BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KARIAKOO LINDI YAPUMULIA MASHINE LIGI DARAJA LA PILI TANZANIA BARA.

Mlinzi wa timu ya Kariakoo Lindi, Khalfan Mwande kushoto akiwania mpira na mshambuliaji wa Burkina FC, Thadei Isidoli wakati wa mchezo ligi daraja la pili Tanzania bara uliofanyika uwanja wa jamhuri Morogoro ambapo katika mchezo huo Kariakoo Lindi ilikubali kipigo cha bao 1-0.

Juma Mtanda, Morogoro.

Jahazi la timu ya soka ya Kariakoo Lindi ligi daraja la pili Tanzania bara imeendelea kudidimia baada ya kutandikwa bao 1-0 na Burkina FC katika mchezo mkali uliopigwa uwanja wa jamhuri mkoani Morogoro.

Bao la Burkina lilipachikwa wavuni na Hassan Mkota dakika ya 64 kufuatia kuunganisha vyema krosi iliyomiminwa na winga, Thadei Isidoli na kumkuta mfungaji aliyefumua shuti la juu kwa mguu wa kushoto na kujaa wavuni.

Kutokana na matokeo hayo, Kariakoo Lindi imeendelea kuburuza mkia kwa kukusanya pointi sita huku ikibakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Changanyikeni FC ya Dar es Salaam ambapo imejiweka katika mazingira hatari zaidi ya kushuka daraja.

Kariakoo ilijaribu kutengeneza mashambulizi ya kupata bao na kusawazisha lakini ngome ya ulinzi ya Burkina ilikuwa imara kuondosha hatari zote katika lango lao.

Cosmo Politan Fc ndio wanaongoza kundi hilo kwa kukusanya pointi 18 wakati Burkina FC yenyewe imefikisha pointi 14 na kuepuka hatari ya kushuka daraja.

Akizungumza na MTANDA BLOG mara baada ya kumalizika kwa mchezo, huo Kocha mchezaji wa Kariakoo Lindi, Jonathan Moses alisema kuwa kufanya vibaya kwa timu yao kunatokana na kukosa kocha kwa kipindi kirefu baada ya kocha wa awali kuondoka.

“Hii timu haina kocha tangu kuanza kwa michezo ya hatua ya pili na mimi ndiye kocha mchezaji na mpaka sasa tuna pointi sita na tupo mkiani katika msimamo wa ligi na mchezo wa mwisho tutacheza na Changanyikeni FC jijini Dar es Salaam na endapo tutashinda tutafikisha pointi tisa tu ambazo tayari zimepitwa na wenzetu.”alisema Moses.

Moses alisema kuwa kuondoka kwa kocha mkuu kumeathiri zaidi mwenendo wa timu katika ligi daraja la pili na kujikuta wakiambulia vipigo vinavyowafanya kuburuza mkia.
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment