MOHAMED DEWJI WA SIMBA SC KUJARIBU KUZIMA MBWEMBWE ZA YUSUPH MANJI WA YANGA SC KATIKA SOKA LA TANZANIA.
MBWEMBWE zinazofanywa na tajiri wa Yanga, Yusuf Manji zinawakera mashabiki wa Simba ambao wamepagawa zaidi baada ya kusikia maneno ya Bilionea mwenye damu ya Mnyama, Mohammed Dewji ‘MO’ akiomba apewe timu arudishe heshima.
Kama wenye timu yao wakikubaliana na mchakato watakaopewa Julai 31 kwenye mkutano, inamaanisha kwamba MO ndani ya siku 11 kuanzia leo Jumanne ataanza kumwaga mkwanja Msimbazi. Muda huo usajili ndiyo kwanza utakuwa unachanganya.
MO alitamka hivi karibuni kwamba apewe Simba amwage fedha na timu irudi kwenye ubora wake, viongozi wakamwambia akaushe siyo kitu rahisi kiivyo.
Licha ya kwamba hali ilikuwa imetulia kwa miezi kadhaa kwa mashabiki, habari za ndani zinadai vigogo wenye kauli ndani ya Simba wanamuunga mkono MO apewe Simba. Habari zinasema kwamba katika vikao vya hivi karibuni kuhusu Simba mpya hali hiyo imekuwa ikijitokeza.
Ingawa hajakiri kwamba kuna migongano ya mawazo baina ya vigogo hao, lakini Rais wa Simba, Evans Aveva ameona isiwe shida. Ameanzisha mchakato wa kisomi kukusanya maoni na atapeleka pia suala hilo kwa wenye timu yao katika mkutano mkuu utakaofanyika Julai 31. Ni Siku 11 tu kuanzia leo.
Aveva amesema tayari ameunda kamati ya kupokea maoni juu ya mpango huo huku akisisitiza kutomjadili MO pekee bali kampuni yoyote yenye pesa ambayo ina lengo la kununua hisa katika klabu hiyo.
“Unajua MO si kama anahitaji kuidhamini Simba, la hasha, ingekuwa hivyo mbona tungekuwa tushamalizana naye, anachokitaka Mo ni kuinunua Simba sasa kitu hiki hakipaswi kufanyiwa papara,” alisema.
“Tumeanza kwa kuiundia kamati ambayo inafanya kazi ya kutafuta maoni ya wana Simba juu ya mkakati huo, lakini pia kwenye mkutano wetu mkuu tunatarajia kuwasilisha mpango huo na kujadiliwa na wanachama,” alisisitiza Aveva.
Bosi huyo wa Simba alifafanua kwamba katika mpango huo si kwa MO pekee, bali mchakato uliopo ni kutoa fursa kwa kampuni yoyote yenye pesa kununua hisa.
“Tunahitaji kuifanya Simba kuwa na mapato, kuwa klabu tajiri lakini kabla ya kuuza hisa lazima kwanza tushirikishane na wana Simba kutoa maoni yao juu ya nini kifanyike,” aliongeza.
Kuhusu udhamini wa TBL alisema: “Siwezi kueleza moja kwa moja kwamba TBL imesitisha kuidhamini Simba, bado hatujapata barua rasmi kutoka kwao zaidi ya kuzisikia juu juu habari hizo, nikipata barua rasmi nitakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia.” MWANASPOTI.
0 comments:
Post a Comment