UONGOZI WA KLABU YA SIMBA SC WAINAMISHA USO CHINI NA KUPIGA MAGOTI YA UNYENYEKEVU KWA RAIS MAGUFULI
UONGOZI wa klabu ya Simba umewasilisha barua maalumu ya kumwomba radhi Rais John Magufuli, kutokana na kitendo cha mashabiki wa klabu hiyo kuharibu miundombinu ya Uwanja wa Taifa katika mchezo wa watani wa jadi uliochezwa Oktoba mosi, hali iliyopelekea kutimuliwa kutumia uwanja huo.
Tayari Simba imewasilisha barua hiyo kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, barua ambayo licha ya kuomba msamaha pia klabu hiyo imeiomba Serikali kuendelea kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kuwatimua.
Hatua hiyo ya Simba imekuja siku chache baada ya Serikali kupitia Waziri wa Wizara hiyo, Nape Nnauye, kutangaza kuzifungia klabu za Simba na Yanga kutumia uwanja huo kwa muda usiojulikana, baada ya kutokea kwa vurugu zilizopelekea uharibifu mkubwa wa mali za uwanja.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara, alisema klabu hiyo imeandika barua hiyo ikiamini kuwa Serikali ni sikivu na kuahidi kutorudia tena makosa hayo.
“Tunapiga magoti kuiomba Serikali itusamehe kwa hili lililotokea, tunafanya hivi tukiamini kuwa Serikali yetu kupitia Rais Magufuli ni sikivu, hivyo tunaamini kuwa itatusikiliza na hatimaye kuruhusiwa kuutumia uwanja, na tunaahidi kuwa tukio hili halitatokea tena,” alisema Manara.
Aidha, Manara aliongeza kuwa hadi sasa klabu hiyo haijafanya maamuzi yoyote juu ya uwanja mbadala hadi hapo itakapopata majibu ya barua hiyo.
“Tumepeleka maombi yetu, kwa hiyo tunasubiri majibu na tunaamini kuwa kabla ya mechi yetu na Kagera Sugar, basi tutajua upi ni uwanja wetu wa nyumbani,” alisema.
Klabu hiyo pia imetangaza rasmi Kamati ya Ushindi yenye wajumbe nane itakayoongozwa na Mwenyekiti, Musley Al Rawah, wakati Makamu Mwenyekiti wa kwanza ni Hassan Hassanoo.
“Tunaamini kuwa kamati hii yenye watu makini wataisaidia Simba kupata ushindi msimu huu, vigezo kadhaa vimezingatiwa katika uteuzi huu, kimojawapo kikiwa ni mjumbe kuwa mwanachama asiye na mashaka,” alisema.
Katika hatua nyingine, klabu hiyo imelilalamikia Shirikisho la Soka nchini (TFF), kupitia Bodi ya Ligi kwa kutokuwa makini na maamuzi juu ya mwamuzi Martin Saanya anayeendelea kuchunguzwa.
“Kadi aliyopewa Mkude imefutwa, lakini mwamuzi anaendelea kuchunguzwa, Simba tuna mashaka na hili, tunataka kufahamu uchunguzi huo unafanywa wapi wakati kila kitu kipo kwenye video na ni kwa muda gani,” alihoji Manara.Mtanzania
0 comments:
Post a Comment