KOCHA MSAIDIZI MBEYA CITY FC AFICHUA SIRI YA JAMHURI KIHWELU KUFUNDISHA SOKA TANZANIA.
KOCHA Msaidizi wa Mbeya City, Mohamed Kijuso, amesema siri kubwa ya kuimaliza Mwadui FC na kumstaafisha kocha Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ katika mchezo wao wa juzi, imetokana na wachezaji wake kufuata vizuri maelekezo ya makocha wao.
Mbeya City ilitoa kichapo cha bao 1-0 katika mchezo dhidi ya Mwadui uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya juzi na kusababisha kocha wa Mwadui Julio kutangaza kujiuzulu kufundisha soka la Tanzania kwa madai waamuzi wamekuwa wakimuonea.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kocha Kijuso iliyotumwa na Msemaji wa Mbeya City Dismas Ten kwa vyombo vya habari jana, ushindi wa Mbeya umetokana na juhudi za wachezaji kufanya kama walivyoelekezwa.
“Mchezo ulikuwa mzuri, vijana wamecheza kwa kufuata maelekezo ya Mwalimu, hili limetusaidia kuibuka na ushindi, hatukuwa vizuri kipindi cha pili lakini safu yetu ya ulinzi ilisimama imara kufuta makosa yote,” alisema Kijuso.
Kocha huyo alisema huu ni wakati mwingine wa kujiandaa na mchezo ujao kwa sababu tayari wana nguvu na ari kubwa kufuatia ushindi huo.
Kwa ushindi huo, Mbeya City imefikisha pointi 11 kwenye msimamo wa ligi ikishika nafasi ya saba baada ya kucheza michezo saba, kushinda mitatu, kupata sare mbili na kupoteza miwili.
Katika mchezo ujao, Mbeya City itaikaribisha Stand United kwenye uwanja huo utakaochezwa Oktoba 8, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment