
WAKATI wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametoka kupinga kwa nguvu zote kukatwa asilimia tano ya viinua mgongo vyao kama kodi, jana waliitaka serikali kuongeza Sh. 50 katika kila lita ya mafuta ya diseli na petroli.
Kupanda kwa bei ya nishati ya diseli na petroli, kwa vyovyote, kutaendana na ongezeko kubwa la gharama za maisha ikiwamo kupanda kwa bei za vyakula na usafiri.
Juzi, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alikatiza malalamiko ya wabunge wa chama hicho kwa kutaka kuwapo kwa mjadala wa makato ya kodi katika kiinua mgongo cha wawakilsihi hao wa wananchi baina ya serikali na wabunge, badala ya kendelea kulia hadharani kama ilivyokuwa.
Serikali inakusudia kukata kodi ya asilimia tano katika kiinua mgongo cha Wabunge kisichotokana na mishahara.
Mwaka jana kila mbunge alilipwa Sh. milioni 230, baada ya kuvunjwa kwa Bunge la 10, na kama watapata angalau kiasi hicho pia mwaka 2020, kila mbunge atabakiwa na Sh. milioni 218.5.
Akichangia mjadala wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2016/17 juzi, Lusinde alisema binafsi anakubali kukatwa kodi lakini akashauri wabunge kutoendelea kulijadili suala hilo ndani ya Bunge.
Wabunge wametaka kila lita ya mafuta ipande kwa Sh. 50 zaidi ili fedha zitakazopatikana zielekezwe katika miradi ya maji vijijini na kuondoa adha ya ukosefu wa huduma hiyo.
Wakichangia mjadala wa Bajeti bungeni jana mjini Dodoma, Wabunge wa CCM walisema katika bajeti ya mwaka jana fedha zilizotengwa kwa ajili ya maji na umeme, zilipelekwa mjini zaidi na hivyo wananchi kuendelea kutaabika.
Mbunge wa Magu, Boniventure Kiswaga alisema utetezi wa serikali kuwa kuongeza fedha kwenye mafuta ni kusababisha mfumuko wa bei, siyo kweli kwa kuwa zitakwenda kuwezesha upatikanaji wa maji vijijini.
Kiswaga alisema iwapo serikali itakataa ombi la kuongeza Sh. 50 katika kila lita ya mafuta, atashika shilingi kwenye bajeti isipite huku akiomba wabunge wenzake kumuunga mkono.
Serikali haikuongeza kodi ya petroli katika bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango Juni 8, kwa nia ya kutowatwisha mzigo mkubwa zaidi wananchi.
Kiswaga alisema sera ya maji inataka kila mwananchi kupata maji umbali wa mita 400 ifikapo mwaka 2020 na kwamba ni lazima jitihada hizo zianze sasa ili kufikia malengo ya kupeleka maji katika vijiji.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba, alisema tatizo la maji vijijini ni kubwa na kwamba namna ya kutatua ni kuhakikisha kiasi hicho kinaongezwa kwenye mafuta ili kuwezesha serikali kupata mapato ya kupeleka miradi ya maji.
Mbunge wa Morogoro Kusini, Omari Mgumba alisema mzigo wa kukosa maji kwa muda mrefu umebebwa na wananchi na kwamba hofu ya serikali kuongeza kiasi hicho kwenye mafuta haina mashiko kwani lengo ni kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama.
Akiwasilisha mapendekezo ya bajeti, Dk. Mpango, alisema serikali imetenga Sh. trilioni 1.02, sawa na asilimia 4.8 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa, kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama nchini.
Alisema baadhi ya shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya maji mijini na vijijini, ulipaji wa madeni ya wakandarasi na utekelezaji wa shughulinza mfuko wa maji.
Katika bajeti ya mwaka jana, serikali iliongeza Sh. 100 kwa kila lita ya petroli na dizeli na Sh. 150 kwa lita ha mafuta ya taa, ambazo zilielekezwa kwenye umeme vijijini na baadhi kwenye huduma ya maji.
MAUMIVU TAYARI
Tayari Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na maumivu kwa wananchi wa kawaida baada ya kujikita kwenye vyanzo vya mapato kama tozo za vinywaji baridi, juisi, vilevi, sigara na gesi asilia.
Vyanzo vingine vitakavyoongeza makali ya maisha ni kuongezwa kwa ushuru wa namba binafsi za magari na kuongeza tozo ya asilimia 10 katika miamala ya simu.
Waziri wa Fedha na Mipango alisema katika mwaka ujao wa fedha, watatoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma wa simu katika kutuma na kupokea fedha, badala ya ushuru huo kutozwa tu kwenye kutuma fedha pekee. Dk. Mpango alisema katika utaratibu wa sasa, baadhi ya kampuni zinazotoa huduma zimetumia mwanya kwa kuhamishia sehemu kubwa ya ada hizo kwenye kupokea fedha na hivyo kuwa nje ya wigo wa kodi.NIPASHE

0 comments:
Post a Comment