BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ALIYEKUWA MBUNGE WA CHADEMA JIMBO LA LONGIDO ADONDOKEA PUA TENA MAHAKAMANI


Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Longido, Onesmo Ole Nangole (Chadema).

RUFANI ya aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Longido, Onesmo Ole Nangole (Chadema) ilitupwa na Mahakama ya Rufani jana, baada ya korti hiyo kuona alikiuka amri ya mahakama iliyomtaka afanye marekebisho ya rufani yake na siyo kuiandika upya.

Akisoma uamuzi huo jana, Msajili wa Mahakama Rufani nchini, Amir Msumi, alisema rufani hiyo imeondolewa kwa gharama kutokana na pingamizi lililowasilishwa mahakamani hapo.

Rufani hiyo ilisikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na mwenyekiti Jaji Bhernard Luanda.
Majaji wengine waliosikiliza rufani hiyo Stella Mugasha na Kipenka Mussa.

Msumi alisema majaji hao wameiondoa rufani hiyo kwa gharama, kwa sababu iliandikwa upya.

Nangole alikuwa akipinga kutenguliwa ubunge wake, Juni 29, mwaka jana na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Akifafanua, Msumi alisema majaji walibaini ukweli kuwa upande wa Nangole ulikiuka amri ya mahakama iliyotolewa Oktoba 24, mwaka jana, kuwa waongeze majina ya Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini wakaenda kuandika upya.

“Upande wa mkata rufani, alichokifanya, badala ya kuongeza kama mahakama ilivyomwagiza, wakaandika upya rufani yao kinyume na maagizo ya mahakama, hivyo tunaiondoa rufani hii mahakamani,” alisema.

Aidha, mahakama hiyo iliamuru upande wa Nangole kulipa gharama za wakili mmoja wa upande wa mjibu rufani na kukataa ombi la Dk. Masumbuko Lamwai la kutaka walipwe mawakili watatu.

Dk. Lamwai, akimwakilisha mjibu rufani ambaye ni aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, aliiomba mahakama hiyo kutupa rufani ya Nangole mwanzoni mwa wiki.

Katika ombi lake, Dk. Lamwai alisema wanapinga kusikilizwa kwa sababu kuna mapungufu kisheria na ongezeko la maneno nje ya maagizo ya Mahakama.

"Tunashangaa sasa hawa wenzetu wamekwenda kuongeza na kuweka maneno mengine mengi ambayo mahakama haikuwaelekeza kuongeza, na kusababisha ongezeko la vitabu vya taarifa badala ya saba na vikawasilishwa nane," alidai Dk. Lamwai mwanzoni mwa wiki mbele ya majaji hao.

"Hii hatukubali, ipo nje kisheria, wamekwenda kujaza maneno yao wenyewe."

Alisema kutokana na kasoro hizo wanaomba rufani hiyo isisikilizwe na mahakama hiyo iamuru mleta maombi kulipa gharama.

Ndipo jana Msajili Msumi aliposema zaidi kuwa kabla ya kutoa uamuzi huo, majaji hao walijiridhisha kwa kuangalia Kamusi ya Kiswahili inasemaje kuhusu tafsiri ya neno marekebisho, ambapo walibaini kuwa ni kufanya marekebisho madogomadogo sio kuandika upya kama walivyofanya waleta maombi.

HAIPO TENA
Akizungumza baada ya uamuzi huo kutolewa, Dk. Lamwai alisema “mahakama haikuwa na njia nyingine zaidi ya kuitupilia mbali rufani hiyo na sasa haipo tena."

"Labda waombe kibali kuleta rufani tena nje ya muda, lakini lazima waeleze sababu ya kutotii maelekezo ya mahakama.”

Lamwai alimshauri Nangole kukubali kurudi katika uchaguzi, kwani huko labda ataipata haki, lakini mahakama imejidhihirisha hawezi kupata haki anayoitafuta.

Dk. Kiruswa, alishukuru mahakama kuharakisha kumpatia haki yake na kumpa furaha na ana amini hata wangeenda kusikilizwa rufani yenyewe angeshinda kwa sababu haki ni yake.

Wakili wa Nangole, Method Kimomogolo alisema wanatafakari uamuzi huo na wataangalia usahihi wake, ikiwa pamoja na kushauriana na mteja wao kama warudi kwenye uchaguzi au wakate rufani nyingine mpya.

Nangole alikataa kusema chochote.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Silvangilwa Mwangesi, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo mwaka jaa, alisema katika uchaguzi huo, kulikuwa na dosari nyingi na hivyo akatengua matokeo ya uchaguzi wa ubunge na kuamuru urudiwe.

Moja ya dosari hizo ilitajwa kuwa kujazwa matokeo ya Ubunge kwa kutumia fomu namba 21c za matokeo ya Udiwani badala ya kutumia fomu namba 21b.

Alisema kuwa baada ya kutokea dosari hizo, ilitakiwa msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Longido, Felix Kimario atoe maelezo juu ya uamuzi wa kutumia fomu hizo, lakini alipofika hakuweza kufanya hivyo, hivyo mahakama ikaona ilifanywa kwa makusudi.


Pia Mahakama Kuu ilijiridhisha kuwa kulikuwa na fujo katika chumba cha majumuisho ya kura ambazo zilianzishwa na Ole Nangole.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: