BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WANAWAKE WANAOWATIKISA WANAUME DUNIANI KATIKA UONGOZI NDANI ZA NCHI ZAO NDIO HAWA.



Kamla Persad-Bissessar alichaguliwa kama waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Trinidad and Tobago, wakati chama chake kilishinda uchaguzi kwa idadi kubwa ya kura mwezi Mei mwaka 2010

MFUMO dume hauko Tanzania pekee, ni kama upo dunia nzima. Pamoja na elimu kubwa na uelewa wa haki mbalimbali za kijamii na kisiasa kwenye nchi zilizoendelea, suala hili bado ni mtihani japokuwa hivi sasa wanawake wanashika madaraka makubwa.


Rekodi ya dunia hivi sasa inaonyesha kuwa kuna wanawake 22 wanaoshika wadhifa wa juu kabisa kwenye nchi zao. Wanawake hao ni ama Rais au Waziri Mkuu.

ANGELA MARKEL

Huyu ni Kansela wa Ujerumani ambaye amekuwa madarakani tangu Novemba 22, mwaka 2005.

Kansela Markel ni miongoni mwa wanawake wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani na mara kadhaa, amekuwa akitajwa na majarida mbalimbali likiwamo la Forbes kama mtu mwenye ushawishi.

Angela Dorothea Merkel alizaliwa Julai 17, 1954 na ni mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kushika wadhifa huo nchini Ujerumani.

RAIS ELLEN JOHNSON-SIRLEAF

Mwanamama huyu ni Rais wa Liberia tangu mwaka 2006, akiwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo na Afrika.
Alizaliwa Oktoba 29, 1938 akishinda uchaguzi wa mwaka 2005 ambao ulimwingiza madarakani rasmi mapema Januari 16, mwaka 2006.

Juni 2016, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, akiwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo tangu jumuiya hiyo ilipoundwa.

Sirleaf amepata tuzo mbalimbali ikiwamo ya Amani ya Nobel aliyopata mwaka 2011.

Pia anatambuliwa kama ‘mpigania amani’ na pia Septemba mwaka 2013, alipewa tuzo ya Indira Ghandhi, kutokana na juhudi zake za kujenga amani.

Mwaka 2014, jarida la Forbes lilimtaja Sirleaf kuwa miongoni mwa wanawake 70 wenye ushawishi zaidi duniani.

CRISTINA KIRCHNER

Jina lake halisi ni Cristina Elisabet Fernández de Kirchner. Amekuwa Rais wa pili mwanamke nchini Argentina. Alichaguliwa kushika wadhifa huo tangu mwaka 2007 hadi 2015.

Hata hivyo, Cristina ameweka rekodi mpya nchini humo akiwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kwa awamu ya pili.
Cristina aliyezaliwa Februari 19, mwaka 1953 ni mjane wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Nestor Kirchner.

Mwanamama mwingine aliyewahi kushika wadhifa huo ni Isabel Martinez de Peron aliyekaa madarakani mwaka 1974 hadi 1976.

SHEIKH HASINA WAJED

Sheikh Hasina ni Waziri Mkuu wa Bangladesh. Mwanamama huyu alizaliwa Septemba 28, mwaka 1947 akikulia kwenye familia ya mwanasiasa ambaye ni baba yake mzazi, Sheikh Mujibur Rahman.

Sheikh Mujibur alikuwa rais wa kwanza wa Bangladesh. Sheikh Hasina amekulia katika maisha ya misukosuko mingi ya kisiasa akilazimika kuishi na bibi yake uhamishoni kutokana na matatizo ya kivita jambo ambalo pia lilimkwamisha kwenda shule kwa wakati.

“Sikuruhusiwa kwenda shule kwa sababu ilinilazimu kupita kwenye daraja la mbao na bibi yangu aliogopa sana kwamba naweza kutumbukia mtoni,” Hasina amekaririwa akieleza kisa hicho mara kwa mara.

Amekuwa Waziri Mkuu wa Bangladesh tangu Januari mwaka 2009 akishika wadhifa huo kwa mara ya pili. Awali alikaa madarakani akiwa na wadhifa huo mwaka 1996 hadi 2001.

HELLE THORNING-SCHMIDT

Huyu alikuwa Waziri Mkuu wa Denmark kuanzia 2011 hadi 2015 na ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nchini humo. Hivi sasa ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Save the Children.

AMINATA TOURE

Aminata Touré ni Waziri Mkuu wa pili mwanamke wa Senegal baada ya Mama Madior Boye.
Alizaliwa Oktoba 12, 1962 na alishika wadhifa huo kuanzia Septemba Mosi, 2013 hadi Julai 4, mwaka 2014.

ERNA SOLBERG

Huyu ni Waziri Mkuu wa Norway tangu Oktoba 16, 2013 akiwa ni mwanamke wa pili kushika wadhifa huo mkubwa nchini humo baada ya Gro Harlem Brndtland.

Alizaliwa Februari 24, mwaka 1961 akiwa ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini na chama chake cha Conservative.

MARIE-LOUISE COLEIRO PRECA

Mwanamama huyu ni Rais wa Malta tangu Aprili 4, mwaka 2014. Marie Louise Coleiro Preca, alizaliwa Desemba 7, mwaka 1958 na ni rais wa tisa wan chi hiyo.

Amekuwa mbunge wa katika Bunge la Malta tangu mwaka 1998 hadi 2014 alipojitosa kwenye urais.

PARK GEUN-HYE

Ni rais wa Korea Kusini anayeweka rekodi kuwa mwanamke wa kwanza katika nchi hiyo na ukanda mzima nchi za Kaskazini Mashariki ya Bara Asia.

Mwaka 2013 na 2014, jarida la Forbes lilimtaja Park kuwa miongoni mwa wanawake 11 wenye ushawishi zaidi duniani na mwanamke mwenye ushawishi mkubwa zaidi Asia Mashariki.

Mwaka 2014, Forbes ilimtaja tena Park kuwa mtu wa 46 mwenye ushawishi mkubwa zaidi duniani na mtu wa tatu kutoka Korea Kusini kuingia kwenye orodha hiyo baada ya Lee Kun-hee na Lee Jae-yong.

CATHERINE SAMBA-PANZA
Mwanamama huyu ni kama ‘ameokoa’ jahazi la Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.


Catherine Samba-Panza (62), aliteuliwa kuwa rais wa muda wa CAR kuanzia mwaka 2014 hadi 2016, akiwa ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.

Kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa nchi, Samba-Panza alikuwa meya wa jiji la Bangui kuanzia mwaka 2013. Orodha ni ndefu, kwa leo tukomee kwenye hawa wachache ambao ni changamoto kwa wanawake wengine wenye sifa kujitosa kuwania nyadhifa kubwa ndani ya nchi zao.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: