BODI YA CHAKULA, DAWA NA VIPODOZI WATEKETEZA ZAIDI YA TANI 62 ZA VYAKULA VIBOVU ZANZIBAR
Na Mdau Salma Said, Zanzibar.
Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDB) imeangamiza zaidi ya tani 62 za vyakula vibovu na vilivyopitwa na wakati katika zoezi lililofanyika Kibele Mkoa Kusini Unguja.
Mkuu wa Idara ya Biashara na Uendeshaji wa ZFDB, Abdulaziz Shaib Mohammed amesema bidhaa hizo mbovu zinatokana na tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kujenga matumaini ya kuingiza faida kwa bidhaa wanazouza bila kuangalia usalama wa bidhaa hizo kwa afya za watumiaji.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi la kuangamiza bidhaa hizo, Abdulaziz ambae pia ni Mkuu wa operesheni wa uangamizaji amesema bidhaa hizo zimegundulika kufuatia operesheni iliyofanywa na Bodi katika maghala na maduka mbali mbali ya Unguja.
Mkuu wa Idara ya Chakula wa ZFDB, Aisha Suleiman amesema mchango mkubwa wa raia wema ndio uliofanikisha kugundulika bidhaa mbovu na zilizopitwa na wakati katika maduka na maghala mbali mbali.
Hata hivyo amewataka wananchi kujenga tabia ya kuchunguza tarehe ya kumaliza muda bidhaa wanazonunua na wanapogundua bidhaa imepitwa na wakati watoe taarifa katika Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Wakati huo huo Afisa Mkuu wa Idara ya Dawa na Vipodozi wa ZFDB, Mwadini Ahmada Mwadini amesema vipodozi haramu vilivyokamatwa baadhi yake vinakemikali zenye sumu na hazifai kwa afya ya binaadamu.
Dawa zilizoangamizwa katika operesheni hiyo ni mafuta ya kula lita 10,105, sukari tani 2.15, mchele tani 26, tende tani 10, bidhaa mchanganyiko za mboga mboga tani 13 na vipodozi tani tatu.
Kwa hisani ya Makame Mshenga.
0 comments:
Post a Comment