MAHAKAMA YA KISUTU YATOA ONYO KWA TUNDU LISSU
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imetoa onyo kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kutokana na kutokufika mahakamani kusikiliza kesi ya kutoa maneno ya uchochezi inayomkabili.
Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa ametoa onyo hilo na tahadhari ya kisheria kwa Lissu kwa kuwa mshitakiwa huyo, hakufika mahakamani kwa sababu yupo Mwanza.
Kesi hiyo ilitajwa jana kwa ajili ya kusikilizwa na upande wa Jamhuri, ulikuwa na shahidi ambaye ni ofisa wa jeshi la polisi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Kimweri.
Kabla ya kuanza kusikilizwa, Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala aliomba kesi hiyo iahirishwe kwa kuwa Lissu yupo Mwanza kwenye kesi namba moja ya 2015 inayosikilizwa mbele ya Jaji Noel Chocha na imepangwa kusikilizwa mfululizo.
Wakili wa Serikali, Mohamed Salum alipinga ombi la kuahirishwa kwa kesi hiyo kwa sababu kwa mujibu wa Kifungu cha 148 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), mwenye mamlaka ya kutoa taarifa zinazomhusu mshitakiwa mahakamani ni mdhamini na si wakili.
Alidai, kutokana na kifungu hicho, ombi la wakili Kibatala ni batili pia aliiomba mahakama imueleze taratibu za kisheria, na kesi hiyo itakapotajwa tarehe nyingine, mshitakiwa afike mahakamani.
Mahakama ilikubali ombi la upande wa Jamhuri na kutoa onyo na tahadhari ya kisheria kwa mshitakiwa kutokufika mahakamani.
Hakimu Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 2 mwaka huu, kesi itakapotajwa tena.
Katika kesi hiyo inadaiwa Juni 28, mwaka huu katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa nia ya kushawishi na kufanya uchonganishi kati ya wananchi wa Tanzania na serikali, Lissu alitoa maneno ya uchochezi.
Inadaiwa alisema, “Mamlaka ya serikali mbovu ya kidikteta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote, huyu dikteta uchwara lazima apingwe kila sehemu, kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga, nchi inaingia ndani ya giza nene”.
0 comments:
Post a Comment