BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAWENZI MARKET FC JONGOO WA MJINI ALIVYOTINGA LIGI DARAJA LA KWANZA MOROGORO

Wachezaji wa klabu ya Mawenzi Market FC wakiwa wamemnyanyua kocha wao msaidizi, John Tamba juu mara baada ya timu hiyo kufuzu kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao na kukusanya pointi tisa baada ya kuifumua JKT Oljoro bao 2-0.
 

Na Juma Mtanda, Morogoro
Ligi daraja la pili Tanzania bara msimu wa mwaka 2016/2017 imehitimishwa kwa timu tatu kufuzu kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao wa mwaka 2017/2018 baada ya kumalizika kwa michezo ya hatua ya nne bora ya ligi hiyo wikiendi iliyopita viwanja viwili vya Kambarage Shinyanga na jamhuri Morogoro.

Katika uwanja wa Kambarage Nyerere wenyeji Transit Camp FC ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Cosmo Politani FC ya Dar es Salaam wakati uwanja wa jamhuri Morogoro JKT Oljoro FC ilijikuta ikitandikwa bao 2-0 na Mawenzi Market FC.

Timu tatu zilizofuzu kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao baada ya kumalizika kwa ngwe ya michezo ya hatua ya nne bora ni pamoja na Transit Camp, Mawenzi Market FC na JKT Oljoro na Cosmo Politani ikishindwa kufuzu.

Transit Camp FC na Mawenzi Market FC zimemaliza zikiwa na pointi sawa (9) zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa wakati JKT Oljoro FC ilimaliza kwa kuwa na pointi nane huku Cosmo Politani ikiishia na pointi zake saba.

Hatua hiyo ya michezo ya nne bora imetokana na timu hizo kufanya vizuri na kuongoza katika hatua ya awali ya makundi ya manne ya A, B, C na D.

Katika uwanja wa jamhuri Morogoro wenyewe Mawenzi Market FC ilihitaji kupata ushindi katika mchezo wao na JKT Oljoro na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 2-0 katika mchezo mkali ulioshuhudia kipindi cha kwanza kikimalizika bila nyavu kutikiswa.

Mlinzi wa Mawenzi Market FC maarufu majogoo wa mjini, Berbato Mgotwa aliipatia timu yake bao la kuongoza dakika 52 baada ya mpira wa kona aliouchonga na kujaa wavuni moja kwa moja.

Mawenzi Market FC walijihakikishia ushindi huo kwa kufunga bao la pili lililofungwa na mshambuliaji wao tegemeo, Hamis Mkopi dakika ya 81 baada ya kupokea pasi ya Hassan Ngozi na kufumua shuti la chini akiwa eneo la hatari.

Juhudi za washambuliaji wa JKT Oljoro FC kupata ushindi katika mchezo huo zilikwamishwa na safu imara ya ulinzi ya Mawenzi Market FC iliyokuwa ikiongozwa na nahodha wao, Juma Senkubo na kuondoa mipira yote ya hatari iliyokuwa ikielekea lango lao lililokuwa likilindwa na kipa, Omary Omary.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo kilianza kwa kila timu kufanya mashambulizi ya kustukiza huku Mawenzi Market FC ikionekana wachezaji wake wana uchu zaidi ya kupata bao lakini safu ya ulinzi ya JKT Oljoro ilikuwa imara na kuwadhibiti washambuliaji hao.

JKT Oljoro iliyokuwa ikijilinda zaidi katika mchezo huo ilipoteza nafasi chache kwa washambuliaji wake kupachika mabao na kujikuta wakiambulia kipigo cha bao 2-0 katika dakika ya 52 na 81.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: