Juma Mtanda, Morogoro .
Mkazi wa mtaa wa Sanivina kata ya Kichangani, Martha Maeda (33) amelazwa katika wodi namba tatu hospitali
ya rufaa mkoa wa Morogoro baada ya kudaiwa kujeruhiwa kwa kuchomwa mkuki katika
mkono wake wa kulia majira ya saa 10 alfajili ya Januari 15 mwaka huu.
Tukio hilo linalodaiwa kuhusishwa na vuguvugu za siasa katika uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya
Kiwanja cha Ndege mkoani hapa ambapo Martha Maeda ni mwanachama wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema).
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili
hospitali ya mkoa mjini hapa jana, Martha Maeda alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira
ya saa 10 alfajili baada ya kambi yao kuvamiwa na watu wenye silaha za jadi katika
mtaa wa Kimunyu kata ya Kiwanja cha Ndege wakati wakiandaa chai kwa ajili ya
kuondoa baridi.
“Nilichomwa mkuki majira ya saa 10
alfajili baada ya mimi na wenzangu watatu tulivyoamka ndani na kwenda nje ili kuandaa
moto kwa ajili ya kuchemsha chai na muda mfupi ilipita gari ndogo na kusimama
usawa wa nyumba tuliyoweka kambi na kutelemka ambapo wanaume hao wasiopungua wanne
walikuwa na silaha kama mapanga, rungu, sime, fimbo, mkuki na kutuvamia.”alisema
Martha.
Baada ya watu hao kuwavamia, wenzake
watatu walifanikiwa kukimbia na yeye alipojaribu kukimbia alinaswa na kuni mguuni
kisha kuanguka chini na mmoja wa wavamizi hao kumchoma mkuki katika mkono wake
wa kulia akiwa chini na damu kuanza kutoka lakini alifanikiwa kuuchomoa na
wahalifu hao waliingia kwenye gari na kutokomea eneo hilo.alisema Martha.
Mganga Msaidizi wodi namba tatu ya
akinamama hopsitali ya rufaa mkoa wa Morogoro, Dk John Muneja alithibitisha
kumpokea majeruhi, Martha Maeda majira ya saa 11 alfajili januari 15 mwaka huu akiwa
amejeruhi katika mkono wa kulia baada ya kujeruhiwa na kitu chenye nja kali.
“Martha tulimpokea na kumpatia huduma ya
kwanza na sasa anaendelea vizuri na matibabu na tutaangalia na maendeleo yake.”alisema
Dk Muneja.
Msemaji wa chama cha demokrsia na
maendeleo (Chadema) wilaya ya Morogoro mjini, Shabaan Dimoso alieleza
kusikitishwa na tukio hilo na kudai ni mbinu chafu zinazofanywa na wapinzani
wao ili kuwadhoofisha katika kampeni za uchaguzi mdogo wa kata ya Kiwanja cha
Ndege ambapo wamemsimamisha mgombea.
“Hili ni tukio la nne kufanyiwa chama
chetu na hii inatokana na chuki zenye lengo la kuudhoofisha upinzani hasa
Chadema jambo ambalo sio sahihi kwa mustakabali wa misingi ya katiba ya nchi
hii yenye kufuata misingi ya haki.”alisema Dimoso.
Dimoso alieleza kwa kudai kuwa Chadema
imekuwa ikiandamwa kwa kufanyiwa matukio yasiyo ya kiungwana kutoka kwa
wapinzani wao lakini na jeshi la polisi wilaya ya Morogoro mjini nalo
likihusika kufanya hujuma.
“Hapa Chadema tayari tumepoteza kompyuta
mpakato (Laptop) mbili ambapo moja imechukuliwa kinguvu na askari wa jeshi la
polisi na nyingine ikiharibiwa vibaya kwa kuivunja jana (juzi) jioni na askari
hao hao baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea wetu
katika mtaa wa Bondwa.”alisema Dimoso.
Dimoso alidai kuwa Laptop hizo zilikuwa
zikitumika kwa ajili ya kupiga nyimbo za kuhamasisha wananchi na kuendeshea
vipaza sauti katika spika wakati wa mikutano ya kampeni ya kumnadi mgombea
udiwani wa Chadema kata ya Kiwanja cha Ndege, Salum Milindi.
Akielezea tukio la mwanachama wao
kuchomwa mkuki, Dimoso alisema kuwa hilo sio tukio la kwanza kuvamiwa katika
kambi ya Chadema kwani Januari 13 majira ya saa 2 usiku mwaka huu, mtu mmoja
alivamia kambi hiyo akiwa na panga kisha kudhibitiwa na baadaye taarifa ilitolewa
jeshi la polisi na kupewa Mor/RB/529/2017.
Dimoso ametoa wito kwa vyama vya siasa
vinavyoshiriki uchaguzi huo kuwa kufuata taratibu, sheria na kanuni za uchaguzi
ili kuendeleza amani katika kipindi hiki cha kampeni na hatimaye siku ya kupiga
kura.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa
Morogoro, Leonce Ferdinad amethibitisha kupokea taarifa za mtu mmoja kujeruhiwa
na mkuki na tukio hilo linafanyiwa uchunguzi ili hatua kali za kisheria zichukuliwe.
Ferdinand alisema jeshi la polisi
linachunguza tukio la mwanamke kuchomwa mkuki na kulazwa hospitali ya rufaa
mkoa wa Morogoro na hawana taarifa za askari wa jeshi hilo kuchukua ama
kuharibu kompyuta mpakato mbili (Laptop) na endapo taarifa itatolewa hawatasita
kulifanyia uchunguzi.
“Tumepokea taarifa za mwanamke kuchomwa
mkuki katika mkono majira ya saa 10 alfajili Januari 15 mwaka huu lakini tukio
la Chadema kudai jeshi la polisi imeharibu kompyuta mpakato na moja kuishikilia
taarifa hizo bado hajafika.”alisema Fernandi.
Ferdinand alisema kuwa matukio yote
yaliyofanyika ni kinyume na sheria hivyo kama kuna mtu atapeleka malalamiko yatafanyiwa kazi kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria haijalishi ni askari ama laa uhalifi ni uhalifu tu
Kaimu kamanda huyo aliongeza kwa kusema kuwa jeshi la polisi ndilo lenye jukumu
la kuchunguzu matukio yote ilimradi taarifa imetolewa na kutolea ufafanuzi.
0 comments:
Post a Comment