HIVI NDIVYO RAIS MSTAAFU ZANZIBAR ABOUD JUMBE MWINYI ALIVYOAGA DUNIA JIJINI DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aboud Jumbe Mwinyi (96), amefariki dunia jana jijini Dar es Salaam.
Jumbe ambaye alikuwa Rais wa pili wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alifariki jana saa saba mchana nyumbani kwake Kigamboni Mji Mwema na atarajiwa kuzikwa leo Kisiwani Unguja, Zanzibar.
Taarifa za kifo chake zilianza kusambaa jana mchana na baadaye kuthibitishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud, ambaye alisema kuwa, mzee Jumbe amefariki akiwa na umri wa miaka 96.
“Mimi ndiyo ninaingia hapa nyumbani kwake Kigamboni na tutakuwa na kikao na wanafamilia ambapo tutaamua muda wa mazishi. Ila kwa hatua za awali tutazika kesho (leo) Unguja.
“Kwa muda mrefu mzee Jumbe alikuwa akisumbuliwa na maradhi lakini pia na umri wake umekuwa mkubwa hivyo kazi yake Mola haina makosa na hakika tutamkumbuka mzee wetu kwa harakati zake za kudai masilahi ya Zanzibar na Watanzania kwa ujumla,” alisema Aboud.
Mwaka 1984 mwanasiasi huyo aliyekuwa na nguvu katika Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere, alijiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kulazimishwa, akituhumiwa kutaka kuvunja Muungano.
Mei 18, 2002, aliyekuwa mwandishi wa gazeti la Mtanzania, Yussuf Kajenje, alifanya mahojiano na marehemu Aboud Jumbe nyumbani kwake Mji Mwema Kigamboni.
Mahojiano hayo yalichapishwa katika gazeti la Mtanzania Jumapili, Mei 26, 2002, ambapo yalikuwa hivi;
“Siku hizi sisikii vizuri na pia sioni sawasawa. Hivyo niwie radhi kwa mapungufu yatakayojitokeza wakati wa mazungumzo yetu,” alianza kusema Aboud Jumbe wakati akikaa vizuri katika moja ya masofa yaliyokuwa sebuleni baada ya kutoka mahali ambako bila shaka alikuwa amejipumzisha.
Kwa wakati huo akiwa na zaidi ya miaka 80, Aboud Jumbe alionekana wazi kuwa umri ulikuwa umeanza kumtupa mkono, alikuwa amezeeka.
Hata hivyo, mbali na uzee huo bado alikuwa na uwezo mkubwa kufuatilia mambo yanayotokea duniani na alionekana kumbuka mengi aliyokutana nayo tangu enzi zake za utotoni.
“Tangu nilipotoka serikalini mwaka 1984, nimekuwa nikifanya shughuli mbalimbali za kujipatia riziki, na kutafuta mwisho mwema kwa Mwenyezi Mungu,” alisema Aboud Jumbe.
Akizungumzia juu ya maisha yake tangu utotoni, Aboud Jumbe ambaye alizaliwa Zanzibar Juni 14, 1920 alisema mambo mengi yalimtokea kwa namna tofauti na jinsi alivyotarajia.
“Utastaajabu kwamba katika maisha yangu yote sikuwahi kuwa na mpango. Na kama ulikuwapo, basi haukufanikiwa.
“Kwanza nikiwa na miaka 10 nilipelekwa kusoma madrasa, lakini nikatolewa kwa nguvu na askari waliokuwa wakipita kuwakamata watoto wenye umri mkubwa wa kwenda shule. Nilipenda sana kuendelea na madrasa, lakini haikuwezekana.
“Ingawa nilipenda madrasa, sikutoroka katika shule ya Mnazi Mmoja (sasa inaitwa Ben Bella) ambako nilikuwa nimepelekwa kusoma. Nilifanikiwa kumaliza darasa la nane katika shule hiyo,” alisema Aboud Jumbe.
Alisema kwamba siku moja asubuhi akiwa anafua nguo, alifahamishwa na mkuu wa shule hiyo ambaye alikuwa mzungu kwamba alikuwa amefaulu mtihani, hivyo alitakiwa kuendelea na masomo ya sekondari katika shule hiyo.
Alisema akiwa Makerere ndiko alikopata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. “Wote tulikuwa tunasomea ualimu na tulielewana sana,” alisema
Aboud Jumbe alisema kwamba mara baada ya kuhitimu Makerere, alifundisha kwa miaka 15. “Mwaka 1958, kiongozi wa chama cha ASP, Sheikh Thabit Kombo, alinijia akaniomba nisaidie harakati za chini kwa chini za kupambana na utawala wa kisultani.”
“Nilishauriana na mke wangu, mama, pamoja na dada yangu kuhusu uamuzi wa kuacha kazi ya ualimu iliyokuwa ikinipa mshahara wa Sh 1,500. Walikubali, nami nikaingia katika harakati za chini kwa chini ambazo hazikuwa na mshahara mkubwa.”
Aboud Jumbe alisema kwamba mapinduzi yalipofanyika mwaka 1964, alipata wadhifa wa kuwa Katibu wa Mipango mpaka mwaka 1972 wakati alipochaguliwa kuwa Rais wa SMZ. “Kwa mara nyingine hilo halikuwa katika matarajio yangu.”
Akizungumzia juu ya maisha yake ya ndoa, Aboud Jumbe alisema kwamba alioa mke wa kwanza mwaka 1948, miaka mitatu tangu alipoanza kazi ya ualimu. Miaka minne baadaye, 1952, alijaliwa kupata mtoto wa kwanza. Mkewe huyo wa kwanza ambaye alifariki mwaka 2000, alizaa watot o wanane, wawili wa kike, na sita wa kiume.
Aboud Jumbe alisema kwamba baada ya mapinduzi ya mwaka 1964, alioa tena mke mwingine ambaye alizaa watoto watano wa kiume. “Baadaye tuliachana, kisha nikaoa mke mwingine wa kutoka Pemba ambaye ndiye ninayeishi naye sasa (wakati wa mahojiano), na amezaa watoto wawili, wa kike na wa kiume.”
Mbali na wake zake hao watatu, Aboud Jumbe alioa mwanamke mwingine ambaye kwa kauli yake ndiye aliyekuwa akisafiri naye mara kwa mara katika safari za kikazi. Alizaa naye watoto watatu. Kwa ujumla alioa wake wanne, na hadi mwaka 2002 alikuwa amejaaliwa kupata jumla ya watoto 18.
Namna alivyojiuzulu
Akizungumzia juu ya kujiuzulu kwake mwaka 1984, Aboud Jumbe alisema kuwa kulitokana na baadhi ya viongozi aliokuwa nao serikalini Zanzibar kumfitini kuwa anataka kuiuza nchi.
Alisema viongozi hao wafitini (anamtaja Maalim Seif) walieneza uvumi kwamba kulikuwa na mpango wa kutaka kuipindua serikali ili kuua Muungano. “Hata hivyo, viongozi hao baadaye walipata matatizo nao wakatoka serikalini kwa kufukuzwa.
“Siku moja kabla ya Sherehe za Mapinduzi ambazo zilikuwa zimepangwa kufanyika Pemba, walikuja wajumbe wawili wa Baraza la Mapinduzi wakaniambia kuwa kule Pemba hali haikuwa nzuri, na kwamba kungetokea maasi.
“Nilimpa taarifa hizo Mwalimu Nyerere, naye akaja Zanzibar kama ilivyokuwa imepangwa bila kujali taarifa nilizokuwa nimempelekea,” alisema.
Aboud Jumbe alisema kuwa katika kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilichofanyika Dodoma mwaka 1984 kujadili hali ya machafuko ya kisiasa Zanzibar, hakuna aliyejua kwamba angechukua uamuzi wa kujiuzulu. “Hata Mwalimu Nyerere hakujua”.
“Nilichukua uamuzi wa kujiuzulu kwa sababu masharti yangu matatu ya kufanya kazi popote pale yalikuwa yamevunjwa,” alisema.
Alisema kuwa sharti lake la kwanza kufanya kazi ni lazima isiwepo hali ya kutia shaka, na pawepo uwazi na ukweli.
“Sharti la pili ni kuwa na uwezo kimwili na kiakili, na si kuendeshwa na kufanywa kama sanamu,”.
Alitaja sharti la tatu ni kuwa ni lazima wote wakubaliane kufanya kazi pamoja, jambo ambalo Aboud Jumbe alisema masharti hayo yote yalivunjwa, hivyo aliamua kujiuzulu.
Alipojiuzulu alitaka kurudi kwao Zanzibar, lakini kwa maelezo yake Mwalimu Nyerere alimzuia. “Nyerere alinishauri nisirudi Zanzibar wakati huo kwa sababu hali haikuwa nzuri. Alisema nisubiri mambo yatulie kwanza,” alisema.
Baada ya kujiuzulu, mbali na mambo mengine ambayo alikuwa akiyafanya ni pamoja na kuandika vitabu. “Nimekuwa nakijishughulisha na kazi ya uandishi wa vitabu. Mpaka sasa (wakati wa mahojiano) nimekwishaandika vitabu vinne; cha kwanza ni ‘Safarini’ ambacho maudhui yake ni kwamba binadamu wote katika maisha tuko safarini.”
Aboud Jumbe alisema aliamua kuandika kitabu hicho kwa lengo la kuikumbusha nafsi yake pamoja na binadamu wengine mambo ya kufanya ili kupata mwisho mwema kwa wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu.
JPM amlilia
Rais wa Dk. John Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, kutokana na kifo cha Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea jana Jijini Dar es Salaam.
Aboud Jumbe Mwinyi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 1972 hadi 1984.
Rais Magufuli, alisema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alijitoa kupigania Uhuru, Umoja, Haki na Maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilikipitia.
“Nimeshitushwa sana na kifo cha Mzee wetu Aboud Jumbe, kwa hakika Tanzania imepoteza mtu muhimu ambaye katika kipindi cha uongozi wake alitoa mchango mkubwa wa kuipigania na kuijenga Tanzania tunayoiona leo.
“Kupitia kwako Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein napenda kuwapa pole familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote, wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa ujumla kwa kufikwa na msiba huu mkubwa,” alisema Rais Magufuli.MTANZANI
0 comments:
Post a Comment