BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SIKU YA SIMBA SC NI SIKU ILIYOJAA MACHUNGU NA FURAHA KIDOGO IKITOKANA NA KUIFUNGA KLABU YA VILLA PEKEE







Kikosi cha timu ya viongozi wa Simba wakati wa siku maalum ya klabu hiyo, maarufu kama ‘Simba Day’ msimu wa 2015/2016

KLABU ya Simba, leo inahitimisha wiki yake iliyobatizwa jina la 'Simba Day' kwa kucheza mechi dhidi ya AFC Leopards ya Kenya badala ya Inter Clube ya Angola kama ilivyotangazwa awali.Hiyo itakuwa ni timu ya pili kutoka Kenya kupambana na Simba kwenye mechi za tamasha hilo.

Mwaka 2012, ilicheza na Nairobi City Stars, na ni mara ya kwanza kucheza na timu hiyo, moja ya klabu kubwa nchini Kenya.

Historia ya Simba Day

Kwa ufupi tu ni kwamba, Simba Day ilianzishwa mwaka 2009 chini ya uongozi wa mwenyekiti wa wakati huo Hassan Dalali pamoja na Katibu wake, Mwina Kaduguda.

Madhumuni ya siku hiyo kwa mujibu wa waasisi ni kukutanisha pamoja Wanasimba wote bila kujali matabaka yao, yaani viongozi, wanachama, wachezaji na mashabiki kujadili mambo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya klabu yao.

Lakini pia hutumia siku hiyo walioichagua ambayo ni Agosti 8 kutambulisha kikosi chao chote cha msimu unaofuata wa ligi na hata mechi za kimataifa.

Hufanya hivyo kwa kutambulisha mchezaji mmoja mmoja na namba atakayoivaa kwa msimu husika, pamoja na kuonyesha jezi mpya za msimu watakazotumia.

Sambamba na hilo, uwanjani hapo hutawaliwa pia na burudani kadha wa kadha kutoka kwa bendi na wasanii mbalimbali maarufu ambao wanakuwa wapo kwenye chati wakati huo.

Hilo ndilo tamasha la Simba la kila mwaka linalotambuliwa kama Simba Day ambalo kila mwaka hufanyika Agosti 8, kasoro mwaka 2014 ambalo lilifanyika Agosti 9.

Ikumbukwe kuwa Agosti 8 pia huwa ni siku ya mapumziko ya sikukuu ya Nanenane.

Tamasha hilo la Simba kuwa ni hitimisho la wiki nzima kwa viongozi wa klabu hiyo, wanachama, mashabiki na wachezaji kutembelea na kutoa misaada sehemu mbalimbali za kijamii kama vile kwenye vituo vya watoto yatima, hospitalini na hata kufungua matawi.

Huu ndiyo mpango ulioasisiwa na uongozi wa Simba chini ya mzee Dalali.

Yafuatayo ni matokeo ya mechi zote za tamasha la Simba Day tangu ianzishwe.

1. Simba 1-0 SC Villa (2009)

Hii ndiyo mechi ya kwanza ya ‘Simba Day’ ilipoanzishwa na timu ya SC Villa kutoka nchini Uganda kualikwa.

Katika mechi hiyo Simba iliifunga SC Villa bao 1-0. Bao hilo lilifungwa katika dakika ya nane tu ya mchezo na kiungo Hilary Echessa, akiwa ndiyo kwanza amesajiliwa kutoka timu hiyo hiyo aliyoifunga.

Mechi hii ilichezwa kwenye uwanja wa Uhuru kwa sasa lakini zamani ukiitwa wa Taifa.

Wakati huo Simba ilikuwa inafundishwa na Patrick Phiri. Na ndiyo msimu ambao Simba ilitwaa ubingwa bila kufungwa.

Ulikuwa msimu wa kwanza wa wacheza Emmanuel Okwi na Joseph Owino kusajiliwa Simba ambao nao walicheza kwa mara ya kwanza mechi hiyo wakiwa na timu yao mpya.

2. Simba 0-0 Express (2010)
Simba iliadhimisha mwaka wake wa pili wa Simba Day kwa kulazimishwa sare ya bila kufungana na wageni waalikwa timu ya Express kutoka nchini Uganda kwenye uwanja wa Uhuru.

Timu hiyo pia ilikuwa chini ya kocha Phiri, huku ikiwa na baadhi ya wachezaji kama Ally Mustafa ‘Bathez’, Owino, Mohamed Banka, Rashid Gumbo, Okwi, Patrick Ochan, Shija Mkina, Amri Kiemba na Mussa Hassan Mgosi na Jerry Santo.

3. Simba 0-1 Victors (2011)
Mwaka wa tatu Simba iliadhimisha siku yake, ilipokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa timu ya Victors nayo pia kutoka nchini Uganda.

Mechi hii ilichezwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Bao la washindi lilifungwa dakika ya 70 kwa njia ya penati na Patric Sembuya.Simba ilikuwa chini ya kocha Milovan Cirkovic.

4. Simba 1-3 Nairobi City Stars (2012)
Ikiwa tena chini ya Cirkovic, Simba ilipokea kipigo cha mabao 3-1 toka kwa Nairobi City Stars kutoka nchini Kenya, mechi iliyochezwa kwenye uwanja mkuu wa Taifa. Huo ni mwaka wa nne wa Simba Day.

Mabao ya washindi walifunga na Duncan Owiti dakika ya 57, dakika ya 64 na Bruno Okullu dakika ya 64 na Boniphace Onyango kwenye dakika ya 79.

Bao pekee la Simba lilifungwa na Felix Sunzu kwenye dakika ya 15.

5. Simba 4-1 SC Villa (2013)

Simba ilifanya kufuru kwa kuisasambua bila huruma SC Villa ya Uganda mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa chini kocha Abdallah Kibadeni.

Magoli ya Simba kwenye tamasha hilo yalifungwa na Jonas Mkude kwenye dakika ya 43, William Lucian ‘Gallas’ dakika ya 53, na Betram Mombeki aliyefunga magoli mawili katika dakika ya 70 na 72.

6. Simba 0-3 Zesco (2014)
Kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Zesco kilikuwa ni cha tatu kwa Simba kwenye mechi zake sita za tamasha la Simba Day tangu lianzishwe miaka sita iliyopita.

Yalikuwa ni mabao ya Jackson Mwanza kwenye dakika ya 14, Clatos Chane dakika ya 64 kwa penati na Mayban Mwamba dakika ya 90.

Kwa matokeo haya yote, yanathibitisha kuwa Simba imecheza mechi sita za Simba Day tangu kuanzishwa, imeshinda mbili, sare moja na kufungwa mechi tatu.

7. Simba 1 - 0 SC Villa-2015

Kiungo Awadh Juma aliwainua vitini mashabiki wa Simba kwa kufunga bao pekee dakika ya 89 na kuifanya timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya SC Villa. 


Tayari baadhi ya mashabiki wa timu hiyo walikuwa wameshatoka uwanjani, wakiamini kuwa mechi hiyo ingetoka sare.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: