MMILIKI WA KAMPUNI YA FOREPLAN JUMA MWAKA ASAKWA KILA KOSA NA ASKARI POLISI DAR ES SALAAM BAADA YA KUTOKA AMRI YA KUKAMATWA
Mmiliki wa kampuni ya Foreplan, Juma Mwaka.
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kingwangalla, alitoa saa 24 kwa jeshi la polisi kuanzia jana kuhakikisha kuwa linamkamata na kumtia mbaroni mmiliki wa kituo cha tiba asilia cha Foreplan kilichopo Ilala jijini Dar es Salaam, Dk. Juma Mwaka.
Hatua hiyo imetokana na kile alichoeleza kuwa ni kitendo chake cha kukaidi agizo halali la kukifungia kituo hicho kwa kukiuka masharti ya kibali walichopewa.
Baada ya Dk. Kigwangalla kufika kwenye kituo hicho ambacho sasa kinatambulishwa zaidi kama kampuni, alilazimika kupatiwa kibali cha polisi ili kuingia ndani katika kituo hicho na kujiridhisha kwa kufanya ukaguzi.
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kingwangalla.
Aidha, baada ya Dk. Kigwangalla kufika hapo, Dk. Mwaka hakuonekana na ndipo alipowataka Polisi kumkamata kokote alipo. Kamanda wa Mkoa wa Polisi wa Ilala, Salum Hamduni, aliiambia Nipashe kuwa hadi kufikia majira ya saa 1:00 usiku jana, bado polisi walikuwa wakimsaka Dk. Mwaka ambaye hakuwa akipatikana.
“Tayari kuna watu wanafanya kazi ya kumfuatilia… watakapompata watanijulisha na mimi nitatoa taarifa juu ya kinachoendelea,” alisema Kamanda Hamduni.
Julai 11 mwaka huu, Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Dk. Edmund Kayombo, alitangaza kufungiwa kwa kituo cha Foreplan cha Dk. Mwaka kutokana na kukiuka masharti ya kibali alichopewa kwa kujitangaza kuwa anatoa tiba za kisasa badala ya zile za asilia.
MATOKEO UKAGUZI
Akizungumza baada ya ukaguzi wake, Dk. Kigwangalla alisema wamekuta shehena ya dawa za tiba asilia na pia dawa za vitamini B na za madini ya chuma licha ya tabibu huyo kupigwa marufuku na Baraza la Tiba asilia juu ya kuttumia dawa hizo.
Dk. Kigwangalla alitaka Dk. Mwaka ajisalimishe mwenyewe Polisi na wakati huohuo akalitaka jeshi la polisi lihakikishe linamsaka na kumkamata pindi asipofanya hivyo ili aeleze ni kwa nini amekuwa akikiuka maagizo halali ya serikali ya kufuata taratibu zilizopo katika kutoa huduma za tiba za asili. Alimtaka pia tabibu huyo kuonyesha vithibitisho halali vya ufanyaji kazi wake.
Aidha, Dk. Kigwangala aliziagiza mamlaka husika, zikiwamo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Baraza la Famasia, Baraza la Tiba Asilia na Tiba Mbadala, kuhakikisha wanachukua hatua za kisheria dhidi ya ukiukwaji wa sheria kutokana na kituo hicho kuendelea kutoa huduma kinyume cha utaratibu licha ya kufungiwa kufanya hivyo.
Jitihada za Nipashe kumpata Dk. Mwaka kupitia simu ya mkononi zilishindikana jana baada ya kupigiwa mara kadhaa bila ya mafanikio.
UKAGUZI HOSPITALI MWANANYAMALA
Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Mwananyamala na kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kuandaa mpango wa haraka wa upatikanaji wa vitanda 350 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Pia Dk. Kigwangalla alizindua mradi wa Tiba kwa Kadi (Tika) katika Manispaa ya Kinondoni utakaowawezesha wananchi walio katika sekta isiyo rasmi kupata matibabu.
Mradi huo unaowahusisha mama na baba lishe, bodaboda na wananchi wengineo, huhusisha uchangiaji wa Sh. 40,000 kwa mwaka mmoja na mchangiaji kupata matibabu katika hospitali za serikali za manispaa hiyo.
Dk. Kigwangalla alisema halmashauri hiyo inapaswa kuwafikia walau asilimia 60 ya wananchi kwa ajili ya mpango huo.
Mstahiki Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob, alitaka watendaji kwenda maeneo ya watu ili kuwaandikisha pamoja na kuwashirikisha watendaji wa Serikali za Mitaa na wenyeviti ili mradi huo ufikie malengo yake.
Mratibu wa Tika, Aleswa Zebedayo, alisema wazee, wajawazito na watoto watalipiwa na halmashauri.
0 comments:
Post a Comment