Juma Mtanda, jphtjuma@gmail.com
Kasi ya utumbuaji majipu kwa watumishi wa serikali ya awamu ya tano imeendelea kushika kasi baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya kilosa mkoani Morogoro, Kessy Mkambala kuwasimamisha kazi watumishi 10 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za ukiukwaji wa kanuni za uwajibikaji kazini.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu wilayani Kilosa, Mkambala alieleza kuwa watumishi hao amewasimamisha kazi kwa kutokufuata kanuni na sheria mbalimbali za kiutendaji na wataobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wasiofuata maadili ya kazi.
Mkambala alieleza kuwa miongoni wa waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Manunuzi ya halmashauri hiyo, Geofrey Njovu kwa tuhuma za kufanya manunuzi yasiyofuata taratibu huku akidaiwa kuisababishia halmashauri hasara ya mamilioni ya fedha.
Mkurugenzi hawezi kunisimamisha kazi isipokuwa ana uwezo wa kumenipumzisha majukumu ya kazi na tayari aliniandika barua ya kunisimamisha kazi kwa siku 7 kisha kuandika barua nyingine kwa siku 30 kwa ajili ya kunichunguza.alisema Afisa Manunuzi Geofrey Njovu wakati akifafanua tuhuma hizo.
“Mkurugenzi hana mamlaka ya kunisimamisha kazi wenye mamlaka hayo ni Takukuru baada ya kunichunguza kama kubaini ubadhirifu na sitaweza kuishtaka halmashauri kwa suala hili.”alisema Njovu.
“Ni kweli nimewasimamisha kazi watumishi 10 kutoka idara ya manunuzi ndani ya halmashauri, watumishi sita wa idara ya afya na watendaji wa vijijini watatu kwa nyakati tofauti na hii inatoakana na watumishi kujisahau na kushindwa kutekeleza majukumu yao yapasavyo.”alisema Mkambala.
Watumishi wengine waliotumbuliwa jipu na Mkurugenzi huyo ni pamoja na watumishi sita kati ya saba wa kituo cha afya Kidete akiwemo ni Nehemia Masando, Joseph Emmanuel, Rahma Masoud, Aisha Issa, Christian Mundikeya na Wiliam Mjata.
“Nilifanya ziara ya kustukiza mwishoni mwa wiki katika kituo cha afya Kidete na hakukuwa na mtumishi yeyote jambo ambalo lililinishangaza mimi na timu yangu ya wakuu wa idara kwa kubaini mambo mengi ya matumizi mabaya ya ofisi, kutowahudumia wagonjwa ipasavyo, kutofanya usafi wa majengo vikiwemo vyumba vya kulazia wagonjwa na kuwapa kero wananchi wanaotumia kituo hicho.”alisema Mkambala.
Alieleza kuwa kazi ya kuwasimamisha watumishi hao inalenga kupisha uchunguzi wa tuhuma zao za kutokutoa huduma kwa wananchi vile ipasavyo, kutokuwepo kazini kwa muda wa kazi, kufanyakazi kwa mazoea, kutuhumiwa na kamati ya huduma za afya kata ya Kitete juu ya tuhuma hizo ambapo tume maalumu umeundwa kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo.
Natoa wito kwa watumishi wote ndani ya halmashauri ya wilaya ya Kilosa wafanye kazi kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano inayosisitiza uadilifu hasa kwa watumishi wa umma ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi wenye uchumi wa chini ili waweze kupanda anagalau katika daraja la kati kiuchumi kwa kufuata kauli mbinu ya rais ya hapa kazi tu.alisema Mkurugenzi huyo.
Kusimamishwa kazi kwa watumishi sita kituo cha afya Kidete imesababishwa na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dk Kebwe Stephen kufanya ziara ya kukagua uharibifu wa miundombinu ya reli wilayani humu na kubaini uharibifu na kuwahutubia wananchi wa Kidete.
Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa mkoa aliwaeleza wananchi mikakati ya serikali ya awamu ya tano na namna ya kuzitatua baadhi ya kero ili zipatiwe ufumbuzi kabla ya wananchi hao kuibua kero ya watumishi kituo cha afya hali iliyopelekea mkuu wa mkoa kumwagiza Mkurugenzi huyo kuhakikisha anatatua tatizo hilo kwa muda wa siku saba.
Watumishi wengine waliopewa barua ya kusimamishwa kazi ni pamoja na Mtendaji wa kata ya Vidunda, Zinadu Masanza ambaye anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi pamoja na tuhuma za kutofanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za kiutumishi.
Watendaji wengine ni Batista Chang'a wa kijiji cha Tindika pamoja na Mtendaji wa kijiji cha Chonwe, Adrian Chiligwa ambao wote kwa pamoja wanatuhumiwa kwa kukosa uadilifu kazini.
Hata hivyo Mkambala amemwagiza Mganga mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha huduma katika kituo cha afya Kidete zinaimarika ndani ya muda mfupi ili kuondoa kero kwa wananchi kwa kupeleka haraka watumishi wengine wenye waadilifu na wenye moyo wa kufanya kazi.
Kwa upande wa Mtendaji Wa Kata ya Vidunda, Zidadu Masanza akizungumza kwa njia ya simu alieleza kushangazwa na tuhuma za kusimamishwa kazi na Mkurugenzi kwa madai ya kutokabidhiwa barua ya kusimamishwa kazi na hawezi kuzungumzia zaidi.
“Mwandishi…sijapata barua ya kusimishwa kazi na mwajili wangu hivyo siwezi kujibu maswali yako ya kutaka maoni ya kwanini umesimamishwa kazi kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kutofanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za kiutumishi labda nikipata hiyo barua nitakuwa na jibu.”alisema Masanza.
Akizungumzia suala la kuwasimamisha kazi watumishi wa kituo cha afya Kidete, Diwani wa kata hiyo, Mohamed Punda alieleza kuwa juhudi zinazofanywa na Mkurugenzi huyo ni zakupongezwa kwani anaonekana anaendana na kasi ya rais Magufuli.
“Tulikuwa tunamhitaji Mkurugenzi mwenye kasi ya utendaji wa kazi kama ya Rais Magufuli, ni kweli ziara ya Mkurugenzi juzi imemkuta mtumishi mmoja tu na mimi nimeafiki kusimamishwa kazi watumishi sita kwani huu ni uzembe.”alisema Punda.
Punda alisema kuwa kituo hicho kinahudumia watu 12,302 ndani ya kata hiyo huku akidai chanzo cha watumishi hao kuwa wazemba na tuhuma nyingine zinatokana na marumbano yasiyo na tija ya kugombea madaraka hali inayopelekea utoaji wa huduma kudhorota.Chanzo/MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment