TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE YAONYESHA MAAJABU KATIKA MATIBABU YA MOYO TANZANIA
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuonesha maajabu katika matibabu ya moyo ambapo ndani ya wiki moja iliyopita imeweza kufanya matibabu ya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 17 kwa ufanisi mkubwa na kuandika historia ya aina yake.
Madaktari bingwa wa taasisi hiyo iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijiini Dar es Salaam wakishirikiana na madaktari bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Open Heart International (OHI) ya Australia ndio waliofanikisha upasuaji wa awamu hii uliowahusisha watoto 12 na watu wazima watano.
Kwa upasuaji huo wa wagonjwa 17 wiki iliyopita, kunafanya idadi ya waliopasuliwa moyo mwaka huu kufikia 345. Aidha idadi hiyo inaonesha ongezeko la kasi la utoaji wa huduma hiyo ukilinganisha na miaka iliyopita ambapo uwezo wake ulikuwa ni kwa wagonjwa 100 na kuandika historia ya aina yake katika Bara la Afrika.
Pamoja na mafanikio katika matibabu ya wagonjwa, idadi hiyo ya wagonjwa wanaotibiwa imepunguza mzigo wa serikali kugharamia matibabu nje ya nchi kwa karibu asilimia 70.
Mathalani kitendo cha wagonjwa 345 kutibiwa katika taasisi hiyo kwa mwaka huu pekee, kinafanya nchi kuokoa zaidi kidogo ya Sh bilioni 5.1, ambazo zingepaswa kutumika kwa upasuaji kama huo nje ya nchi, ambapo wataalamu wa afya wanasema mgonjwa mmoja hulazimika kutumia Sh milioni 15, kama kadirio la chini.
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji katika taasisi hiyo, Dk Bashiri Nyangasa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu zoezi la upasuaji la wiki iliyopita alisema madaktari bingwa hao kutoka Australia wakishirikiana na madaktari bingwa wa moyo wa taasisi hiyo walianza kambi ya kutoa tiba hiyo Novemba 19 na kumaliza Novemba 23.
Dk Nyangasa alisema katika kambi hiyo matibabu hayo 17 ya upasuaji wa moyo yalifanyika, 12 kati yake yakiwahusu watoto huku tisa kati yao wakifanyiwa upasuaji wa moyo uliohusisha kifua na watatu wakifanyiwa matibabu ya moyo bila upasuaji.
Aidha alisema watu wazima watano pia walifanyiwa matibabu ya moyo na kwamba huduma zote zilifanywa ndani ya wiki moja kwa mafanikio makubwa bila vifo kutokea, huku likiwepo tukio la upasuaji mkubwa wa moyo unaojulikana kitaalamu kama bypass.
Alisema kwa ujumla taasisi hiyo ya JKCI, imekuwa ikiboresha huduma siku hadi siku na kwamba utaalamu wanaopata madaktari wa taasisi hiyo ndani na nje ya nchi na ushirikiano wa madaktari bingwa wa nje, umewezesha taasisi hiyo kuongeza idadi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji hapo.
Akizungumzia upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 345 kwa mwaka huu, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na miaka iliyopita, Dk Nyangasa alisema mafanikio makubwa yamepatikana huku vifo vilivyotokea vikiwa chini ya asilimia 10, kiwango ambacho kinakubaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Huduma za moyo katika taasisi hiyo zilianza kutolewa mwaka 2008 na kadri miaka inavyosonga mbele ndivyo huduma zinavyozidi kuboreka zaidi, huku idadi ya wagonjwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na uelewa na mwamko wa wananchi wa kufuata huduma za afya katika taasisi hiyo.
Akizungumzia changamoto iliyojitokeza wakati wa kambi hiyo ya wiki iliyopita, Dk Nyangasa alisema walikabiliana na changamoto kubwa ya umeme kukatikakatika, wakati kazi ya upasuaji ikiendelea na hivyo kuwa kwenye wakati mgumu wa kutoa huduma.
Changamoto nyingine ni uhaba wa vitanda kwenye taasisi hiyo na kuwepo kwa vitanda 100 na kutokana na wingi wa wagonjwa inabidi wengine wasubiri hadi waliolazwa wapate matibabu na kuruhusiwa kuondoka ndio wafuate.
Kwa upande wake daktari Jayme Bennetts kutoka OHI alisema wamefanikiwa kutoa tiba kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo hapa nchini na kushauri jamii kubadilisha mtindo wa maisha kwa kuwa unachangia ongezeko la magonjwa ya moyo.
Hiyo inakuwa kambi ya 10 ndani ya mwaka huu kwa madaktari bingwa kuja nchini kushirikiana na wenzake kufanya matibabu kwa wagonjwa na kambi hizo ni sehemu ya mafunzo na inapunguza msongamano wa wagonjwa wanaosubiri tiba za magonjwa ya moyo na kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa walio hatarini.
Naye daktari bingwa wa upasuaji moyo kwa watoto, Dk Godwin Godfrey alisema matatizo ya moyo yako mengi kwa watoto na hiyo ni ukweli kuwa idadi kubwa ya watu duniani ni kundi la watoto.
Akizungumzia tatizo la moyo kuwa na tundu au matundu kwa watoto, Dk Godfrey alisema asilimia moja ya watoto wote duniani huzaliwa wakiwa na tatizo hilo lakini kadri mtoto anavyokua tatizo la tundu linaweza kuzibika bila matibabu, na yale yasiyoziba, uchunguzi hufanywa na matibabu kutolewa ikiwa ni pamoja na kufanyiwa upasuaji.
Takwimu zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2012 na 2015, wagonjwa 1,465 walitibiwa nje ya nchi kwa gharama za Serikali na karibu asilimia 50 ya wagonjwa hao walikuwa wanaugua magonjwa ya moyo.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment