BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KLABU YA YANGA YATUNISHA KIFUA KULIIPA SIMBA SH50 ZA MLINZI HASSAN KESSY


 
Mlinzi wa Yanga, Hassan Kessy.

KLABU ya Yanga imekataa kuilipa Sh. milioni 50 Simba kama ilivyoagizwa na Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, iliitaka Yanga kuilipa Simba Sh. milioni 50,000 na faini ya Sh. milioni 3 kwa kosa kumsajili beki Hassan Ramadhan Kessy kinyume cha utaratibu.

Lakini, mabingwa hao wa Tanzania wameandika barua TFF wakitaka hukumu hiyo ipitiwe upya kwa kuwa hawakubaliani na kulipa Sh. milioni 50.

Msemaji wa TFF, Alfred Lucas aliithibitishia Nipashe jana jioni juu ya Yanga kukataa kulipa fedha hizo, wakitaka hukumu ipitiwe upya.

“Ni kweli kuna barua kama hiyo Yanga wameleta wakipinga kulipa fedha hizo na wanataka hukumu hiyo ipitiwe upya. Barua imefika kwa wahusika inafanyiwa kazi, majibu yakitoka tutayatoa,”alisema Lucas.

Mapema Desemba Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, iliitia hatiani Yanga kwa kosa la kumsajili Kessy akiwa ndani ya mkataba na Simba.

"Kitendo cha Klabu ya Yanga kupeleka jina la mchezaji wa klabu nyingine CAF huku mchezaji huyo akiwa ndani ya mkataba na mwanachama mwingine wa TFF ni kosa kubwa," ilisema hukumu hiyo.

Taarifa ya Kamati ilisema kwamba kwa mujibu wa kanuni za Ligi kifungu cha 69 (5), Yanga inapaswa kupewa adhabu itakayowafanya wanachama wote waheshimu nafasi ya TFF kwenye suala la usajili na si kuanza kwenda CAF au kwingineko ili kulinda hadhi ya soka ya Tanzania.

Aidha, Kamati iliagiza Ofisa wa TTF aliyehusika ama kwa kushirikiana na uongozi wa Yanga au kwa kutochukua hatua stahiki kwa wakati, apelekwe kwenye mamlaka yake ya nidhamu, yaani, Katibu Mkuu wa TFF ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yake.

Na hiyo ni baada ya kupitia mawasilisho ya pande zote kwa njia ya mahojiano na vielelezo na kubaini Kessy alikuwa na mkataba na Simba uliokuwa unaisha Juni 15, mwaka 2016 na Yanga walikiri mbele ya Kamati kupeleka jina la mchezaji huyo akiwa ndani ya mkataba na klabu nyingine.

Kamati pia imesema TFF kupitia Sekretarieti yake ilikuwa na nafasi ya kuweza kuielekeza Yanga hatua stahiki za kuchukua ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Simba kama taratibu zinavyoelekeza.

"Kama hatua hii ingechukuliwa kwa wakati mwafaka mgogoro huu usingekuwa na sura ya sasa na pengine usingekuwepo. Simba SC walileta machapisho yanayotokana na mtandao/blog wa mtu waliomtaja kuwa ni Bin Zubeiry ukimwonyesha Mchezaji yuko na viongozi wa Yanga."

"Yanga ilionesha mkataba uliosainiwa na Hassan Hamis Kessy tarehe 20/6/2016 na hivyo hakukuwa na sababu ya msingi ya kufanya mambo yaliyoainishwa kwenye kipengele cha 2 na cha 4 kabla ya kumalizika kwa mkataba kati mchezaji Hassan Kessy na klabu ya Simba." "Bila kuathiri hadhi ya uanachama wengine wa TFF, Klabu ya Simba ni klabu kubwa kama ilivyo Klabu ya Yanga, umakini mkubwa upaswa kutumika katika kushughulikia klabu hizi ili kuepuka madhara yasiyokuwa ya lazima,"ilisema barua ya Kamati.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: