BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

AGUSTINO MREMA AANZA KUJIPAIMA MWENYEWE VITA YA DAWA ZA KULEVYA


MWENYEKITI wa Bodi ya Parole, inayoshughulikia msamaha wa wafungwa magerezani, Agustino Mrema, amesema vita dhidi ya dawa za kulevya ameanza kupambana nayo baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli, kushika nafasi hiyo.


Mrema alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema muda mfupi baada ya kuanza kazi katika nafasi hiyo alianza kupambana na vita hiyo kwa kuzungumza na vijana wanaotumia dawa za kulevya ikiwamo kuwashawishi wawataje wafanyabiashara wa biashara hiyo haramu.

Aliongeza kuwa vijana hao walikuwa wanagoma kuwataja wahusika wakihofia usalama wao, lakini aliamua kuwapeleka katika vituo kwa ajili ya kuwasaidia kupata matibabu.

Mrema alisema kupambana na vita hivyo ilikuwa ni miongoni mwa mikakati yake aliyokuwa ameiweka baada ya kuteuliwa kuhakikisha anawaelimisha wananchi hususani vijana kuepukana na masuala ya uhalifu ambayo yangewasababisha kukutwa na hatia.

Pia alisema lengo lake ilikuwa ni kuhakikisha uhalifu unapungua na hivyo kuepuka kujaza magereza kutokana na masuala ya uhalifu.

"Kwa hiyo nina mshukuru sana Rais John Magufuli kwa kutia mkono wake katika suala hili la vita dhidi ya dawa za kulevya, mimi nilianza mapema kwa hiyo nashukuru imeendelezwa, naahidi tuko pamoja katika vita hii, hata ushauri nilishaanza kuutoa kwa vijana walioathirika," alisema Mrema.

"Nimekuwa nikitoa ushauri nasaha na elimu kuhusu umuhimu wa kutii sheria bila shuruti kwa makundi mbalimbali ya vijana kutokana na tabia na mienendo waliyonayo kuliko makundi mengine, lengo ni kuhakikisha hawaingii hatiani na hivyo kusababisha msongamano wa wafungwa kwenye magereza, mahabusu nchini yaani kupunguza idadi ya wafungwa watarajiwa."

Alisema vita nyingine alianza kupambana nayo kwa ajili ya kupunguza idadi ya wahalifu baada ya kuanza kazi hiyo ni waendesha bodaboda, vibaka, wasichana wanaouza miili yao, au dada pamoja na kaka poa.

Akizungumzia hali ya magereza nchini, Mrema alisema hivi sasa inakabiliwa na changamoto ya kujaa wafungwa kutokana na baadhi yao kushindwa kulipa faini wanazodaiwa na Mahakama na hivyo kulazimika kuendelea kuishi magerezani hata pale wanapomaliza vifungo vyao.

" Kuna wafungwa ambao wamefungwa baada ya kushindwa kulipa faini kama ilivyoamuliwa na Mahakama na ndio maana nilihamasisha wasamaria wajitokeze ili kusaidia kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani na ndio maana nimekuwa nikiwaelimisha vijana kuepuka vitendo vya uhalifu ili wasifungwe maana wakifungwa wanajaza magereza yetu, " alisema.

Mrema alidai kwamba wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimtuhumu kwamba anaendesha bodi hiyo kama mtu binafsi na kwamba hakuwahi kufanya hivyo japokuwa uteuzi wa wajumbe wengine ulikuwa haujakamilika.

Alisema tayari uteuzi wa wajumbe wa wengine wa bodi hiyo umekamilika na kwamba inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Machi 3 mwaka huu na Waziri wa Mambo ya Ndani.

Alimshukuru Rais Magufuli kwa kumsaidia kumpeleka India kwa ajili ya matibabu baada ya kupatwa na maradhi hivi karibu. 


"Ninamshukuru sana Rais, hivi mnavyoniona hapa nilikuwa naumwa nilikuwa na hali mbaya, lakini namshukuru Rais na wasaidizi wake waliohakikisha nimepata matibabu na hivi sasa nimepona," alisema Mrema.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: