ya Iringa.
Emmanuel Thomas anadaiwa kutumia jina la Imani Vamwanga akiwa na leseni No:930909003 ligi daraja la kwanza.
Kutokana na msimamo wa ligi ya mabingwa wa mikoa kituo cha Morogoro, Stend Misuna FC imeongoza kwa kuwa na pointi 12 wakati nafasi ya pili ni Namungo FC yenye pointi 11 huku Sifa Politani FC na Makumbusho FC zikiwa na pointi sita zikitofautiana mabao ya kufungwa na kufunga.
Stend Bagamoyo imemaliza na pointi tano wakati Muheza United FC ambayo ilijitoa ikiwa na pointi nne na Mbuga FC ikiambulia poiniti mbili na kuburuza mkiani.

0 comments:
Post a Comment