JOSEPH MBILINYI (SUGU), JOSEPH HAULE (PROF JAY) KAMA SI UBUNGE BASI WANGEJAMBISHWA KWELI KWELI NA WANGEKOMA
Joseph Haule (Prof Jay) mbunge wa jimbo la Mikumi kupitia Chadema.
Na Ndimi Luqman Maloto
MAZISHI ya Mfalme Muhammad Ali hivi karibuni yanafundisha nini? Akikaribia kumaliza muongo wa nne tangu alipostaafu masumbwi, heshima yake ilibaki juu mno. Marekani ilisimama, dunia ikalazimishwa kufuatilia kwa matangazo ya moja kwa moja.
Kituo cha televisheni bei mbaya ulimwenguni, CNN, kilimpa hadhi kubwa Mfalme Ali kwa kurusha mfululizo wa matukio ya kuelekea na wakati wa mazishi, vilevile kumbukumbu mbalimbali za maisha yake ndani na nje ya ulingo. Kilinunua na kumiliki haki za kurusha matangazo ya msiba wa Mfalme Ali.
Wenzetu walipofikia, msiba wa mtu mashuhuri ni biashara. Wanafahamu kuwa ulimwenguni kote watu watapenda kufuatilia mfululizo wa matukio ya mazishi. Hivyo, vituo vya runinga vinawania haki ya kurusha matangazo. Fedha inaingia.
Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chadema, Joseph Mbilinyi (Sugu)
Kibongo-Bongo, ipo misiba ilishtua mno lakini kila chombo kilikuwa na haki ya kurusha matangazo. Wakati wasanii walijipanga na kutembeza bakuli, kuomba fedha za mazishi ya Mfalme wa Freestyle Bongo, Albert Mangweha ‘Ngwair’, hawakuwaza kama uuzaji wa haki ya matangazo ya msiba, ingetosha kumaliza shida nyingi.
Ilishindikana nini kamati ya mazishi na familia ya marehemu Steven Kanumba kutengeneza fedha kupitia haki ya matangazo ya redio na hata televisheni? Kwamba kunakuwa na kituo ambacho kimethibitishwa kwa ajili ya kutoa taarifa mpya na rasmi. Vingine vinafuata baada ya chenye haki kurusha kwa mara ya kwanza.
Nilipewa kazi ya kuandaa na kusambaza taarifa za vyombo vya habari kuelekea mazishi ya Kanumba Aprili 2012. Vipo vyombo vya habari nilivipelekea taarifa na havikutoa. Hii ni kwa sababu kuna umaalum ulikosekana.
Nilipokuwa nazungumza na Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, akinielekeza cha kuandika, nilijua tu kwamba Dar es Salaam haitatosha. Na kweli haikutosha, watu wengi hawakupata nafasi ya kumtolea heshima ya mwisho Kanumba. Ilibidi wacheza sinema waoneshe maigizo yao, mwili ukazungushwa, mara watu wakashtukia mwili upo Makaburi ya Kinondoni unazikwa.
Tafsiri hapo ni kuwa kila kitu kinaandaliwa. Kama watu wangeamua Kanumba azikwe kawaida na mtikisiko wa jiji usitokee, basi usingetokea. Vivyo hivyo, ingewekwa utaratibu wa vituo vya runinga na redio kununua haki za matangazo, ingewezekana bila shaka, maana taifa zima lilimezwa na taarifa za kifo chake.
Hapo sijagusa Afrika Mashariki na Kati ambako alijitengenezea ukubwa kwa kazi zake.
Ni familia ya marehemu Amina Chifupa iliamua kupiga teke furushi la pesa kwa kutoteua urushaji wa matangazo ya televisheni kama njia mojawapo ya kutengeneza fedha. Alizikwa kienyeji pamoja na umaarufu mkubwa aliokuwa nao, vivyo hivyo jinsi kifo chake kilivyotikisa.
Najaribu tu kunoa vichwa vya watu, kuzitazama fursa za kifedha kwa jicho pana. Usikimbilie kulia, mwangalie aliyekufa ni nani? Usikimbilie kwenye televisheni na redio kuomba misaada ya kifedha, tuliza kichwa kuupamba msiba uonekane ni maalum kisha pesa nyingi zitaingia kwa heshima, siyo za kuombaomba kisha mnatoana macho, eti fulani kala rambirambi.
Mazishi ya heshima kwa kiongozi mashuhuri au mtu yeyote maarufu ni mipango na kupanga ni kuchagua. Kama ambavyo tulichagua kuwazika kikawaida marehemu Nasma Hamis Kidogo na gwiji Issa Matona, ni uamuzi tu, hata Mfalme Ali ingeamuliwa azikwe kawaida wala dunia isingeomboleza.
Hata Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, kama Serikali ya Rais Benjamin Mkapa isingetoa uzito stahiki, naye angezikwa kimyakimya. Ni uamuzi tu, si unaona Muammar Gaddafi hajulikani alipozikwa?
Heshima ya mtu siyo mpaka afe, hata akiwa hai. Kama jamii itaamua kumpa heshima yake akiwepo, atapewa tu na ikimnyima ataikosa. Ni kama ambavyo Rashid Matumla alivyo leo, ikitokea akifa hivi sasa (ni mfano tu, simuombei), hatapewa heshima inayolingana na hadhi yake.
Matumla na utaalam wake, mkali wa kurusha ndonga, aliyejaaliwa kiwiliwili cha kujinganyonga mithili ya nyoka. Hodari kweli wa kukwepa ngumi. Mbane kwenye kamba, uso unauona lakini hupigi ngumi ikampata. Wakambatiza jina la Snake Boy, kwamba ni kama nyoka jinsi alivyo mwepesi kukwepa.
Siku hizi wanamwita Snake Man lakini siyo snake yule. Siyo Matumla bingwa aliyebeba mikanda ya dunia kwa uzito wake. Mabondia wachanga ambao hawajawahi kufikia rekodi hata robo ya Matumla, eti siku hizi wanamjambisha. Wanasema kaisha, ni nani alipata kuwa mfalme wa milele?
Hata Francis Cheka yupo anamalizia enzi zake. Zipo nyakati hataweza kupigana kama ambavyo ilifika wakati Maneno Oswald ‘Mtambo wa Gongo’ alimgeuza Matumla ni punch-bag yake. Ukiona mshale wa saa unasinzia au unasitasita ni mawili, ama betri imekufa au saa yenyewe inaelekea ukingoni.
Saida Kalori na mtikisiko aliousababisha kwenye muziki wa asili ya Kihaya Bongo, ameishia tu kujambishwa. Nani mwenye habari naye tena? Hajaacha muziki, anaendelea kuzichanga kwa kuungaunga.
Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ na uthubutu wake kama siyo ukomando alionao, naye angekuwa ameshajambishwa. Mdada pamoja na kipaji kikubwa alichonacho, vilevile uwezo wa kuicheza mizungu ya kibiashara, ni mbishi kupata kutokea. Hiyo ndiyo sababu hajambishwi.
Katika mixtape ya Antivirus Volume II, rapa Suma Genge au Suma Genius a.k.a Suma Gangster, kwa kifupi Suma G, akitambaa vizuri na mdundo kwenye wimbo Wataokota Wao, anabomoka kuwa watoto wadogo wanawajambisha wakongwe. Ni kweli kabisa.
Kujambishwa ni kawaida katika eneo lolote lile. Ukiwa na pesa zikipungua au zikiisha utajambishwa kuwa umefulia. Ukiwa mwanamuziki maarufu, kisha umaarufu ukashuka na nyimbo zikawa hazisikiki utajambishwa kuwa umeishiwa.
Bongo heshima ya mtu haitunzwi. Wakongwe waliopambana kutengeneza barabara ya muziki, kuifanya Bongo Fleva kuwa biashara wala hawapewi thamani yao. Wanajambishwa kuwa hawakutumia nafasi zao vizuri. Wanasahau kwamba bila wao biashara iliyopo sasa isingekuwepo.
Baba yangu, marehemu Alhaj Swaleh Nyambo aliwahi kuniambia kuwa tajiri huamini ametajirika kwa matokeo mazuri ya akili yake, vivyo hivyo humuona maskini hana akili. Ni rahisi sana leo hii Diamond Platnumz kumuona Inspector Haroun ‘Babu’ hana akili kwa sababu hakupata mafanikio makubwa ya kimaisha na Rap Katuni yake.
Mr Nice anajambishwa kwa mgeuko wa kimaisha alionao, watu hawakumbuki kuwa alibuni aina yake ya muziki na kuita Takeu. Nani mwingine kama Mr Nice? Juma Nature Kiroboto ‘Kibla’ wenye uthubutu wanamjambisha mfalme huyu wa Temeke.
Fred Mariki ‘Mkoloni’ wa Wagosi wa Kaya na ‘u-genius’ wake wote wa kimuziki, kuna watu wanamjambisha. Wengine waliushuhudia moto wa Wagosi kutoka Tanga ila kiburi tu!
Kuna kipindi nilicheka niliposikia eti Mfalme Afande Sele anashindanishwa na Godzilla. Watu heshima hawana. Ila sikushangaa maana hata Jongwe, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alishajambishwa sana kwenye muziki. Ni ubunge umemrejeshea heshima yake.
Ikasemwa Sugu kaisha, eti Sugu mbovu! Sugu ninayemjua au mwingine? Nakumbuka neno lake kwangu baada ya dhoruba la Malaria No More, kwamba anajikita kwenye kilimo. Muziki aliukatia tamaa na Marekani akasema haendi tena. Siasa imemrejesha barabarani.
Vijana chipukizi walithubutu kuimba kuwa muziki umemkataa Sugu. Hii maana yake ni kuwa heshima aliyonayo leo ni kwa sababu ya ubunge wake. Mshahara mzuri, posho, mipango mikubwa, dhamana ya kiheshimiwa, anajenga hoteli ya nyota tatu Mbeya, Hotel Desderia, unawezaje kumjambisha?
Ni sawa tu na Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule ‘Prof Jay’, dharau ilishaanza kubisha hodi. Akatoa Kipi Sijasikia kupunguza midomo ya wachongaji. Alipokuwa anagombea ubunge, hata wasanii wenzake walikwenda jimboni kwake kufanya kampeni ili ashindwe.
Nilizungumza na Jay mwenye masikitiko wakati huo baada ya kushambuliwa na wasanii wenzake. Hii ni kuonesha kuwa kama angekosa ubunge angejambishwa mpaka angekoma.
Jay na kichwa chake kizuri cha kuandika mashairi, jumlisha na uprofesa wake wa Hip Hop ya Tanzania, alishaanza kushushwa bei mbele ya wasanii wachanga. Ubunge wake umesaidia kuondoa zile dharau na ‘zeleu’ zote. Unawezaje kumjambisha mheshimiwa mbunge?.
Lugman Maloto anapatikana katika ukurasa wa facebook
kwa kubofya hiyo link chini.
https://www.facebook.com/luqman.maloto/posts/1375344049147276
0 comments:
Post a Comment