BAADHI ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) walitwangana kwa mara nyingine tena nje ya viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salam wakati kesi kuhusiana na mvutano uliopo ndani ya chama chao ikishika kasi jana. Waliojigeuza mabondia ni waungaji mkono wa pande mbili tofauti katika kesi hiyo, kwa maana ya wale wa upande wa walalamikaji na upande wa walalamikiwa.
Wafuasi hao walishushiana vipigo baada ya Jaji Sakiet Kihiyo kutoa uamuzi wa kutokujitoa kusikiliza kesi ya madai ya iliyofunguliwa na bodi ya udhamini ya CUF dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ya kuzuiliwa kuingilia masuala yanayohusu chama chao.
Awali, Novemba 24 mwaka huu, wafuasi hao walitwangana mbele ya Jaji Kihiyo aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo baada ya wafuasi wanaodaiwa kumuunga mkono Maalim Seif kumzuia Profesa Ibrahim Lipumba kuingia kusikiliza madai dhidi yake.
Jana, Profesa Lipumba alifika katika viunga vya mahakama hiyo saa 7:00 mchana na mara alipoingia zikaibuka fujo kati ya walinzi wake na wa upande wa Bodi ya Baraza la Chama hicho, wanaodaiwa kuunga mkono uongozi wa chama hicho upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif.
Hata hivyo, polisi walifanikiwa kuingilia na kutuliza vurugu kubwa zilizoelekea kujitokeza mahakamani hapo.
MWENENDO WA KESI KORTINI
Wakili wa Serikali Mkuu, Job John, alidai mbele ya Jaji Kihiyo kwamba kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya uamuzi wa jaji kuendelea na kesi hiyo ama kujitoa.
Jaji alisema walalamikaji waliwasilisha sababu mbili za kuomba ajitoe kusikiliza kesi hiyo lakini hazina msingi wa kisheria na kwamba ataendelea kuisikiliza.
“Katika maombi ya namna hii, Jaji au Hakimu ana mamlaka ya kujitoa katika kesi yoyote kwa kushawishika na hoja za mwombaji… lakini katika kesi hii sijaona sababu za msingi za kunishawishi nijitoe na kwamba hoja za waombaji hazina ukweli,” alisema na kuongeza:
“Walalamikaji wamekuwa na tabia ya kumkataa Jaji/Hakimu ili wamtafute wanaomtaka wao… maombi haya hayana mashiko ya kisheria. Mahakama yangu inayatupilia mbali,” alisema Jaji Kihiyo wakati akisoma uamuzi wake.
Mbali na Msajili, walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ya madai namba 23/2016 ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Lipumba na wanachama wengine 11 wa chama hicho.
Awali, mahakamani hapo, Wakili wa Walalamikaji, Juma Nassoro, alidai kuwa wanaomba Jaji Kihiyo kujitoa kusikiliza kesi hiyo.
Aidha, wamewasilisha pingamizi dhidi ya majibu ya walalamikiwa kwamba yana upungufu wa kisheria.
Alidai kuwa viapo vya walalamikiwa vina upungufu wa kisheria na kwamba vilitoa maelezo ya uongo pamoja na mwapaji kuweka maelezo ya kuambiwa.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata, aliwasilisha pingamizi la awali kwamba mahakama hiyo haijatoa kibali cha kufungua kesi dhidi ya walalamikiwa.
Kesi hiyo bado haijapangiwa tarehe ya kuendelea kusikilizwa.

0 comments:
Post a Comment