BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HIVI NDIVYO MKUU WA UPELELEZI JESHI LA POLISI WILAYA YA KIBITI ALIVYOUAWA KINYAMA KWA KUMIMINIWA RISASI

WATU wasiofahamika, wamevamia kizuizi cha kutoza ushuru wa mazao ya misitu cha Jaribu Mpakani, wilaya ya Kibiti mkoani Pwani na kuua watu watatu, akiwamo Ofisa wa Polisi, baada ya kuwafyatulia risasi kinyama.

Habari zilizopatikana jana katika eneo la tukio, zilisema mauaji hayo yalitokea juzi usiku na hapakuwa na kitu chochote kilichoporwa au kuibiwa kutoka eneo hilo.

Habari hizo zilisema Ofisa wa Polisi aliyeuawa ni Mkuu wa Upelelezi wa wilaya hiyo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Peter Kubezya.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Boniveture Mushongi alisema katika taarifa yake jana kuwa Kubezya aliuawa katika majibizano ya risasi na majambazi hao, baada ya kupigwa risasi kiunoni.

Habari ziliwataja wengine waliokufa baada ya kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi ni Ofisa Uvuvi wilayani na mlinzi wa kituo hicho.

Ofisa Uvuvi aliyeuawa ametajwa kuwa ni Peter James na mlinzi ni Rashid Mgamba.

Aidha, taarifa kutoka chanzo cha kuaminika ndani ya Jeshi la Polisi zilisema Mrakibu Kubezya alikuwapo katika kizuizi hicho kusaidia operesheni maalum.

Mashuhuda wa tukio hilo waliiambia Nipashe kuwa lilitokea juzi saa 1:00, usiku baada ya watu wanne wakiwa na bunduki, kuvamia kituo hicho na kumuua mpelelezi mkuu huyo wa wilaya kwa kumpiga risasi tumboni.

Taarifa hazikuweza kubainisha Ofisa Uvuvi na mlinzi wa kituo hicho walipigwa risasi katika maeneo gani, lakini zilisema walifariki papo hapo.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, baada ya watu hao kufanya mauaji hayo, walikimbia na kutelekeza pikipiki mbili walizokuwa wanazitumia pamoja na kuacha kipeperushi kinachoeleza kupinga uwapo wa kizuizi cha ushuru wa mazao ya misitu, ikiwamo mkaa.

Kipeperushi hicho, ilidaiwa, kizuizi hicho kinadhulumu wananchi.

KITUO KIDOGO
Matukio ya majambazi kuua Polisi, hasa katika mkoa wa Pwani, si mara ya kwanza kujitokeza.

Juni 11, 2014, watu waliojifanya kuwa ni raia wenye kuhitaji msaada, waliingia kituo kidogo cha polisi Kimanzichana kwa kukimbia, wakiwa na silaha za jadi kabla ya kumkatakata askari Joseph Ngonyani na kupora bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 30.

Mbali na PC huyo, majambazi hao pi walishambulia askari wengine waliokuwa kituoni hapo kabla ya kupora SMG ya pili iliyokuwa na risasi 30 pia na risasi za akiba 41, na kutokomea kusikojulikana.

Ngonyani alifariki dunia alipokuwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.

Askari mwingine aliyetambulika wakati huo kama PC Venance alijeruhiwa mgongoni kwa risasi na mgambo aliyetambuliwa kwa jina la Mariam alijeruhiwa kichwani, shingoni na begani.

Miaka miwili iliyopita, majambazi 15 yaliyokuwa na silaha yalivamia Kituo cha Polisi cha Ikwiriri, Rufiji mkoani Pwani na kuua askari wawili na kupora silaha zilizokuwapo kituoni hapo.

Askari walioelezwa kupoteza maisha katika uvamizi huo ni Koplo Edgar aliyekatwa mapanga na WP Judith aliyepigwa risasi ubavuni upande wa kulia na kutokea upande wa kushoto.

Silaha zilizoporwa kituoni hapo zilikuwa SMG mbili, SAR mbili, shotgun moja na bunduki mbili za kufyatulia mabomu ya machozi. Majambazi hao pia waliiba risasi 60 za SMG kabla ya kutokomea kusikojulikana.NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: