Mbunge wa viti maalumu kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Morogoro, Devotha Minja amewataka wananchi waliokumbwa na mafuriko wilayani Kilosa kufanya maandamano ya amani kwenda Ikulu kwa lengo la kufikisha kero mbalimbali kwa rais, Dk Magufuli.
Akizungumza na wahanga wa mafuriko katika kijiji cha Mateteni kata ya Mbigili juzi mkoani hapa, Minja alisema kuwa serikali iliahidi kutoa viwanja kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko lakini inaonekana baadhi ya vijiji havijapatiwa viwanja hivyo.
Minja alisema kuwa serikali isipotekeleza ahadi zake kwa wananchi kama wahanga wa mafuriko inakuwa haiwatendei haki kwani kazi ya serikali ni kuboresha huduma za jamii ikiwemo wahanga hao kupewa maeneo ya kudumu lakini mpaka leo imekaa kimya.
“Rais amewataka akinamama kufyatua watoto lakini kwa maisha ya wananchi wanaoishi katika kambi za mafuriko wataweza kufyatua watoto kwa maisha ya dhiki wanayoishi kweli?...lakini kwa kauri hii sidhani kama inajenga heshima kwa mwanamke.”alisema Minja. Mhe Minja akijiandaa kumchukua mtoto ili amsalimie katika kambi hiyo.PICHA NA MTANDA BLOG.
Aliongeza kuwa kutokana na uzembe wa kushindwa kuwajibika kwa baadhi ya viongozi wa serikali ya wilaya ya Kilosa, kuna umuhimu wa kutekeleza agizo la Waziri Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi haraka iwezekanavyo, kwa serikali hiyo kubainisha maeneo yote ya ardhi ya mashambapori ambayo hajaendelezwa yabainishwe ili kutoa nafasi ya rais kufuta hati za umiliki.
“Bunge linalofuata nitahakikisha suala langu la kwanza bungeni ni kumuuliza Waziri mkuu na waziri Lukuvi kwanini mpaka leo wananchi wa Mateteni hawajapatiwa maeneo mazuri ya viwanja vya kudumu vya kujenga nyumba?.. Jukumu la wananchi kuishi maisha bora ni jukumu la serikali...Lakini akinamama na watoto ndio wahanga wakubwa na wamekuwa wakiteseka”alisema Minja.
Minja alisema kuwa inashangaza kuona Tanzania inasaidia wakimbizi kutoka nje ya nchi wakiishi maisha mazuri lakini unastajabu kuona watanzania tena idadi ndogo inaishi maisha ya dhiki na taabu ndani ya nchi yao hilo ni lazima lisemwe.
Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Morogoro Chadema, Devotha Minja akizungumza jambo na wahanga wa mafuriko Mateteni kata ya Mbigili wilaya ya Kilosa wakati alipowatembelea.Picha/MTANDA BLOG
Kwa upande wa Mwenyekiti wa kitongoji cha Mateteni kijiji cha Mateteni kata ya Mbigili wilayani Kilosa, Poplin Gembe (41) alisema kuwa jumla ya kaya 263 zilikumbwa na mafuriko mwaka 2014 kipindi cha masika na kusababisha hasara kubwa ikiwemo uharibifu wa mazao na mashamba na mali nyingine.
Naye Mwenyekiti wa mahema katika kambi ya wahanga hao, Haruna Ramadhani (58) alieleza kuwa kambi hiyo inakabiliwa na changamoto ya kutokea kwa magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na magonjwa ya baridi au vichomi (nimonia) ambayo yamesababisha madhara kwa wahanga hao.
“Mwezi wa nne mwaka huu ulilipuka ugonjwa wa kipindupindu na kuua kijana mmoja lakini ugonjwa wa Emonia pia uliua mtoto.”alisema Ramadhan.
Ramadhani alieleza kuwa mwaka jana watoto sita walipatwa na ugonjwa wa nimonia wakati mwaka huu watoto wawili walipatwa na ugonjwa huo lakini serikali ilijitahidi kudhibiti mlipuko wa kipindupindu.
Kambi hiyo ina kaya 263 lakini kutokana na hali ya uchakavu wa mahema ni kaya 65 ndizo zinazoendelea kuishi huku wengine wakirejea katika makazi ya awali baada ya mahema yao kuchakaa zaidi.
Mmoja wa akinamama katika kambi hiyo, Salima Msabaha alieleza kuna wakati kipindi cha baridi hulazimika kulala nje ya mahema na watoto kwa kuhofia upepo kuezua mahema kusababisha madhara mengine kutokana na kuchakaa kwa miti inayoshikilia mahema.
Endapo serikali itasaidia miti, mbao na maheba mapya itasaidia kuendelea kujihifadhi kama hakuna sehemu nyingine ya kuwapeleka ambapo makazi yamekuwa ya shida pindi mvua inanyesha maji yamekuwa yakiingia ndani.chanzo/MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment