Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameendelea na staili yake yenye utata ya kutangaza majina ya watu anaotaka waripoti kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusu biashara na utumiaji wa dawa za kulevya.
Baada ya awamu ya kwanza kuwalenga wasanii, jana alitaja orodha ya watu 65 iliyohusisha wanasiasa, wafanyabiashara wadogo na wakubwa, viongozi wa dini na wamiliki wa hoteli na migahawa, akisema wanaweza kuwa na taarifa zitakazoisaidia polisi kuwabaini wauzaji wa dawa hizo.
Makonda, ambaye mbinu yake ya kutaja majina hadharani inapingwa na watu mbalimbali wakiwemo wabunge, jana alianza kwa kueleza njia zinazotumiwa na wasafirishaji wa dawa hizo duniani kupitishia mizigo Tanzania kabla ya kusafirishwa kwenda nchi nyingine.
Alisema mizigo ya dawa hizo zinazojulikana pia kwa jina la mihadarati, husafirishwa kwa njia ya meli na kushushiwa kwenye klabu za starehe na bandari bubu, nyingine husafirishwa kwa kutumia magari ya mitumba yanayonunuliwa Japan.
Alisema ameamua kutaja watu hao kwa kuwa baadhi wanamiliki klabu za starehe ambazo ziko ufukweni akidai kuwa huenda dawa hizo hushushwa huko, klabu za usiku ambako biashara hufanyika na wamiliki wa makampuni ya mafuta.
Makonda alitaja majina ya watu hao bila ya kuhusisha moja kwa moja na tuhuma za kuuza au kutumia dawa hizo, lakini akisisitiza kuwa wanaweza kuwa na taarifa zitakazosaidia polisi.
“Kama mnavyofahamu kuna watu niliwaita pale central (kituo kikuu cha polisi) na waliweza kufika. Kuna tofauti kubwa kati ya kuitwa na kukamatwa. Mkuu wa mkoa ana nafasi ya kumwita mtu yeyote, na kwa sababu yeye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, anaweza kuvitumia vyombo vyake kujiridhisha kwamba kuna moja, mbili, tatu na hatua zaidi zikachukuliwa,” alisema Makonda akitetea hatua yake ya kuwataja majina watu anaotaka kuhojiano nao polisi.
“Unapoitwa na mkuu wa mkoa, unapewa haki yako ya msingi ya kusikilizwa. Kwa sababu kuna mambo yanatoka ndani na watu wanatoa taarifa mitaani, wanazifikisha kwenye vyombo husika, nafasi ya kwangu ya kwanza ni kupata fursa na wewe kukusikiliza. Na kampeni hii ya madawa ya kulevya si ya kwenda kimyakimya.”
Katika orodha hiyo, ambayo ina tatizo la uhakika wa majina kulingana na watu hao maarufu, wamo watu kama mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye Makonda alimtaja kama Aikaeli Mbowe ingawa katika kufafanua alisema ni mbunge wa Hai na kwenye taarifa yake ya maandishi ameandikwa kama “Philemoni Mbowe”.
“Kaka yangu Aikaeli Mbowe, nafikiri mnamfahamu. Anaishi hapa, ni mbunge wa Hai (Kilimanjaro), lakini bahati nzuri ni mkazi wa Dar es Salaam. Naye tunamhitaji Ijumaa,” alisema Makonda.
Hata hivyo, jana jioni Makonda alifafanua kupitia mitandao ya kijamii kuwa alimlenga Freeman Mbowe.
Pia amemtaja mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan, ambaye katika taarifa hiyo ya Makonda iliyo na mwandiko wa mkono, inaonyesha anaitwa “Idd Azan Zungu”.
Makonda pia alimtaja Yusuf Manji bila ya kutoa maelezo zaidi tofauti na kwa wengine.
Kuhusu Gwajima, Makonda alianza kwa kutomtaja jina akihoji waandishi kama wanamfahamu na walipomtaka ataje akakubali, lakini akaendelea na majina mengine kabla ya kumtaja.
“Yule mchungaji ni Gwajima, naye nitahitaji kukutana naye,” alisema bila ya kutaja ni wa kanisa gani, ingawa kwenye taarifa yake iliyoandikwa kwa mkono kamtaja kwa jina la Josephat Gwajima.
Orodha hiyo, ambayo pia haijasainiwa, imewataja watu wengine kwa jina moja, baadhi kwa majina yanayoonekana kuwa ni ya umaarufu wa mitaa wanakoishi na wengine kutajwa kama wamiliki wa hoteli na klabu za starehe.
Makonda alisema lengo si idadi ya waliokamatwa au idadi ya waliotajwa ili wawapate wahusika halisi.
“Kampeni hii si ya kufanya kimyakimya. Kuna watu wanasema hii kitu ungeifanya kimyakimya kwa sababu tumeshafanya kimyakimya kwa miaka mingi, lakini bado tatizo limeendelea kuwa kubwa,” alisema Makonda.
“Listi (orodha) hii ni kubwa kidogo. Si rahisi kusoma mmoja mmoja. Mimi naamini vita hii si ngumu, tumewapa sana nguvu wauaji hawa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, tukajijengea hofu, tukaacha kuwagusa, tukaona hawagusiki na matokeo yake tunateketea sisi. Sisi ni wengi kuliko wao, nia ya Mungu na Rais wetu (John) Magufuli ni njema kwa Taifa letu.”
Makonda pia aliwataja baadhi ya wamiliki wa casino na wafanyabiashara nyingine, huku akiwataka wenyeviti wa mitaa kuendelea kutoa majina ya washukiwa.
Kuhusu mbinu zinazotumiwa na wasafirishaji wa dawa hizo zilizopigwa marufuku duniani, Makonda alisema mara nyingi hutumia usafiri wa meli.
Alisema mbinu kubwa ni kupakia dawa hizo katika mizigo ya sukari na baadaye kuiweka kwenye mapipa ambayo kabla ya kuwasili Bandari ya Dar es Salaam, huwekwa kifaa maalumu cha utambuzi wa eneo (GPRS) na kutupwa baharini na baadaye wamiliki wa mizigo huifuata na kupitishia bandari bubu za Bagamoyo mkoani Pwani, Zanzibar na Tanga.
“Wananunua kutoka Pakistan na wanakuja moja kwa moja na meli. Wanachofanya ni, meli ikishapakia mizigo wanachukua boti zao wanapakia dawa kwenye mifuko kama ya sukari kisha wanapakia kwenye mapipa wanayaingiza kwenye meli, ikikaribia kwenye bandari, yapo maeneo matatu ambayo mapipa hayo yanatupwa baharini,” alisema Makonda.
Akifafanua zaidi alitaja maeneo hayo kuwa ni Tanga, Bagamoyo na Zanzibar na kusema kwamba mara nyingi mapipa hayo yenye dawa za kulevya hutupwa ikiwa na GPRS.
Alisema wafanyabiashara hao wanapofika bandarini mizigo huyo huwa haina dawa za kulevya na inapakuliwa mizigo halali na baadaye timu yao hurudia mapipa hayo kwa njia ya boti na kuyachukua.
“Wanachokifanya wanakuwa na mashine zao za kubaini GPRS. Wanayaopoa, wanatoa dawa za kulevya wanasafirisha mpaka Mtwara na kisha wanaingiza Afrika Kusini,” alisema Makonda.
Aliitaja njia ya pili kuwa ni ya magari, ambayo alisema yananunuliwa Japan, lakini yanapelekwa Bombay nchini India au Pakistan kwa ajili ya kupakia mihadarati hiyo.
“Kwenye ramani huwezi kufanya mzunguko huo (wa kupeleka magari India na Pakistan kwanza). Wanachokifanya ni kununua magari wanaweka mizigo yao sehemu nyingine ili wafikishe mizigo hiyo nchini. Ukiangalia, utaona ni mzunguko mrefu sana. Wana magodown (maghala) hapa na bei zao (za magari) zipo chini. Sina maana wote wenye bei za chini wanasafirisha,” alisema.
Alisema wapo wenye sehemu zao za kuegeshea boti ambao wanafanya kazi kwa uhuru kwa kuwa boti zinaingia na kutoka kwa uhuru.
Aliitaja njia ya tatu kuwa ni kupakia mzigo wa dawa za kulevya katika meli zinazokuja na mafuta, kwa kuwa “kazi yetu ni kuangalia mafuta kama yana viwango na kama kila kitu kimezingatiwa (na si kukagua mihadarati). Wanatumia mfumo huo kusafirisha”.
Aliitaja njia ya nne kuwa ni kuwabebesha vijana kwa ahadi ya malipo ya fedha na badala yake kuwatelekeza wanapokamatwa.
Alimtaja mfanyabiashara mmoja ambaye alidai anasafirisha wasichana wa umri wa kati ambao hubebeshwa dawa za kulevya na dola 5,000 za Kimarekani (sawa na takribani Sh10 milioni) kwa ajili ya kuonyesha kuwa wana kiwango cha kutosha cha fedha kukidhi mahitaji ya uhamiaji ya China.
“Akifanikiwa kuingiza mzigo, analipwa dola 7,000. Mama huyu ana duka kubwa Sinza na Tanga. Tulikuwa tunamfuatia na baadaye tukagundua baada ya kuangalia kampuni ya kukata tiketi,” alisema.
Alisema walibaini kuwa mama huyo huwa halipi nauli kwa fedha taslimu, ili hao vijana wakikamatwa wapotee na kwamba sasa wapo wawili waliokamatwa China na ameshawatelekeza.
Makonda alisema kuwa msako wake unajumuisha pia Watanzania walio nje ya nchi ambao ni wakazi wa Dar es Salaam na kuwataka waripoti polisi mara watakaporejea nchini.
“Nimeshaelekeza watu wa Airport (uwanja wa ndege) kwamba watakapotua, moja kwa moja waelekezwe central. Warudi haraka na wakibaki huko tutawafuata. Zipo njia nyingi na mawasiliano mengi.”MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ MADAWA YA KULEVYA YAWATIKISA VIGOGO TANZANIA, WAMO AKINA MBOWE, GWAJIMA, MANJI WAITWA POLISI
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment