BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

PROF LIPUMBA AMGEUZIA KIBAO MAALIM SEIF, AMTAKA KURIPOTI HARAKA OFISI KUU YA CUF DAR AMPANGIE KAZI

Profesa Ibrahimu Lipumba kushoto na Maalim Self Sharif Hamad.

WAKATI Baraza Kuu la Uongozi Taifa la Chama cha Wananchi(CUF) limetangaza juzi kumfukuza uanachama Profesa Ibrahimu Lipumba, msomi huyo hang'oki katika nafasi yake ya uenyekiti wa chama hicho, amesema.

Aidha, Prof. Lipumba amemtaka Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Self Sharif Hamad ambaye alikuwa sehemu ya wajumbe katika kikao kilichomfukuza mjini Zanzibar, kuripoti ofisi kuu ya CUF jijini Dar es Salaam ili ampangie majukumu.

Baada ya kukutana kwenye kikao kilichoitishwa na Kamati ya Utendaji ya CUF, baraza hilo juzi lilitangaza kumvua uanachama mtaalamu huyo wa uchumi kwa maelezo kuwa amekiuka matakwa ya katiba ya chama na sheria za nchi.

Hata hivyo, katika mkutano wake na waandishi wa habari kwenye ofisi kuu ya chama hicho Buguruni, Prof. Lipumba alisema hatambui uamuzi uliofikiwa na baraza hilo kwa madai kuwa kikao kilichofikia uamuzi huo ni batili na hata kama kingekuwa halali, baraza hilo halina mamlaka kumfukuza uanachama.

Prof. Lipumba alidai kuwa kwa mujibu wa katiba ya CUF, mamlaka ya kumfukuza mwenyekiti wa chama ni mkutano mkuu wa wanachama pekee.

Alisema kwa sasa anaendelea na majukumu yake ya kawaida akiwa mwenyekiti na amepanga kukutana na Maalim Seif ofisini hapo kesho.

Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo, Prof. Lipumba alidai Maalim Seif na timu yake wamepanga kufika kwenye ofisi hizo siku hiyo na watamkuta na kuwapokea akiwa "ngangari kinoma", akiwa amejaa tele kwenye kiti.

"Mimi ninawakaribisha waje na nitawapokea, ofisi ya Katibu Mkuu iko hapa, na mimi siwezi kusema nimfukuze, ni haki yake kufika wakati wowote anaotaka isipokuwa nimwambie mimi watanikuta nimejaa tele kwenye kiti," alisema.

"Na akifika, kabla ya kwenda ofisi, apitie kwangu nimpangie majukumu, nitampokea na kumpatia mwongozo halali wa kuingoza CUF.

“Baraza Kuu haliwezi kutoa adhabu ya kumfukuza uanachama mwenyekiti wa taifa, isipokuwa mkutano mkuu, hata kama kikao hicho (cha juzi cha Baraza Kuu) kingekuwa halali, mimi sing'oki CUF na niko ngangari kinoma, nimejaa tele kwenye kiti na sina mpango wa kuhama chama hiki na nitaendelea kuongoza.

"Haya yaliyosemwa na kuandikwa kwenye vyombo vya habari ni ngonjera tu, hayaendi popote.” Prof. Lipumba pia alisema anatarajia kuitisha kikao cha Baraza Kuu katika kipindi kitakachotangazwa baadaye na atafuata utaratibu, kwa madai kuwa hatafanya kama inavyofanywa na wenzake walioketi Zanzibar.

BARA NA ZANZIBAR
Alisema lengo lake ni kuhakikisha anawaunganisha wana-CUF wa pande zote za Bara na Zanzibar na si kuwatenganisha.
Alisema ili kujenga muungano ulio imara, vyama vya siasa vinapaswa kuwa na mtazamo wa kitaifa bila kujali vipo Zanzibar ama Tanzania Bara.

“Hatuna CUF Bara na Zanzibar, chama chetu ni kimoja isipokuwa kinachonifedhehesha leo hii ni kwamba chama ambacho tulikuwa tunasimamia na kutetea haki, leo hii tumeanza kuivunja, hii ni aibu na niwaahidi watanzania kwamba nitahakikisha ninarejesha misingi ya chama iliyokuwapo hapo awali," alisema.

Baada ya Prof. Lipumba kuzungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Ulinzi wa CUF Bara, Abdallah Machela alisema mpaka sasa ofisi hizo ziko mikononi mwa kikosi cha ulinzi na kwamba ni wao pekee watatoa ruhusa kwa mtu ama kiongozi yeyote kuingia katika ofisi hizo mpaka mvutano uliopo uishe.
“Hatutoki hapa usiku na mchana,” alisema Machela.

Kabla ya kuanza kwa mkutano wa Prof. Lipumba na waandishi wa habari, Nipashe ilishuhudia ofisi hizo zikiwa chini ya kikosi cha ulinzi cha chama hicho ndani na nje.

Baadhi ya wafuasi walisema wamejitokeza kwa wingi katika ofisi hizo kwa ajili ya kumdhibiti Maalim Self asiingie katika ofisi hizo.


Wafuasi hao walikuwa wanasema hawataki kumuona Maalimf Self akiingia katika ofisi hizo na wako tayari kwa lolote mpaka pale atakapomtambua Prof. Lipumba kuwa ndiye mwenyekiti wa chama hicho.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: