SERIKALI KUFUTA TOZO TANO KATI YA TISA ALIZOKUWA ANATOZWA MKULIMA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema uamuzi wa serikali wa kufuta tozo tano kati ya tisa alizokuwa anakatwa mkulima wa zao la korosho uko pale pale na unatarajiwa kuanza kutumika katika msimu wa mwaka huu, hivyo kuitaka Bodi ya Korosho kuusimamia.
“Watendaji wa serikali katika ngazi mbalimbali mnatakiwa kuhakikisha kwamba maelekezo haya yanafuatwa. Malengo yetu ni kumpunguzia mkulima mzigo wa tozo nyingi alizokuwa anakatwa,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akipokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Mtwara, pamoja na taarifa ya kuondolewa kwa baadhi ya tozo katika zao la korosho zilizowasilishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego.
Alisema, serikali iliamua kuzifuta tozo hizo baada ya kubaini kuwa zilikuwa zikiwanyonya wakulima, hali iliyosababisha wauchukie mfumo wa stakabadhi ghalani.
“Kuanzia mwaka huu serikali imeamua mfanyabiashara yeyote wa korosho alipe malipo ya awali kabla ya kuingia kwenye mnada, ili tuwe na uhakika wa kununua korosho hizo na kuwalipa wakulima kwa wakati,” alisema.
Akizungumzia changamoto ya kushuka kwa uzalishaji wa korosho, Waziri Mkuu aliutaka mfuko wa wakfu wa kuendeleza zao hilo ufanye utafiti wa kubaini sababu ili waweze kutafuta namna ya kuipatia ufumbuzi.
“Nitakuja kukutana na viongozi wa mfuko waniambie wanafanya nini na wamefanya nini miaka mitatu iliyopita na wana mpango gani huko mbele tunakokwenda kama hakuna mpango tutauangalia mara mbili mbili kwani wana fedha nyingi lakini hata mbegu hawapeleki kwa wakulima,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliitaka Bodi ya Korosho kuhakikisha kila msimu wakulima wanapata pembejeo bora na zinawafikia kwa wakati.
0 comments:
Post a Comment