WANANCHI wengi wanaoishi miji mikubwa ukiwemo wa Arusha, wanakabiliwa na magonjwa yasiyoambukiza na yasiyojulikana kirahisi, kwa sababu ya matumizi ya vyakula na vinywaji visivyozingatia lishe bora. Hayo yalisemwa jana jijini Arusha na wataalamu wa afya wakiwemo madaktari bingwa wa magonjwa yasiyoambukiza katika zoezi linaloendelea la upimaji wa afya kwa hiyari, katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, ambapo wamebaini idadi kubwa ya watu wenye matatizo hayo, lakini wakiwa hawajui kama wanaumwa.
Akizungumza mmoja wa madaktari hao, Dk Rose Hyness, alisema uchunguzi uliokwishafanywa na wadau ikiwemo taasisi inayojishughulisha na magonjwa yasiyoambukiza nchini, umeonesha mkoa wa Arusha asilimia 30 ya watu wazima, wanakabiliwa na magonjwa ya sukari ambayo pamoja na kusababishwa na vyakula, pia yanachangiwa na kutofanya mazoezi.
“Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima wameiomba serikali kuweka mfumo unaoeleweka wa kuwawezesha wananchi kupima afya zao na ikiwezekana kutenga siku ya kupima afya, kama inavyotenga siku ya kufanya usafi, kwani watu wengi ni wagonjwa lakini hawajui na hawaendi hospitali hadi wanapozidiwa na kupoteza maisha,” alisema Dk Rose.
Mwajuma Ally na Nelson Sauga walisema watu wengi hasa wa kipato cha chini, hawana muda wa kupima afya zao kutokana na kujielekeza zaidi kupambana na ugumu wa maisha.
Walisema watu wengi wanapojisikia kuumwa wanakunywa dawa za kienyeji ama wanazonunua kwenye maduka ya dawa bila kupima.
“Ila tunapozidiwa ndio tunakwenda hospitalini na kujikuta matatizo yamekuwa makubwa na yanakuwa vigumu kutibika, hivyo vyema utaratibu wa kupima afya bure ukaendelea, sababu mimi nilivyosikia bure ndio nimekuja ila ingekuwa fedha nisingekuja maana sina,” alisema Sauga.
Katibu wa Taasisi hiyo inayojishughulisha na magonjwa yasiyoambukiza, Kasembo Kurwa alisema tatizo la ulaji na unywaji usiozingatia vigezo na watu kutofanya mazoezi ni kubwa zaidi maeneo ya mjini kutokana na urahisi wa upatikanaji wa vyakula na vinywaji, lakini pia ukosefu wa muda na maeneo ya kufanya mazoezi.
Alisema lengo la taasisi ni kufanya uhamasishaji na upimaji katika maeneo ya vijijini, ambako pia tatizo la wananchi kutokuwa na utaratibu wa kupima afya ni kubwa, likichangiwa na ukosefu wa hamasa na pia umasikini wa kipato.

0 comments:
Post a Comment