BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAZIRI NAPE KULA SAHANI MOJA NA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM PAUL MAKONDA ?.

Mwenyekiti wa MOAT, Dk. Reginald Mengi (kushoto), akijadiliana jambo na Waziri Nape Nnauye (katikati) na Mkurugenzi wa Clouds Media Group,, Joseph Kusaga.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alifanya najisi alipovamia kituo cha habari usiku akiwa ameongozana na askari wenye bunduki.

Aidha, Waziri Nape amesema kwa kuwa kuna sheria, mikataba na katiba vinavyolinda uhuru wa vyombo vya habari, hatakiwi kuwapo ofisini endapo atashindwa kusimamia ukiukwaji usitokee.

Makonda, ambaye jana aliagizwa kuchapa kazi na Rais John Magufuli licha ya tuhuma dhidi yake, alivamia kituo cha televisheni cha kampuni ya Cloud Media Ijumaa usiku na kuingia ndani kwa nguvu akiwa ameongozana na polisi na wanajeshi wenye bunduki.

Akizungumza akiwa ameambatana na viongozi wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat) katika ofisi za Clouds jana, Waziri Nape alisema kitendo cha Makonda kuvamia chombo cha habari huku akiwa na silaha ni kunajisi uhuru wa habari jambo ambalo halikubaliki kokote.

“Kitendo cha namna hii kinanajisi uhuru wa vyombo vya habari," alisema Nape ambaye aliunda kamati ya watu watano kuchunguza tukio hilo jana na kutoa taarifa kwake leo.

"(Kamati itachunguza) kama amekifanya yeye (kitendo kile), (na) kwa namna gani.

"Ndiyo maana kamati inakwenda kutuletea matokeo … niseme tumezoea kuona matukio ya aina hii kwenye nchi ambayo imepinduliwa, watu wanakwenda studio na bunduki kutangaza kupindua nchi.

“Inapotokea kwenye nchi ambayo haijapinduliwa, Rais yupo, halafu watu wanaingia studio na bunduki inaleta sura ambayo siyo sawa sawa.

"(Makonda) anatakiwa kuendelea kuwapo au kutokuwapo, (lakini) kwanza tusubiri ripoti; halafu ipo mamlaka yenye dhamana naye, baada ya ripoti tutaona la kufanya.”

Waziri Nape alisema kamati hiyo itafanyakazi kwa saa 24 na kuwasilisha taarifa yake ambayo itawekwa hadharani kwa Watanzania.
"Hakitafichwa kitu chochote."

Habari zinasema Makonda alivamia kituo hicho saa 4:45 usiku akiwa ameambatana na askari sita wenye bunduki.

Akiwa kwenye jengo la televisheni hiyo, imedaiwa Makonda alikwenda kwenye moja ya studio zilizokuwa zikiendesha kipindi cha 'Shilawadu' na kuwalazimisha watangazaji kumpa nakala ya video ya mwanamke anayedaiwa kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, taarifa ambayo haikurushwa hewani siku hiyo.

Waziri Nape alisema amechukua hatua za haraka kwa tukio hilo kwa kuwa “tumeanza kuona dalili za hasa wanasiasa kukosa ngozi ngumu."

"Ukiwa mwanasiasa lazima ukubali kuwa na ngozi ngumu, nimefanya siasa kwa miaka 16.”

Alisema matukio ya udhalilishaji dhidi ya waandishi wa habari yanaanza kutokea nchini kama Arumeru, Kahama na maeneo mengine.

”Yanatokea kama vile kuna watu wanataka kuanza kuwa juu ya kila kitu, kwamba ukiwa mwanasiasa umepewa madaraka unaweza kuamua stori gani iende, stori gani isiende, ichapweje na iandikweje," alisema Nape.

"Hili halitavumilika nadhani ngojeni tupate matokeo ya utafiti huu halafu tutachukua hatua na hapo mtaona tunaheshimu uhuru wa habari kwa kiasi gani.

"Vinginevyo sitakiwi kuwapo kama vyombo vya habari havitakuwa na uhuru wa kutosha maana sheria, mikataba na katiba ipo. Kinachotakiwa ni usimamizi, nikishindwa hayo sitakiwi kuwapo.”

KUOMBA RADHI
Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group Ltd, Joseph Kusaga alimtaka Makonda kuomba radhi.

"Hakuna binadamu ambaye ni msafi, lakini lazima akiri kwamba kitendo kilichofanyika siyo sahihi. Kama akiomba radhi ataendelea kuwa rafiki yetu.”

Hata hivyo, akizungumza katika uzinduzi wa maungano ya badarabara Ubungo, jijini Dar es salama jana, Rais John Magufuli alimtaka Makonda kuchapa kazi licha ya tuhuma hizo za kuvamia kituo cha televisheni na utata wa taaluma yake.

Awali, Mwenyekiti wa Moat, Dk. Reginald Mengi, alisema jambo hilo ni hatari, linaogopesha na linatishia maisha ya waandishi wa habari huku akimpongeza Waziri kwa kuunda kamati na kwamba wanasubiri matokeo na kujua ukweli wa pande zote mbili.

“(Kamati mseme) zaidi mtachukua hatua gani," alisema Dk. Mengi. "Isiishie tu kwamba tutagundua ilikuwa hivi na hivi basi, tunataka kufahamu ni hatua gani zitachukuliwa ili tujisikie tuna usalama.

"Kama hatua hazitachukuliwa ipo siku nyingine atakuja na helikopta na kutua juu ya studio za Clouds ama mbinu nyingine yoyote. Matokeo ya uchunguzi yaiishie kwenye hatua za kuhakikisha kitu kama hiki hakitatokea tena.

“Chochote kitakachoamuliwa ni lazima kuwe na ‘formal apology’ (uombaji radhi rasmi) kwa Clouds na watu wake... Clouds walikuwa wanafuata kanuni za uandishi wa habari na watu wake. Yeyote aliyehusika aseme hatarudia tena.”

Dk. Mengi alisema kwa imani yake, Rais Magufuli anapenda waandishi wa habari, wananchi na Waziri pia anayewapenda sana, lakini ni vyema mapenzi hayo yakaonyeshwa kwa vitendo.

“Sifa moja ya mwandishi wa habari ni kutokuwa muoga," alisema zaidi Dk. Mengi. "Hili lisiwaogopeshe mkaacha kufanyakazi zenu kama kawaida. Uwoga ni adui mkubwa wa mwandishi wa habari almradi anafanya kihalali na kufuata kanuni za tasnia.” 


Kamati ya Nape itaongozwa na Mwenyekiti Dk. Hassan Abbas ambaye ni Mkurugenzi Idara ya Habari MAELEZO na wajumbe wake ni Deodatusi Balile ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Jesse Kwayu ambaye ni Mhariri Mtendaji wa zamani wa Nipashe, Mengida Johannes kutoka Wapo Redio na Mabel Masasi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano(TCRA).NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: