PANZIA LA LIGI KUU KUANZA KUTIMUA VUMBI LEO KWA MICHEZO 10, SIMBA SC KUTUPA KARATA KWA NDANDA FC UWANJA WA TAIFA DAR ES SALAAM
HATIMAYE kivumbi cha Ligi Kuu Tanzania Bara kinaanza leo, ambapo timu 10 zitashuka dimbani ili kuanza kampeni za kuwania kutwaa taji la michuano hiyo.
Kwa sasa ubingwa huo unashikiliwa na Yanga, ambao waliunyakua msimu uliopita baada ya kufikisha pointi 73, huku nafasi ya pili ikienda kwa Azam FC, waliokamata nafasi hiyo baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 64.
Katika mechi za leo mabingwa watetezi, Yanga wataweka kiporo mchezo wao dhidi ya JKT Ruvu na watacheza Agosti 31 ili kuiwezesha Yanga kuhitimisha mchezo wake wa Kombe la Shirikisho la Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo utakaofanyika Jumanne. Timu hiyo inaondoka kesho.
Tayari Yanga imefungishwa virago kwenye michuano hiyo baada ya kupokea vipigo mfululizo kutoka kwa TP Mazembe bao 1-0 katika Uwanja wa Taifa, kabla ya kunyukwa bao 1-0 na Mo Bejaia huku wakichukua kipigo cha `mbwa mwizi’ kutoka kwa Medeama cha mabao 3-1.
TP Mazembe ndio wapo kileleni na pointi 10, Medeama pointi nane, Mo Bejaia tano na Yanga nne wakiwa wapo mkiani mwa kundi hilo, ingawa walipata ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Mo Bejaia katika Uwanja wa Taifa jijini siku chache zilizopita. Katika michezo ya Ligi Kuu leo, viwanja vitano tofauti vitawaka moto wakati timu hizo zitakapopepetana kuwania pointi tatu muhimu.
Mechi za fungua dimba zitakazopigwa leo ni Simba ikiwakaribisha Ndanda katika Uwanja wa Taifa, Stand United itamenyana na timu iliyopanda daraja ya Mbao FC kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga, wakati Mtibwa Sugar itaivaa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Manungu na Majimaji ‘Wanalizombe’ watawakaribisha Maafande wa Tanzania Prisons ya Mbeya.
Upinzani mkali unatarajiwa kuwa kwenye timu za Simba, Yanga na Azam ambazo zinawania nafasi ya juu kileleni kwenye ligi hiyo ambayo inachezwa kwa mara ya 51 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965.
Klabu 16, tatu zilizopanda daraja zitaungana na 13 zilizosalimika kwenye ligi iliyopita, zitachuana kuwania taji hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, Yanga. Yanga ndiyo klabu iliyotwaa mara nyingi ubingwa wa ligi hiyo tangu mwaka 1965, ikitwaa mara 26, huku wakifuatiwa kwa mbali na watani zao, Simba walionyakua mara 18.
Machozi, jasho na damu
Ligi ya msimu huu inatarajiwa kuwa ngumu na yenye upinzani mkali kutokana na vikosi vya timu pinzani ambazo zimekuwa zikichuana juu kileleni kuwania kutwaa ubingwa, huku timu hizo zikisheheni wachezaji wa kigeni na zikinolewa na makocha wa kigeni.
Yanga wako vizuri:
Yanga ndio timu ambayo inaweza kusema ina kikosi bora na itaingia kutetea ubingwa wa ligi ikitokea mashindanoni, hivyo wachezaji kuwa na ari, ambapo wachezaji kama Donald Ngoma amekuwa chachu ya mashambulizi mbele na yeye ndiye mchezaji mwenye msaada mkubwa kuliko mchezaji yeyote pale Yanga.
Juma Abdul ambaye alitwaa tuzo ya mchezaji bora msimu uliopita, amekuwa msaada mkubwa wa kupiga krosi zinazozaa mabao na yupo vizuri katika ukabaji nyuma. Amissi Tambwe, kinara wa mabao, ‘kiraka’ Mbuyu Twite pia anaweza kurudi katika beki namba mbili. Nahodha, Nadir Haroub atarudi kikosini kucheza na Mtogo, Vicent Bossou katika beki ya kati.
Hans atakuwa na beki ngumu huku safu ya kiungo ikitaraji kuongozwa na Mzimbabwe Thaban Kamusoko, Said Juma Makapu, Saimon Msuva, Mnyarwanda Haruna Niyonzima na Deus Kaseke.
Azam: Kukosekana kwa mshambulizi raia wa Ivory Coast, Kipre Tchetche kunaweza kupunguza makali ya safu ya mashambulizi ya Azam FC lakini Hernandez anaweza kuwatumia, nahodha wake John Bocco, Farid Mussa, Ramadhani Singano katika safu ya ushambuliaji.
Himid Mao, M-Ivory Coast, Kipre Bolou, Mnyarwanda Jean Mugiraneza, Salum Abubakary wataongoza safu ya kiungo.
Erasto Nyoni, Shomari Kapombe wanaweza kusaidia katika beki za pembeni. Aggrey Morris na David Mwantika pia wanaweza kuanzishwa katika beki ya kati. Hiki ni kikosi bora pia baada ya kucheza pamoja kwa muda mrefu sasa. Tofauti inaweza kuletwa na timu ambayo wachezaji wake watakimbia uwanjani, watamiliki mpira, kuwa na ustahimilivu.
Zeben ameichukua timu yenye sura nyingi za wachezaji, ambazo zilifanya kazi na Muingereza, Stewart Hall. Katika mechi zake za kujipima uwezo kocha huyo amekuwa akiichezesha timu yake katika mfumo wa 4-4-2 na ule wa 4-3-3.
Simba:
Baada ya kuchechemea kwenye ligi misimu minne iliyopita, Simba ya safari hii imebadilika na inategemewa kuleta ushindani wa hali ya juu.
Kikosi hicho cha Msimbazi, kinamtegemea zaidi mshambuliaji wake, Laudit Mavugo, baada ya timu hiyo kutofanya vizuri kwa misimu minne mfululizo hali ambayo ilizipa nafasi Yanga na Azam kuitambia huku Yanga wakienda mbele zaidi kwa kujiita Wakimataifa kutokana na ushiriki wao kwenye michuano ya kimataifa huku Simba wakishindwa kufuzu kutokana na kuonesha kiwango kibovu.
Usajili wa wachezaji wa kimataifa waliopo Simba kina Vicent Angban, Mavugo, Juuko Murshid, Musa Ndusha, Janvier Bokungu, Fredrick Blagnon na Method Mwanjali umewapa imani Wanasimba kuamini kuwa huu ni mwaka wao wa kufanya vizuri.
Omog amekuwa akiwasuka wachezaji wake kuanzia ulinzi hadi safu ya ushambuliaji, namna ya kumiliki mpira, kutoa pasi za uhakika na pia kucheza na akili za wapinzani.
Kwa mabeki amekuwa akiwasisitiza namna ya kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani wasilete madhara langoni mwao, huku pia akiwaelekeza namna ya kuepuka kufanya faulo zisizo za lazima na kadi za njano na nyekundu.
Kwa viungo amekuwa akiwafundisha namna ya kuwasaidia mabeki kuzuia, lakini pia kuwasaidia washambuliaji kupiga pasi za uhakika jambo ambalo wameonekana kulimudu vizuri.
Upande wa safu ya ushambuliaji, Omog amekuwa akiwaelekeza kutumia vizuri nafasi wanazozipata kupachika mabao ambapo kama maelekezo hayo yatazingatiwa na wachezaji hao mashabiki wa Simba hawatakuwa na presha yoyote msimu huu.
Zilizopanda daraja Ruvu Shooting: Wamerudi ligi kuu bara baada ya kushuka msimu wa 2014/2015, Ruvu Shooting wana uzoefu wa kutosha katika ligi kuu, kocha mzoefu Tom Olaba, wachezaji wenye uzoefu na ligi kuu bara kama Kisiga, hivyo haitakuwa na jipya kwao kuzoea mikiki-mikiki ya ligi kuu, kipindi hiki ni muda sahihi kwa benchi la ufundi pamoja na viongozi kuanza kuandaa timu kwa msimu hujao.
Mbao FC:
Timu kutoka Mwanza, wanapata nafasi baada ya Geita Gold na Polisi kushushwa daraja kutokana na upangaji wa matokeo katika mechi za daraja la kwanza.
Mbao FC ndiyo mara yao ya kwanza kupanda ligi kuu msimu huu, viongozi wanahitaji kufanya kazi kubwa sana kama kutafuta wadhamini mapema, pesa za Vodacom na Azam haziwezi kuwa msaada kwao, wasipojipanga mapema watakuwa kama watalii, watapanda na kushuka kwa msimu mmoja .
African Lyon:
Wamekuwa wakipanda na kushuka kwa vipindi tofauti tofauti, kama ilivyo kwa Ruvu Shooting, African Lyon nao wana uzoefu wa kutosha ligi kuu, inatarajiwa msimu huu kuona.
timu hiyo ikitoa upinzani mkubwa naana tayari wameingia makubaliano na tajiri kutoka uarabuni kuifadhili.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment