
Dar es Salaam. Wakati Yanga ikiwa Uturuki kwa maandalizi ya mechi ya awali ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji ameibuka na kusema kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara hadi kuingia hatua ya makundi ya kombe hilo, kumeitia hasara timu yake na kuiongezea mzigo wa Sh2.5 bilioni.
Yanga iliyoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na Al Ahly ya Misri na kuhamia Kombe la Shirikisho Afrika ambako imefuzu kwa hatua ya makundi.
Yanga itakwaana na MO Bejaia kwenye mji wa Algiers, Algeria mwishoni mwa wiki ukiwa ni mchezo wa kwanza hatua ya makundi.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu ofisini kwake, Manji alisema: “Tumepata hasara, ubingwa wa Bara hadi kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na hii ni kutokana na kushuka kwa mapato ya klabu.
“Hali hii imenilazimisha nitafute fedha nyingine zaidi, Sh2.5 bilioni nje ya utaratibu wa kawaida wa mapato ya klabu ambayo ni hasara kwa upande mwingine, lakini yote ni kuwezesha mambo yaende vizuri,” alisema.
Manji aliyerudi madarakani kwa muhula mwingine baada ya kuzoa kura za ndiyo 1,468 kwenye uchaguzi wa Jumamosi iliyopita, alisema kwa sasa wanakamilisha mipango na kampuni moja ambayo imekubali kuidhamini Yanga kwa mamilioni. Hata hivyo, hakutaka kuiweka wazi kwa kuwa mchakato haujakamilika.
“Kuna kampuni ambayo tupo katika mazungumzo, hii ni kwa ajili ya kuonyesha mechi zetu laivu na wameahidi kutoa fedha zaidi ya zile za udhamini wa Azam Media, siwezi kuitaja kwa kuwa bado mazungumzo yanaendelea, tukikamilisha nitatoa taarifa,” alisema Manji.
Kuhusu kuporomoka mapato ya klabu hiyo, Manji alisema sehemu kubwa imechangiwa na watu wengi kutokwenda uwanjani kama zamani, kwani wanapolipa viingilio, husaidia kutunisha mapato ya klabu.
“Ukweli, kinachoumiza klabu, ni matangazo ya moja kwa moja ya mchezo ambayo husababisha watu kubakia ama nyumbani au baa ili kuangalia mpira.”
Manji alisema kuwa fedha za udhamini wa matangazo ya televisheni hazitoshelezi na kulitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwaacha wajitawale kwa mechi zao kutoonyeshwa laivu.
Kwa upande mwingine, Manji alisema utaratibu wa uuzaji wa vifaa vya klabu kwa kutengeneza jezi, soksi, vitambaa, kofia ungesaidia kuingiza mapato ya klabu, lakini hakuna kinachofanyika kwa kuwa wajanja wachache wanachapisha na kuuza kienyeji.
“Hali nimeikuta na imekuwa ngumu, fedha hizi za jezi, kofia na skafu zingeingia kwenye mapato ya klabu, lakini wajanja wachache wamehodhi na fedha haziniingii klabuni,” alisema.
Manji katika mahojiano hayo, aliitaka TFF kuwaachia wajitawale, hasa katika eneo la kuonyesha mechi na kwamba waseme kiasi gani wanahitaji wawapatie na kuachiwa uhuru wao wa kufanya mambo watakavyo.
“TFF waseme wanapewa shilingi ngapi na Azam kuonyesha ‘live’ ili tuwape, watuache na mechi zetu, si lazima sana. Kama wanapewa Sh10 milioni, sisi tutawapa, watuache,” alisema Manji.
Kuhusu mpango mbadala wa kuongeza mapato ya klabu, ikiwa ni pamoja na kuiweka Yanga katika soko la hisa, Manji alisema itakuwa ngumu kuiingiza katika soko la hisa kwa kuwa klabu inaendeshwa kwa hasara.
Alisema wanahisa watapatikana ikiwa tu timu itapata faida, lakini hakuna mtu anayethubutu kuweka fedha mahali ambako atapata hasara.
Wakati Yanga ikilia kupata hasara, timu ya Medeama ya Ghana ambayo imepangwa kundi moja na Yanga imekaririwa ikieleza kuwa huenda ikajitoa katika mashindano hayo ya pili kwa umaarufu Afrika kutokana na ukosefu wa fedha.
Ofisa utawala wa timu hiyo yenye maskani yake kwenye mji wa Tarkwah, Benjamin Kessie alisema timu yake itashindwa kusafiri kuifuata TP Mazembe ya DR Congo katika hatua ya makundi. Hata hivyo, CAF haijazungumza lolote ikiwa ni pamoja na kuitumia fedha zake za kufuzu hatua hiyo.
Mpango wa timu hiyo kusaka fedha za kuifuata TP Mazembe haujazaa matunda. “Tunaangalia uwezekano wa kujitoa kama hatukupata msaada wa fedha,” ilisema taarifa ya klabu.MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment