BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

IPTL YAMPONZA MKURUGENZI WA EWURA, ATUMBULIWA USIKU NA WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA


DUDE hatari la IPTL. Ndivyo unavyoweza kusema wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi.

Hatua hiyo imechukuliwa siku chache baada Ewura kutangaza kuwa ingeanza kupokea maoni na mapingamizi ya wadau mbalimbali kuhusu kuongezewa muda wa leseni kwa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Taarifa ya Waziri Mkuu iliyotolewa usiku wa kuamkia jana saa 7:08 usiku kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kusimamishwa kwa kigogo huyo ingawa haikueleza sababu za kuchukuliwa hatua hiyo.

“Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi kuanzia leo (jana) Juni 11, 2017,” ilieleza taarifa hiyo.

Wiki iliyopita Ewura ilitoa tangazo ikieleza ilikuwa imepokea maombi ya IPTL ya kutaka iongezewe muda leseni yake ya kuuza umeme nchini.

Wadau mbalimbali wakiwamo wanasiasa, walipinga hatua hiyo kutokana na jinsi IPTL ilivyokwisha kuibua mjadala mzito nchini kiasi cha kusababisha baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali ya Awamu ya Nne kuwajibishwa kwa tuhuma za kupokea mamilioni ya fedha kutoka kwa kampuni hiyo kinyume na sheria.

Kampuni ya IPTL imekuwa ikiiuzia umeme Tanesco huku utata wa bei ya umeme huo ukitawala jambo lililosababisha Bunge la 10 kuazimia ifukuzwe nchini na kunyang’anywa mitambo.

EWURA YASIMAMISHA USIKU
Muda mfupi baada ya Waziri Mkuu kumsimamisha kazi Ngamlagosi, mamlaka hiyo ilitoa taarifa saa 8:02 usiku wa kuamkia jana ya kusimamisha mchakato wa kushughulikia maombi hayo ya IPTL ya kuongezewa leseni.

“Ewura inasimamisha mchakato wa kushughulikia maombi ya leseni ya mwombaji ikiwa ni pamoja na upokeaji wa maoni/mapingamizi dhidi ya maombi hayo mpaka hapo yatakapotolewa maelekezo mengine,” ilieleza taarifa hiyo.

Alipotafutwa, Kaimu Meneja Mawasiliano wa shirika hilo, Leila Muhaji, kujua kama hatua hiyo ya kusimamisha mchakato wa utoaji leseni kwa IPTL utaathiri upatikanaji wa umeme alisema: “Hatua hiyo haitaathiri kwa namna yoyote ile kwa sababu umeme upo wa kutosha” .

ZITTO
Naye Mbunge Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema inawezekana mpango wa kuongeza muda wa leseni ya IPTL akawajibishwa mtu wa Ewura kwa kuwa ndiye aliyetoa tangazo hilo.

“Lakini huyo mtu wa Ewura anaweza kuwa ameshinikizwa, mimi naamini Rais kwa jinsi alivyo hawezi kuwa anahusika na haya matapeli.

“Lakini Rais mtumbuaji anakaaje miezi 20 kwenye kiti cha enzi bila kumaliza suala la IPTL ilhali kuna maazimio ya Bunge yanayopaswa kutekelezwa?

“Nawapa kazi ndogo Watanzania, watazame lile tangazo la Ewura kuhusu IPTL. Tazameni umiliki na wamiliki wa IPTL hivi sasa.

“Kuna hisa asilimia 16 kwa kampuni mbili zenye majina ya ujanja ujanja. Kina nani hao wamegawiwa hizo hisa tena wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli?

“Kwenye kesi ya Standard Chartered Bank dhidi ya Tanesco huko Mahakama ya ICSID ambako Tanesco wanatakiwa kulipa Sh bilioni 352 kwa benki hiyo, wanasheria wa Tanesco na wale wa PAP/IPTL wanashirikiana kwa karibu mno.

“Kwenye rufaa, Tanesco wametakiwa waweke fedha hizo kwanza kwenye akaunti ya benki ya nje kabla ya rufaa kusikilizwa.

“PAP/IPTL wanalinda ufisadi wao kwa kujifanya wanashirikiana na Tanesco kwenye kesi. Kwenye taarifa ya PAC kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow tuliweka wazi kuwa PAP/IPTL waliweka dhamana kuwa ikitokea madai yoyote yale dhidi ya Tanesco basi PAP/IPTL italipa.

“Kwa nini Serikali isitumie ile indemnity kuwataka PAP kulipa hizi fedha? Kwa nini Serikali inayosema inapambana na ufisadi inawakumbatia mafisadi wa PAP/IPTL?

“Kwa nini Serikali iliyoonyesha ujasiri wa kupambana na Kampuni kubwa kama Acacia/Barrick inayumbishwa na matapeli hawa; tena tapeli mmoja tu Harbinder Singh Seth?

“Huko ICSID shirika letu la Tanesco kupitia wanasheria wake wamepeleka hoja kwamba maazimio ya Bunge kuhusu Tegeta Escrow hayana msingi wowote wa sheria na kwamba Bunge linapiga porojo tu.

“Wanasheria hawa wameomba Ofisi ya Bunge iwape barua kuthibitisha kuwa uamuzi wa Bunge hauna msingi wowote na ni maoni tu yanaweza kudharauliwa na kutupiliwa mbali. Shirika la umma linalosimamiwa na Bunge linapeleka barua kwenye vyombo vya ubeberu kuwa Bunge ni porojo tupu?” aliuliza Zitto.

MBOWE ALIIBUA TENA
Mei 11 mwaka huu, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliihoji lini Serikali itatoa majibu ya maazimio mbalimbali yaliyotolewa bungeni kutokana na muda kupita.

Mbowe aliyataja baadhi ya maazimio hayo kuwa ni ya Tokomeza, Escrow na IPTL pamoja na mabilioni ya Uswisi, kwamba muda mrefu umepita bila serikali kutoa majibu.

Kutokana na swali hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema wakati ukiwadia atatoa majibu ya maazimio mbalimbali yaliyotolewa na wabunge hapo bungeni.

“Natambua vikao mbalimbali vilitoa maazimio yanayotaka serikali ilete maelezo kwa baadhi ya maeneo na mambo uchunguzi lakini mambo hayo yanahitaji muda ili kuleta maelezo hapa bungeni,” alisema Waziri Mkuu wakati akijibu swali la papo kwa hapo lililoulizwa na Mbowe.

MITAMBO YA MAFUTA
Pamoja na Serikali kuagiza kubadilishwa mitambo yote ya umeme ibadilishwe iweze kutumia gesi, Kampuni ya IPTL bado haijafanya hivyo kwa mujibu wa tangazo la Ewura.

Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ilitakiwa kuipa IPTL Sh bilioni 100 kuanza mchakato wa kubadili mitambo iweze kutumia gesi.

Hata hivyo hatua hiyo ilipingwa na wananchi na hakuna fedha iliyotolewa na mitambo hiyo inaendelea kutumia mafuta hadi sasa, umeme wake ukitajwa kuuzwa kwa gharama kubwa.

WADAU WAJIPANGA
Baada ya taarifa ya Ewura kuwapo mchakato kuhusu IPTL kupewa leseni, wadau mbalimbali walitangaza kupinga uamuzi huo huku wajipanga kuhamasisha wananchi kuweka mapingamizi.

Hatua hiyo ni kama njia ya kupinga kampuni hiyo kupewa leseni kwa jinsi ilivyoibua mjadala mzito katika Bunge la 10 hasa kutokana na umiliki wake na namna ilivyouzwa.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: