BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

APATA MTOTO MCHANGA BILA YA KUJIFUNGUA SHINYANGA


WATOTO hupatikana baada ya mama mzazi kujifungua, lakini kwa watu wasiofahamika uleaji wa ujauzito kwa miezi tisa haukuwa lazima kwao baada ya mtoto mchanga wa kike mwenye umri wa siku sita kuibwa ndani ya wodi ya wazazi; katika Hospitali ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga.

Mtoto huyo aliibiwa wakati mama mzazi wa mtoto huyo, Zuhura Khamis akioga bafuni huku mwanaye akimuacha amelala kitandani katika wodi hiyo.

Muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, Konchesta Felix, alisema mtoto huyo aliibiwa baada ya yeye kwenda wodi nyingine kuwahudumia wagonjwa, lakini alimuacha mtoto huyo akiwa na mama yake.

“Niliporudi kutoka wodi nyingine, nilipewa taarifa za kuibiwa kwa mtoto huyo...ni jambo la kusikitisha na kushangaza," alisema muuguzi huyo wa zamu.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Emmanuel Kadelya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa lilitokea juzi saa 1:00 asubuhi baada ya mama yake kupelekwa bafuni kuoga.

Aidha, Dk. Kadelya aliwatupia lawama walinzi wa hospitali akisema wamekosa mpangilio mzuri wa ulinzi kwa watu wanaoingia hospitali kuona wagonjwa na kutoka.

“Walinzi wanapaswa kujipanga na kudhibiti watu wanaoingia holela katika wodi,” alisema Dk. Kadelya na kuongeza:

“Ni kweli mama kajifungua kwa operesheni, lakini jukumu la kuangalia mtoto ni lake, akitoka leba akiwa hajitambui, basi mtoto atalindwa na wauguzi wetu hadi hapo atakapopata fahamu."

Kwa upande wake, Suzana Bundala, mama mzazi wa Zuhura, alielezea kusikitishwa na tukio hilo hasa akizingatia bintiye alijifungua kwa njia ya operesheni na ndiye alikuwa mtoto wake wa kwanza.

Matukio ya wazazi kuibiwa watoto yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara nchini, hata hivyo.

Juni 22, 2012, Modesta Sumbuko aliibiwa mtoto mchanga wa kiume wa siku tatu na watu wasiojulikana, kwenye wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga.

Sumbuko alidai kuwa mwanaye aliibiwa saa 11 alfajiri wakati akiwa amelala na kwamba baada ya kuamka aliangalia na kukuta mtoto hayupo.

Machi 16, 2016, hali ya sintofahamu iliibuka katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, baada ya mtoto mchanga wa siku tano kuibiwa wodini katika mazingira ya kutatanisha.

Akisimulia tukio hilo, mama mzazi wa mtoto huyo, Sinyari Lucas mkazi wa Simanjiro mkoani Manyara, alisema lilitokea usiku.

Lucas alisema wakati akiwa kitandani muda wote kabla ya kulala alikuwa na mtoto wake, lakini ghafla aliposhituka usiku alikuta hayupo. 


Wazazi waliokuwapo kwenye wodi hiyo walisema muda wote mzazi huyo alikuwa amelala kitandani na mtoto wake, lakini usiku walishangaa kumsikia anapiga kelele za kuibiwa.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: