Juma Mtanda, Morogoro.
Kumeibuka mgogoro kati ya wakulima na wafugaji uliopelekea watu watatu kujeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika kituo cha afya cha kijiji cha Duthumi ,wilayani Morogoro mkoani hapa.
Akizungumza kwa njia ya simu na MTANDA BLOG mjini hapa, Msaidizi wa mganga mkuu kituo cha afya Duthumi, Isaack Dominic alisema kuwa desemba 5 mwaka huu majira ya asubuhi na usiku walipokea watu watatu wakiwa na majeraha mwilini na kupatiwa huduma ya kwanza.
Dominic aliwataja watu hao kuwa ni Kondo Kinovu 60, Mohamed Kinovu (45) na Kelefe Paul (18).
Akifafanua juu ya majeruhi hao, Dominic alisema kuwa Kondo yeye alijeruhiwa kichwani na kushonwa nyuzi saba huku Mohamed akijeruhiwa sehemu mbili za kichwani na kuvunjika mfupa mmoja katika mkono wa kulia .
Mganga huyo alisema Kelefe alijeruhiwa mkono wa kushoto na kukatwa baadhi ya mishipa ya damu.
“Kondo alishonwa nyuzi saba kichwani baada ya kuchanika ngozi wakati Mohamed yeye alijeruhiwa kichwani na mkono na Kelefe mishipa yake ya damu ya mkono wa kushoto ilidhurika lakini sasa wagonjwa hao wanaendelea vizuri,”alisema Dominic.
Dominic alisema kuwa Kefele alifikishwa usiku kituoni hapo lakini kutokana na majeraha aliyopata alipoteza damu nyingi na kulazimika kumwekea chupa moja ya damu kwani mishipa ya mkono wake ilivujisha damu nyingi.
Mmoja wa majeruhi hao, akiongea na MTANDA BLOG kwa njia ya simu, Kondo Kinovu alisema kuwa yeye na mdogo wake Mohamed walijeruhiwa na kukimbizwa kituo cha afya baada ya kushambuliwa na wafugaji shambani kwao.
Kondo alisema kuwa wakiwa ndani ya shamba lao lenye mazao ya bamia, miwa na migomba ya ndizi walikisia kelele za kuanguka kwa kitu lakini hawakuweza kufahamu.
“Tulisikia kelele za kuangushwa kwa migomba ndani ya shamba letu na tulipofuatilia kwa ukaribu tuliona mifugo na vijana wawili wakidondosha migomba ya ndizi na kuwalisha mifugo wao,” alisema.
Kondo alidai kuwa baada ya kuwasogelea vijana hao walikuwa wakali hukuwakibishana .
“Vijana hao walianza kutushambulia kwa sime na fimbo katika miili yetu na kutujeruhi vibaya,” alisema.
Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo amelaani tukio hilo na kuwataka wakulima na wafugaji kutafuta njia iliyo bora ya kuishi hasa kipindi hiki ambacho kimekuwa na ukame na uhaba wa chakula kwa ajili ya mifugo.
“Silaha zinazotumiwa au kubebwa na wafugaji ni kwa ajili ya kujinda na maadui kama nyota na hatari nyingine na siyo zisitumike katika kushambulia binadamu wenzano.Lazima jamii hizi zizingatie kujiepusha na migogoro inayoweza kupelekea kupoteza uhai wa binadamu.”alisema Chonjo.
Chonjo alisema kuwa juzi kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Morogoro ilifika eneo la Kiegea katika hatua za kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema kuwa taarifa zilipo ndani ya jeshi hilo ni kuwepo kwa watu wawili waliovamiwa eneo la Duthumi.
“Bado upelelezi wa tukio hilo la Dhutumi hauja kamilika lakini ngoja tufuatilie kwa undani tukio hilo kwa kupata taarifa kutoka kwa mkuu wa polisi wilaya ya Morogoro maana baada ya kufika mahakamani ndipo tunaweza kusema lolote.”alisema Matei.

0 comments:
Post a Comment