
KOCHA mpya wa Yanga George Lwandamina jana alianza vibaya baada ya timu yake kufungwa mabao 2-0 na JKU ya Zanzibar katika mechi ya kujipima nguvu iliyochezwa kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kwa kocha huyo Mzambia tangu achukue mikoba Hans van Pluijm aliyepelekwa nafasi ya Mkurugenzi wa Ufundi.
Mechi hiyo ni ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 17 mwaka huu ambapo Lwandamina aliitumia kuangalia kikosi chake.
JKU ilipata bao la kwanza katika dakika ya 11 likifungwa na Emmanuel Martin kwa shuti kali baada ya kuunganisha mpira wa kona fupi kutoka kwa Feisal Salum. Dakika ya 26 Martin aliifungia timu yake bao la pili kwa shuti kali ndani ya box baada ya kumzunguka beki wa Yanga Pato Ngonyani.
Katika mechi hiyo ya jana, Lwandamina alitumia vikosi viwili.
Kikosi cha kwanza kilichokwenda mapumziko kikiwa nyuma kwa mabao 2-0 kilikuwa: Ally Mustafa ‘Barthez’, Hassan Kessy, Oscar Joshua, Pato Ngonyani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Juma, Juma Mahadhi, Matheo Antony, Obrey Chirwa, Malimi Busungu na Geoffrey Mwashuiya.
Kikosi cha pili kilikuwa: Deogratius Munish, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Vincent Bossou, Andrew Vincent, Justine Zulu, Deus Kaseke, Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Simon Msuva, Amis Tambwe na Deus Kaseke. Hata hivyo kikosi hicho hakikubadi matokeo.
Mchezaji Zulu ambaye wengi walitaka kumuona alionyesha kiwango kizuri kwani alikaba na kuchezesha timu ingawa ameonekana mzito.

0 comments:
Post a Comment