TANZANIA KUZALISHA SUKARI TANI 420,000.
Mkurugenzi mkuu wa bodi ya sukari Tanzania, Henry Semwaza akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa tasnia ya sukari kujadili mabadiliko ya muundo wa vyama vya wakulima wa miwa katika kiwanda cha Sukari Kilombero kilichofanyika jana.PICHA/MTANDA BLOG.
Juma Mtanda, Morogoro.
Tanzania ipo katika harakati za kujitosheresha kwa sukari baada ya kuweka mipango mkakati wa kuongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 300,000 hadi kufikia tani 420,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2020/2021 ili kukabiliana na upungufu wa sukari hapa nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa tasnia ya sukari kujadili mabadiliko ya muundo wa vyama vya wakulima wa miwa wilayani Kilombero, Mkurugenzi mkuu wa bodi ya sukari Tanzania, Henry Semwaza alisema kuwa ili kufikia malengo hayo serikali imetoa maelekezo kwa viwanda vilivyopo kupanua na kuongeza uzalishaji.
Semwaza alisema kuwa baada ya upanuzi huo wa viwanda vilivyopo na kujengwa kwa viwanda vipya uzalishaji sukari utaongezaka na kufikia tani 420,000 na zaidi kwa mwaka huo 2020/2021.
“Mpango uliopo ni kuzalisha sukari tani 420,000 na zaidi ifikapo mwaka 2020/2021 ili kukabiliana na upungufu wa sukari nchini lakini suala hilo litakuja na mabadiliko ya uendeshaji katika sekta hiyo ikiwemo ya mabadiliko ya muundo wa vyama vya wakulima wa miwa.”alisema Semwaza.
Semwaza alisema kuwa viwanda watalazimika kuwasaidia wakulima wadogo ili kuongeza uzalishaji huo ambapo kampuni ya sukari ya Kilombero ikiwekewa lengo la kuzalisha tani 180,000 kwa mwaka kufikia mwaka 2020/2021 baada ya kuboresha miundombinu katika kilimo cha miwa ambapo kwa sasa kinazalisha tani 130,000 za sukari kwa mwaka.
Akielezea juu ya muundo wa vyama vya wakulima wadogo wa miwa ulipo sasa, Semwaza alisema kuwa muundo huo umeonekana una mapungufu mengi na mwaka 2012 taasisi ya kuondoa umasikini Tanzania (Lepoa) ilifanya utafiti na kuona mapungufu yapi yanayodidimiza tija katika kilimo ambapo ulionekana una mapungufu mengi.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dk Kebwe Steven akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi mkuu wa bodi ya sukari Tanzania, Henry Semwaza na katikati ni mkuu wa wilaya ya Kilombero, James Ihunyo.
Akizindua mkutano huo na kutangaza kamati za kutoa elimu za kujadili mabadiliko hayo, Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven alisema kuwa elimu ya mabadiliko ya muundo wa vyama hivyo inapaswa kuwafikia wakulima wote wa zao la miwa.
Dk Kebwe alisema kuwa bodi ya sukari Tanzania na wadau wa tasnia ya sukari ina wajibu wa kutoa elimu kwa wakulima baada ya bunge la jamhuri wa Tanzania kupitisha sheria ya sekta ya miwa, vyama vya wakulima wa miwa wataingia moja kwa moja kwenye vyama vya ushirika.
“Hapo awali serikali ilikuwa inashindwa kuingia kwenye vyama vya miwa lakini baada ya bunge kusaini sheria hiyo vinaingia moja kwa moja katika mfumo wa vyama vya ushirika na huko serikali itakuwa na nguvu ya kufanya ukaguzi wa fedha kutokana na matakwa ya sheria.”alisem Dk Kebwe.
Dk Kebwe alisema kuwa kutokana na utendaji mbovu wa viongozi wa vyama vya wakulima wa miwa vya Ruembe Cane Growere Associations (RCGA) na Kilombero Cane Growere Associations (KCGA) uliopelekea kusimamishwa uongozi na waziri wa Kilimo mwaka jana kutokana na tuhuma mbalimbali, serikali tayari imempata mkaguzi Auditax International wa kukagua viongozi wa vyama hivyo.
Dk Kebwe alisema kuwa mkaguzi huyo tayari ameanza kazi (leo) jana ya kukagua mali za vyama hivyo baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wakulima wa miwa kuhusu utendaji mbovu wa viongozi hao.
“Mabadiliko ya miundo ya vyama hayana budi kufanyika kutokana na uwepo wa vyama 17 vya wakulima vinafanya kuwa na ugumu wa kuvisimamia lakini kuna uongozi mbovu na baadhi viongozi kujilimbikizia mali na kutumia vibaya fedha za vyama kwa kujinufaisha wenyewe.”alisema Dk Kebwe.
Mmoja wa wakulima zao la miwa mkoa wa Morogoro, Bakari Mkangano alisema kuwa wadau wa tasnia ya sukari hususani wakulima hawakushirikisha katika mchakato wa sheria sukari iliyopitishwa na bungeni hivi karibuni.
Mkangano alisema kuwa kupitishwa kwa sheria hiyo bila wao kushirikishwa wakulima wametishia kutotoa ushirikiano kwa kamati ya kujadili mabadiliko ya muundo wa vyama vya wakulima wa miwa kwa wananchi wakati wa mikutano ya hadhara ya kutoa elimu hiyo ya sheria ya sukari.
0 comments:
Post a Comment