ESTER BULAYA NA HADITHI YA MENDE KUANGUSHA KABATI INAPOKUWA KWELI KWA STEVEN WASSIRA
Wanayajwa wabunge vijana, ambao ni machachari katika siasa za Tanzania, Ester Bulaya ni miongoni mwao. Bulaya ni zao Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) aliyeamua kuhamia Chadema dakika za lala salama mwaka jana.
Awali, alikuwa ni Mbunge wa Viti Maalumu kundi la vijana wa CCM akiwakilisha Mkoa wa Mara, (2010-2015), lakini mwaka jana kabla ya Uchaguzi Mkuu alihama chama hicho kikongwe an kujiunga Chadema na akawania ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini mkoani humo.
Bulaya anajipambanua kuwa yeye ni miongoni mwa wanasiasa vijana wanaopenda kupigania haki za vijana bila kuangalia itikadi zao za vyama, dini wala kabila na ameendelea kusimamia hilo siku zote hata kabla ya kujitosa kwenye siasa.
Anaamini kwamba vijana wa Tanzania wanaweza kuungana na kufanya kazi kwa pamoja, hata kama watakuwa na itikadi tofauti za vyama, wataweza kulijenga taifa lenye maendeleo na lenye kujiamini.
"Ndio maana nimekuwa mstari wa mbele kushirikiana na vijana wote, na hasa wanasiasa wenzangu, wabunge wenzangu bila kujali wanatoka chama gani cha siasa ingawa baadhi ya wale wasiojua wamekuwa wakinitafsiri isivyo," amesema Bulaya.
Anatolea mfano wa urafiki wake na Halima Mdee ambaye sasa wako chama kimoja cha Chadema, kwamba familia zao ni marafiki na ndio maana walikuwa karibu bila kujali itikadi za vyama vyao.
Anabainisha kuwa msimamo wake wa kushirikiana na vijana wa vyama vya upinzani, ulisababisha wasiojua siasa wadhani kwamba ni msaliti, lakini ameweka wazi kuwa katika uwakilishi wake bungeni alikuwa tayari kwa lolote kwa kulitetea taifa lake.
"Niliamini kwamba CCM si baba wala mama yangu, na wala CCM si Tanzania! Kwa maana kwamba CCM, itapita kama vitu vingine, lakini Tanzania itabaki! Hivyo kitu muhimu ni Tanzania," anasema.
Anasema kuwa katika kutimiza lengo lake la kuwatumikia wakazi wa Jimbo la Bunda, aliamua kuhama CCM na kujiunga Chadema baada ya kubaini kwamba lengo hilo lisingetimia iwapo angeendelea kuwa ndani ya chama hicho tawala. Bulaya alimbwaga Wasira kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana lakini hata hivyo Wasira alipinga ushindi huo, kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi ilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, lakini ilikuwa inasikilizwa mjini Musoma, mkoani Mara.
Waliofungua kesi hiyo ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagira, ambao walidai kuwa mgombea waliemuunga mkono alinyimwa fursa ya kuhakiki matokeo na pia kuongezeka kwa idadi ya vituo vya kupigia kura visivyo halali.
Kesi hiyo ilioanza kusikilizwa jijini Mwanza na kisha mjini Musoma, ilihitimishwa Ijumaa iliyopita baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kumpa ushindi Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema) dhidi ya Stephen Wassira (CCM).
Baada ya ushindi huo, Bulaya amezungumzia kile ambacho anatarajia kukifanya ambacho kimsingi kimeonyesha mwendelezo wake wa kuweka pembeni itikadi za vyama na kusimamia maslahi ya umma.
Kwanza amekiri kukumbana na changamoto nyingi zilizomnyima usingizi kuanzia kwenye kampeni na hata baada ya uchaguzi na kulazimika kutumia muda mwingi mahakamani na kushindwa kuwatumikia vizuri wananchi wa Bunda Mjini.
"Changamoto kubwa niliyoipata ni kupotezea muda, badala ya kuwa jimboni, nilikuwa mahakamani mwaka mzima, lakini ushauri wangu kwa Wasira ni kwamba tushirikiane kuijenga Bunda," anasema Bulaya.
Mbunge huyo amesema pia kwamba yupo tayari kufuata ushauri wa Wasira kwasababu yaliyopita si ndwele bali wagange yajayo kwa mustakabali wa jimbo lao badala ya kuendeleza malumbano ya kisiasa.
"Sina mashaka kuhusu uzoefu wake ndio maana nikasema niko tayari kufuata ushauri wake, lakini cha msingi ni kwamba muda aliotumikia taifa hili na wana Bunda unatosha, apumzike ale pensheni yake atuachie tuendeleze pale alipoishia," amesema.
Amesema kuwa aliwahi kumuahidi Wasira kuwa ataendelea kumshinda, kwa madai kwamba alipata ubunge huo kihalali kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, hivyo kilichobaki sasa ni kuungana na kufanya kazi ya kuleta maendeleo wakazi wa jimbo hilo.
Bulaya amesema kuwa alimtahadharisha Wasira tangu anafungua kesi na kumwambia kwamba alimshinda kwa wananchi, akamshinda kisheria, lakini hakuridhika akakata rufaa na matokeo yake ndio hayo ya kushindwa tena.
"Wasira ametumikia nchi hii na jimbo la Bunda kwa miaka mingi, anatakiwa apumzike na kubaki kutoa ushauri, ndio maana niko tayari kumfuata ili anipe ushauri kwani siasa sio uadui, yaliyopita si ndwele tugange yajayo," amesema.
Wakati wa kampeni za uchaguzi Bulaya amesema kuwa alikumbana na misukosuko mingi kutoka kwa Wasira ikiwamo ya kubambikiwa kesi kwa lengo la kumkatisha tamaa na kwamba hawezi kuwa na kinyongo.
"Nilipoondoka CCM baadhi ya watu walidai nimemkimbia Wasira, lakini nilijua ninachokifanya, kwani nisingeweza kupambana naye nikiwa ndani ya CCM, kwa sababu ningewekewa mizengwe, ndio maana nikahama," amesema.
Bulaya anarudia tena kusema: "Siasa sio uadui wala chuki, bali wanaofanya hivyo wanaonyesha udhaifu na jinsi gani hawajakomaa kisiasa, lakini kimsingi suala la maendeleo halina itikadi, ndiyo maana ninamkaribisha mzee wangu Wasira tushirikiane kufanya kazi ya kuleta maendeleo Bunda."
Historia inaonyesha kuwa Bulaya, alizaliwa Machi 3 mwaka 1980, Ilala Dar-es-Salaam, akiwa darasa la sita, Shule ya Msingi ya Kurasini baba yake mzazi Amos Bulaya aliyekuwa askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa cheo cha meja katika kambi ya Pangawe, Morogoro alifariki dunia.
Akiwa kidato cha pili Shule ya Sekondari Makongo, mama yake Hadija Ismail naye alifariki dunia na akalelewa baba yake mdogo Paul Bulaya (Ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambaye alimsomesha hadi alipohitimu elimu yake ya sekondari na chuo.
Anasema baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, alijiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Morogoro na kupata Diploma ya Uandishi wa Habari na kisha mwaka 2002 alianza kazi katika gazeti la Uhuru mwaka hadi 2008.
Baadaye alikwenda nchini Marekani kusomea mambo ya uongozi, aliporejea akaanza harakati za kuwania ubunge na ndipo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 akajitosa na kufanikiwa kuibuka na ushindi.
Kama ilivyo kawaida yake aliendelea kuwa sauti ya vijana na watoto kwa kwa kuwatetea na kupigania haki ya mtoto wa kike huku akiamini kwamba njia pekee ya kumkomboa mtoto wa kike ni kumpa elimu.
"Katika siasa sikuibuka tu ghafla bali nilianzia mbali, kwani nilikuwa nikienda kwenye mikutano ya chama na mama yangu na kushirikina na watoto wenzangu wa chipukizi na kujifunza mengi ya msingi ningali mdogo," amesema.
Amesema kuwa aliendelea kukua katika hali hiyo hata akiwa ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM na kwamba alipoona amekomaa zaidi alimua kuwania ubunge wa jimbo ingawa kulikuwa na mizengwe.
Bulaya amesema kuwa alipobaini kwamba ndoto yake ya kuwatumikia wananchi wa Bunda kama mbunge inataka kuzimwa, aliona njia pekee ni kuhama kutoka CCM kwenda Chadema.
"Sikukurupa tu bali niliona mbali ndio maana nikaibuka na ushindi ambao umemsumbua Wasira na kuamua kunipotezea muda kwa kukimbilia mahakamani, lakini hayo yote yamepita kilichobaki tuijenge Bunda yetu bila kujali itikadi za vyama," amesema.Nipashe
0 comments:
Post a Comment