
Rais John Magufuli kulia akiteta jambo na Jaji mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman.Picha ya Maktaba
HUKU vitendo vya uhalifu wa mauaji vikiwa vimeshamiri katika siku za karibuni, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, amesema watuhumiwa wa makosa ya ugaidi watakuwa miongoni mwa watakaopandishwa kwenye Mahakama Maalum ya kushughulikia makosa ya Ufisadi na Rushwa kubwa.
Mahakama hiyo inatarajiwa kuanza mwezi huu, wakati ambao Tanzania imeshuhudia kuongezeka kwa uhalifu wa mauaji wenye viashiria vya ugaidi.
Chande amesema majaji 14 wa mahakama hiyo, wataanza kunolewa wiki ijayo.
Alisema mahakama hiyo itasikiliza mashauri ya rushwa na uhujumu uchumi na kesi za ugaidi.
Hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya kutisha ya watu kuchinjwa baadhi yake ni mfano Mei 19, mwaka huu, watu 15 wakiwa wameficha nyuso zao walipovamia msikiti katika mtaa wa Utemini wilayani Nyamagana, Mwanza na kuwaua watu watatu.
Pia Mei 25, mwaka huu, Aneth Msuya (30), dada wa aliyekuwa bilionea na mfanyabiashara wa madini, aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.
Watu wanane pia walichinjwa na watu wasiojulikana Mei 31, mwaka huu mkoani Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari jana alipotembelea maonyesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu alisema majaji wa mahakama hiyo watatoka Mahakama Kuu ya Tanzania na watasikiliza kesi hizo kwa haraka tofauti na ambavyo sasa kesi zinasikilizwa kwenye mahakama za kawaida.
Jaji Mkuu Chande alisema ni matarajio yake kuwa kesi hizo zitakuwa zikiendeshwa na kutolewa uamuzi chini ya miezi tisa.
Kuanzishwa kwa mahakama hiyo ni sehemu ya ahadi ya Rais John Magufuli, aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ili kuharakisha usikilizwaji wa mashauri yanayohusu rushwa kubwa.
Pia Juni 30, wakati wa kutoa hoja ya kuahirisha mkutano wa tatu wa Bunge, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema pamoja na kuanza kwa mahakama hiyo, serikali imeanza mchakato kuifanyia marekebisho Sheria Namba 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007 ili kuongeza ukubwa wa adhabu zinazotolewa sasa.
“Mahakama itawafanya watu waliozoea rushwa na ufisadi kujiuliza mara mbili kabla ya kujihusisha na vitendo hivyo,” alisema Majaliwa.
Akielezea umuhimu wa mahakama hiyo, Majaliwa alisema itasaidia kuendeleza nia ya serikali ya watu kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.
Kauli ya Jaji Mkuu
Jana, Jaji Mkuu alisema majaji wa mahakama hiyo watapatiwa mafunzo ya siku tano kuanzia Julai 11 hadi 15, mwaka huu, katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, mkoani Tanga.
Alisema mahakama ya mafisadi itaanza rasmi, mara baada ya Rais John Magufuli kusaini sheria zilizofanyiwa marekebisho.
Jaji Mkuu alisema baada ya Rais kupitisha sheria hiyo, tangazo litatolewa kwenye gazeti la serikali na utekelezaji wake kuanza rasmi.
"Kwa kuanza na Mahakama ya Mafisadi tayari majaji wetu 14 kutoka Mahakama Kuu wataanza mafunzo maalum ya kuendesha mashauri ya mahakama hiyo, jengo liko tayari tunachosubiri ni Rais kusaini marekebisho ya sheria ya Tanzania ya wahujumu uchumi sura namba 200 toleo la mwaka 2002," alisema.
Alisema katika mchakato huo wa mafisadi, Jaji Mkuu ana jukumu la kufungua masijala na kuanzisha sheria ya kuwalinda mashahidi na watoa taarifa.
Pia alisema makosa yatakayoshughulikiwa na mahakama hiyo ni uhujumu uchumi, rushwa na magaidi.
Aidha, Jaji Mkuu alisema kesi zitakazofikishwa katika mahakama ya mafisadi ni zile ambazo upelelezi wake umekamilika na hazitachukua zaidi ya miezi tisa kutolewa hukumu.
Alisisitiza kuwa: "Tanzania inasifika duniani kote kwa kupambana na mafisadi kwa kitendo cha kuanzisha mahakama ya mafisadi hivyo kesi, zitakazosikilizwa ni zile tu ambazo upelelezi wake umekamilika na hazitafikisha miezi tisa hadi kutolewa hukumu. "
Akiwasilisha Bungeni makadirio ya ofisi yake Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji wa haki kwa kesi zitakazofikishwa kwenye mahakama hiyo.
Aidha, katika siku ya kilele cha Wiki ya Mwaka Mpya wa Mahakama Jijini Dar es salaam mapema mwaka huu, Rais Magufuli alimtaka Jaji Mkuu kutosubiri Bunge kupitisha Sheria ya Uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi, badala yake mahakama hiyo ianze kufanya kazi haraka iwezekanavyo.Nipashe

0 comments:
Post a Comment